Featured Post Today
print this page
Latest Post

NYOSSO ASEMA YANGA WALITOKA KIBAHATI MKWAKWANI

NYOSSO AKIMDHIBITI KAVUMBAGU HIYO JUZI

Beki wa Coastal Union, Juma Said Nyosso amesema Yanga walikuwa na bahati zaidi katika mechi yao jana.


Nyosso amesema walikuwa na nafasi kubwa ya kuifunga Yanga kwa kuwa waliizidi sana.
Lakini akasisitiza katika suala la mpira, ni vigumu kwa kulazimisha kitu ambacho hakiwezekani.

“Tulijitahidi kadiri ya uwezo wetu, tulikuwa katika nafasi nzuri ya kuifunga Yanga ingawa naweza kusema mambo yalikataa tu.

“Sisi ndiyo tulicheza vizuri zaidi siku hiyo, lakini bahati haikuwa yetu,” alisema beki huyo wa zamani wa Simba.
0 comments

LOGARUSIC ATAKA WANAJESHI WASIOKATA TAMAA


Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic amesema anataka kuwa na wachezaji wenye moyo wa ushindani na wasiokubali kushindwa.


Logarusic amesema anaamini kuwa na washindani katika kikosi chake ni jambo la msingi zaidi, na haamini watu wanaokata tamaa mapema.
“Kama unakata tamaa mapema, basi hauwezi kufanya kazi na mimi. Nataka wapambanaji.

“Katika maisha kuna mawimbi, hauwezi kusafiri baharini bila ya kukutana na mawimbi. Ukikata tamaa mapema, hautafika unapokwenda.”
Logarusic anaamini kuwa mmoja wa makocha wakorofi lakini amekuwa akisifika kwa kusimamia suala la nidhamu.

Tokea ametua Simba, inaonekana suala la nidhamu limeimarika zaidi na watukutu wamekuwa na hofu.
0 comments

SERIKALI YATAKIWA KUONDOA KWENYE VIFAA VYA UJENZI WA NYUMBA.

SERIKALI YATAKIWA KUONDOA KWENYE VIFAA VYA UJENZI WA NYUMBA.

MWENYEKITI  wa kamati ya   kudumu ya Bunge ya  Ardhi, Maliasiri na Mazingira James Lambeli


Na Elizabeth Kilindi,Mkinga.

MWENYEKITI  wa kamati ya   kudumu ya Bunge ya  Ardhi, Maliasiri na Mazingira James Lambeli, ameitaka serikali kuondoa kodi  kwenye vifaa vya  mradi wa ujenzi wa nyumba za  gharama  nafuu unaoendeshwa na Shirika la Nyumba Tanzania (NHC)  ili kumuwezesha mwananchi wa hali ya chini kuondokana na makazi duni.

Lembeli aliyasema hayo  baada ya  taarifa ya mradi huo iliyosomwa hapo juzi, mbele ya kamati hiyo na Kaimu Mkurugenzi wa uendeshaji wa shirika hilo, Benedict  Kilimba na kueleza kuwa kodi za serikali zimesababisha  bei ya nyumba hizo kuwa kubwa.


Kwamujibu wa taarifa hiyo  ni kwamba  mfumo  wa kuwataka  wanunue  vifaa vya ujenzi  kwenye maduka maalumu kumeongeza  gharama ya ujenzi huo  na kufikia tsh mil, 31.3 kwa nyumba  yenye vyumba viwili na tsh mil, 35.3 hadi tsh mil, 36.2 kwa vyumba vitatu  bila VAT.

Aidha Kilimba alisema kuwa  mbali na changamoto hizo  shirika pia linalazimika kuilipa serikali kiasi cha tsh mil, 7 mpaka tsh mil, 10  kama kodi  ya ongezeko la thamani VAT   kutokana  na  manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa kila nyumba jambo lililosababisha nyumba hizo kuuzwa  tsh mili, 40. 7  kwa  nyumba ya vyumba viwili na tsh million 46. 3 hadi  tsh mil, 48.2  kwa vyumba vitatu.

Hata hivyo  alieleza kuwa  kama shirika litaruhusiwa kutafuta maduka yenye unafuu na  serikali ikaondoa  kodi ya VAT  mauzo ya nyumba hizo yangeweza kufikia tsh mili, 28  bei ambayo mtu wa hali ya chini angeweza kuimudu tofauti na ilivyo  sasa.

Akizungumza baada ya taarifa hiyo, Lembeli alisema ni wajibu sasa kwa serikali kuonyesha moyo wa dhati katika kuwawezesha wananchi kumudu kubadilisha maisha yao ikiwemo hili la makazi bora ambayo ni haki ya kila mtu.

Aliahidi kubeba jukumu la kuishauri serikali kuondoa kodi ya VAT  kwenye  vifaa vya ujenzi wa nyumba zinazojengwa na mradi wa shirika hilo hasa zile zilizolengwa kwa ajili ya  makazi bora kwa watu wa hali ya chini.

“Jamani sisi wanakamati yetu tumetembea katika nchi mbalimbali kama vile nchi ya Singopore, tumejionea na  kujifunza jinsi serikali ya nchi hiyo inavyowawezesha watu wake katika makazi bora……..takriban asilimia 90 ya nyumba zilizojengwa na serikali ya nchi hiyo zimeuzwa kwa wananchi kwa bei nafuu, vipi sisi huku!” alihoji Lembeli.

Hata hivyo alidai kuwa taarifa ya shirika hilo kuhusu mazingira ya ujenzi wa nyumba hizo inaonyesha kwamba mtu wa kawaida hatakuwa na uwezo wa kuzinunua kutokana na ukubwa wa bei jambo alilolieleza kuwa linaondoa maana halisi ya azma iliyokusudiwa na serikali yenyewe ama wananchi walalahoi.
0 comments

Diwani aliyewekwa ndani na DC ajiuzulu

Diwani aliyewekwa ndani na DC ajiuzulu 


DIWANI wa Kata ya Mswaha-Darajani, Tarafa ya Mombo, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga (CCM), Aweso Kipaku (34), amejiuzulu nafasi hiyo akipinga hatua ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Mrisho Gambo, kumuweka ndani.

Akizungumza na mwandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Kipaku alisema Bw. Gambo aliagiza awekwe ndani Januari 24 mwaka huu, saa 11 jioni na kupata dhamana saa nne usiku.
Alisema polisi walimkamata, kumpeleka Kituo cha Korogwe lakini Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani, alikwenda kumuwekea dhamana na kufanikiwa kutoka.
Mbali ya Kipaku, wengine waliokamatwa na kuwekwa ndani ni Ofisa Mtendaji Kijiji cha Mswaha-Darajani, Bw. Abbas Siafu na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mswaha-Darajani, Bw. Said Kijiwa.
Chanzo cha kukamatwa kwao ni tuhuma zilizotolewa dhidi yao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya wakidaiwa kuchochea mgogoro wa wakulima na wafugaji kwenye Kijiji cha Mswaha-Darajani.
"Juzi tuliitwa kwa Mkuu wa Wilaya na viongozi wenzangu, baada ya kumalizika Kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Wilaya (Gambo) alimuamrisha OC-CID anichukue na kuniweka ndani hadi nilipopata dhamana usiku.
"Najiuliza mimi kiongozi wa wananchi nadhalilishwa kwa kufungwa pingu, kukaa chini tena nikisukumwa, je, wananchi wangu wapo salama kiasi gani... nimeamua kujiuzulu nafasi ya udiwani kwa vile nimedhalilishwa sana," alisema.
Kipaku alisema tayari ametoa taarifa ya kujiuzulu kwake kwa Katibu wa CCM mkoani humo, Gustav Muba jana ambapo zaidi ya wanachama 300 wa chama hicho wanaomuunga mkono wamerudisha kadi.
Aliongeza kuwa, sababu iliyomfanya awekwe ndani ni kitendo cha kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Kijiji uliofanyika Januari 21 mwaka huu na kudaiwa anachochea mgogoro wa wakulima na wafugaji.
"Wakulima wanataka wafugaji waondoke wakidai mifugo yao inakula mazao...Gambo aliahidi angekwenda kusimamia kazi ya kuwaondoa wafugaji kwenye eneo husika lakini hakufanya hivyo mara tatu, leo hii anasema sisi viongozi wa kata ndiyo tufanye kazi hiyo kana kwamba tuna Jeshi la Polisi," alisisitiza.
Alisema Januari 22 mwaka huu, watu wasiojulikana walikwenda kuchoma moto mazizi ya wafugaji lakini chanzo si viongozi wa kata ni viongozi wa Wilaya na Mkoa ambao wamechelewa kuchukua hatua za kumaliza mgogoro husika.
Juhudi za Majira kumpata Bw. Gambo kuzungumzia sakata hilo zilishindikana ambapo juzi alipigiwa simu lakini ilipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Alhajj Majid Mwanga akidai wapo Tanga kwenye kikao na kuhoji mnataka kuzungumza na Mkuu wa Wilaya kwa suala lipi.
Jana simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa ambapo Katibu wa CCM mkoani humo, Muba alikiri kupokea taarifa ya kujiuzulu diwani huyo lakini hakuwa tayari kuzungumza lolote akidai bado hawajajadili uamuzi wake kama wamkubalie au wamkatalie.
"Nimepewa taarifa hiyo lakini tunasubiri barua rasmi, sisi kama chama lazima tumjadili na turidhike na kile kilichofanya ajiuzulu, kama hakina mashiko tunajadiliana na kumuomba aendelee kuwa diwani," alisema Muba

Chanzo;Majira

0 comments

Serikali kuendeleza viwanda nchini

Serikali kuendeleza viwanda nchini

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda 
SERIKALI imeahidi itaendelea kusaidia sekta ya viwanda, hususani vya ndani kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, ili kuhakikisha vinasaidia kutoa mchango katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii.
Akizumgumza katika sherehe ya kukabidhiwa nyumba mbili za kisasa zilizotolewa msaada na Kampuni ya Saruji Tanga (TCCL) kwa ajili ya watumishi wa gereza la Maweni, mkoani hapa mwishoni mwa wiki, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, alisema wizara yake itahakikisha viwanda vya ndani vinapata faida, ili viweze kuchangia maendeleo ya jamii zinazowazunguka.
Alisema serikali inafahamu viwanda vya uzalishaji nchini vinachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya jamii kupitia programu za huduma za kusaidia jamii, na kwamba katika siku za karibuni vimeonyesha matokeo chanya.
“TCCL wamekuwa mstari wa mbele kusaidia na kuchangia jamii kwa madhumuni ya kupunguza umaskini, hasa katika maeneo ya vijijini.
“Tanga Cement wameonyesha mifano ya wazi kabisa kwamba viwanda vya wazawa na wageni wanaokuja kuwekeza nchini wanaweza kuwa na mahusiano mazuri na wenyeji wanaozunguka kiwanda husika,” alisema Dk. Kigoda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji Tanga (TCCL), Reinhardt Swart, alisema kampuni yao wanaelewa programu ya huduma ya kusaidia jamii ni kurudisha fadhila kwa jamii baada ya kufanya au kuwauzia bidhaa zao.
Alisema mwaka jana kupitia programu za huduma za kusaidia jamii, TCCL wametumia takribani sh milioni 327 kwa kujenga na kukarabati shule, zahanati na kusaidia miradi mbalimbali ya jamii nchini.
Aliongeza kuwa hivi karibuni kampuni hiyo imemalizia ujenzi wa maabara ya sayansi kwa Shule ya Sekondari Pongwe na wanatarajia kukabidhi maabara hiyo kwa uongozi wa shule.
Kamishina Msaidizi Mwandamizi (SACP) wa Jeshi la Magereza, Augustino Mboje, alisema jeshi hilo mkoani Tanga linawashukuru viongozi na wafanyakazi wa kiwanda hicho kwa msaada huo kwa sababu utachochea ufanyaji kazi kwa maofisa wa magereza
 
Chanzo;Tanzania Daima 
0 comments

Kikwete ataka kilimo kutumia teknolojia mpya

Kikwete ataka kilimo kutumia teknolojia mpya

kikwete1 243ba

Rais Jakaya Kikwete amesema ili kuhakikisha sekta ya kilimo inapiga hatua lazima ugunduzi wa teknolojia mpya zinazogunduliwa zitumike kwa vitendo. 

Rais Kikwete alisema bila kuviwezesha vituo vya utafiti na kuwatumia wataalamu wengi wa kilimo kama mabwana na mabibishamba, sekta hiyo haitapiga hatua.

Alikuwa akifungua mkutano wa wadau wa kilimo na biashara kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya, jana.
Alisema uhifadhi wa vyakula katika maghala hauridhishi, kutokana na asilimia 30 ya mazao yanayohifadhiwa huharibika jambo ambalo linaweza kuepukika likitafutiwa ufumbuzi.

"Tunatakiwa kutumia ugunduzi wa teknolojia mpya zinazogunduliwa ndani na nje ya nchi kwa vitendo, ili kusaidia kuboresha kilimo nchini jambo ambalo linawezekana tukiamua hasa kwa kushirikiana na wadau wengine," alisema Rais Kikwete.
Alisema wakulima wengi hususan wadogo wanatakiwa kupewa elimu jinsi ya kulima mazao ambayo yanaendana na udongo wa eneo husika, kazi ambayo inatakiwa kufanywa na mabwana na mabibishamba na wadau wa kilimo.

"Pia, rasilimali fedha na watu katika vituo vyetu vya utafiti wa kilimo vinahitaji kuongezewa nguvu, ili kufanya tafiti nyingi na zitakazoweza kusaidia kutatua matatizo," alisema.
yanayowakumba wakulima wengi."

Awali akimkaribisha Rais Kikwete, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza alisema aliwataka washiriki wa mkutano huo kujadili jinsi ambavyo wataweza kuwasaidia wakulima wadogo kuondokana na matatizo yanayowakumba kwa kutumia gunduzi za kisasa zinazovumbuliwa.

 Chanzo: Mwananchi
0 comments

Majalada kesi yasombwa na mafuriko Moro

Majalada kesi yasombwa na mafuriko Moro

janwani1 bb2a6

Wakati Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Magole, Fredy Mbogela akisema kesi zote zilizokuwa zikisikilizwa katika mahakama hiyo ambayo imesombwa na maji pamoja na mafaili yote, zitaanza upya, Mkuu wa Wilaya na Mkoa wa Morogoro wanahaha kukusanya takwimu za waathirika wa mafuriko. (HM)
Mafuriko makubwa yalitokea katikati ya wiki iliyopita Kijiji cha Magole, huku yakisababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu. Pia, mafuriko hayo yalisomba majalada ya kesi mbalimbali mahakamani hapo.

Akizungumza, Hakimu Mbogela alisema hivi sasa kesi zote za jinai zilizokuwa zikisikilizwa mahakamani hapo zitafunguliwa na kusomwa na kusikilizwa upya.
"Polisi ndiyo watakaofungua na kuzipeleka kesi hizo katika mahakama hiyo, kwa sababu wao wanazo kumbukumbu za kesi hizo kupitia kwa waendesha mashtaka na wapelelezi," alisema Hakimu Mbogela na kuongeza:
"Hakuna kesi itakayofutwa kutokana kuharibiwa majalada hayo, kama nilivyosema polisi watazileta kesi mahakamani, hata kama kulikuwa na kesi iliyokuwa imekaribia hukumu
itaanza upya." alisema.


Alisema: mahakama itaanza kufanya kazi baada ya kufanyiwa usafi na kuweka samani.
Alisema hatua ya awali ambayo inaendelea kufanywa, ni kusafisha jengo la mahakama hiyo ndani na nje kwa kutoa matope, magogo ya miti na taka nyingine ambazo zilikwama eneo hilo na kwamba, utaratibu wa utendaji unaendelea kufanywa.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Nestory Munjunangoma alisema Idara ya Mahakama kwa kushirikina na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wapo kwenye mchakato wa ukaguzi na tathmini ya uharibifu wa jengo la mahakama hiyo.

Munjunangoma alisema hivi sasa jitihada za kufanya ukaguzi na upembuzi yakinifu zinafanyika kabla ya TBA kutoa ushauri kulingana na uharibifu uliotokea kamajengo hilo linaweza kukarabatiwa ama kujengwa upya.

Alisema hivi sasa shughuli za mahakama hiyo zimesimama, kuruhusu usafi wa mazingira. Chanzo: mwananchi
0 comments

Deni la Taifa linapaa, serikalini ni matanuzi

Deni la Taifa linapaa, serikalini ni matanuzi

bot1 52cbf

Hivi karibuni The Citizen liliandika habari ya kushtua katika ukurasa wa mbele, likielezea wasiwasi wa wataalamu na mabingwa kadhaa wa masuala ya uchumi kuwa, Tanzania inakabiliwa na janga kubwa la mzigo wa madeni iwapo Serikali haitapunguza kasi ya mikopo isiyokuwa na tija katika kuinua uchumi. 

Onyo la wataalamu hao linatukumbusha jinsi janga la Deni la Taifa lilivyoligharimu Taifa kiuchumi katika miaka ya 90, ambapo karibu rasilimali zote ambazo Serikali ingezitumia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na pia kuziwekeza katika huduma muhimu za kijamii zilielekezwa katika kulipa madeni. Ni aibu na ukweli ulio mchungu kwamba ilipofika mwaka 2006, Deni la Taifa lilikuwa asilimia 70 ya Pato la Taifa, ingawa msamaha wa madeni ulipunguza kiwango hicho hadi asilimia 21 mwaka uliofuata.
Hata hivyo, kilichoendelea baada ya pale ni uthibitisho kwamba Serikali haikupata fundisho kutokana na janga hilo, kwani ilizidisha kasi ya kukopa kiasi kwamba
Deni la Taifa hivi sasa linakadiriwa kuwa kati ya asilimia 40 na 50 ya Pato la Taifa, ambalo linakadiriwa kuwa Sh50 trilioni. Ni vigumu kuamini kwamba Deni la Taifa limekua kwa kasi ya kutisha kutoka Sh10 trilioni mwaka 2005 hadi Sh27 trilioni mwishoni mwa mwaka uliopita.


Kama baadhi ya wataalamu wa masuala ya uchumi wanavyohadharisha, suala hapa siyo Serikali kukopa, bali ni kwamba mikopo hiyo inayokadiriwa kuwa Sh2 trilioni kila mwaka inachukuliwa kufanya kitu gani? Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zinaonyesha kwamba Deni la Taifa lilipaa kwa Tsh5 trilioni kati ya Januari na Oktoba mwaka uliopita.

Mtaalamu mmoja wa uchumi ametukumbusha jinsi miaka ya 70 Serikali ilivyokopa Sh96 bilioni kuanzisha Kiwanda cha Viatu Morogoro, lengo likiwa kuuza viatu nchini Italia. Kutokana na kufilisika kilibinafsishwa miaka ya 90 na hivi sasa majengo yake yamegeuzwa kuwa ghala, huku deni la uanzishwaji wa kiwanda hicho likiwa limelipwa kupitia kodi za wananchi. Mfano mwingine ni bajeti ya Sh122.4 bilioni ya kusambaza pembejeo za ruzuku kwa wakulima kwa mwaka 2011/12, ambapo Tsh89 bilioni zilikuwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imefichua uvundo na ufisadi mkubwa katika mfumo mzima wa pembejeo za ruzuku. Kwa hiyo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inakutana leo kupokea na kujadili ripoti hiyo. Kwa mfano, katika Kijiji cha Lunyala
, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa asilimia 70 ya wananchi walioorodheshwa kupata mbolea walikuwa bandia, huku Benki ya Dunia ikikaririwa ikisema asilimia 60 ya Bajeti ya pembejeo za ruzuku ililiwa na mafisadi.


Kinachosikitisha ni kwamba Deni la Taifa litalipwa na wananchi wote ingawa waliofaidika nalo ni mafisadi na viongozi wachache walio serikalini na mashirika ya umma. Lakini kinachosikitisha zaidi ni tabia ya Serikali kuendelea kukopa kwa lengo la kuendeleza matanuzi na matumizi makubwa yasiyo ya lazima.

Mfano mzuri ni ziara fupi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mkoani Mtwara mwishoni mwa wiki, ambapo aliongozana na ujumbe mkubwa kupita kiasi na magari ya kifahari ya Serikali yasiyopungua 30. Sisi tunadhani unahitajika mjadala mpana wa kitaifa kuhusu Deni la Taifa.

Chanzo: mwananachi
0 comments

MKWAKWANI KUKARABATIWA TENA BAADA YA KUMALIZIKA MZUNGUKO WA PILI WA LIGI KUU

MKWAKWANI KUKARABATIWA TENA BAADA YA KUMALIZIKA MZUNGUKO WA PILI WA LIGI KUU


Na Oscar Assenga, Tanga.
UONGOZI wa Uwanja wa Mkwakwani umesema awamu ya pili ya ukarabati wa uwanja huo unatarajiwa kufanyika mara baada ya kumalizika mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara mwaka huu lengo lao likiwa ufikie kwenye viwango vya kitaifa na kimataifa.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga,
  Gustav Mubba wakati akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo ambapo alisema suala la ukarabati wa uwanja huo ni mkakati wao waliojiwekea kila mwaka.


Mubba alisema mara baada ya uwanja huo kumalizika mashabiki wa soka
  mkoani hapa wanapaswa kuwa na nidhamu kwa kuacha kuingia uwanjani wakati mchezo ukiwa umalizika kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha uharibifu wa vitu vilivyopo uwanjani hapo.    “Napenda kuwaomba mashabiki wa soka baada ya kumalizika mpira wawe na nidhamu waache kuingia uwanjani baada ya kumalizika mechi kwani baadhi yao wanachana nyavu za magoli kitendo ambacho kinaleta usumbufu mkubwa sana “Alisema Mubba.

Aliwataka mashabiki wa soka wajifunze nidhamu ya matumizi ya uwanja
  hasa kwenye mechi ya Yanga na Coastal Union wa wale wanaotokea Dar es Salaam na mikoa mengine kuja kushuhudia mechi hizo wawe wastaharabu na kuacha kuleta vurugu.
0 comments

DK.KIGWANGALLA HATARINI KUVULIWA UANACHAMA CCM

DK.KIGWANGALLA HATARINI KUVULIWA UANACHAMA CCM

Dar es Salaam. Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangalla yuko hatarini kuvuliwa uanachama wa chama hicho, hatua ambayo endapo itachukuliwa itasababisha apoteze nafasi yake ya ubunge.

Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Nzega mkoani Tabora tayari umemjadili Dk Kigwangalla katika vikao vyake vya Kamati za Usalama na Maadili na Kamati ya Siasa, kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu wa mbunge huyo.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana jioni zinasema baada ya vikao hivyo vilivyofanyika Januari 11 mwaka huu, imeazimiwa kuwa suala la Dk Kigwangalla pamoja na madiwani watano wilayani humo lipelekwe katika ngazi ya CCM mkoa na baadaye taifa.

Dk Kigwangalla jana alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema: “Hata mimi nimesikia taarifa hizo, isipokuwa sijapewa taarifa rasmi. Ila nafahamu kwamba vikao vya chama vilikuwepo na mimi niliitwa ila kama ambavyo nimeshasema siwezi kuhudhuria”.

Gazeti hili lilimtafuta Mbunge huyo machachari kutokana na taarifa yake aliyoitoa kwenye mitandao ya Facebook na Tweeter akieleza kuhusu taarifa za kuwapo mpango wa kumfukuza uanachama.

Kupitia mitandao hiyo Dk Kigangwalla aliandika: “Nimepokea taarifa kuwa madiwani walioungana na wananchi wa Nzega pamoja na mimi kupinga uamuzi wa Baraza la Madiwani kuzigawa pesa kwenye Kata wameadhibiwa na Kamati ya Siasa ya Chama Wilaya ya Nzega, bila kusikilizwa na ilhali miongoni mwa ‘mahakimu’ hawa ni watu waliokuwa wakilalamikiwa na madiwani na wananchi. “

Mbunge huyo aliongeza: “Nimepewa taarifa kuwa mapendekezo ya adhabu dhidi yangu kutoka wilayani kwenda vikao vya juu, ...tena bila kusikilizwa maana nilitoa udhuru, ni kuwa ninyang’anywe kadi ya uanachama wa CCM. Nimeshangazwa sana na kusikitishwa na jinsi chama kinavyoendeshwa Nzega.”

Mbunge huyo alisema anaamini viongozi wakuu wa CCM wanafuatilia kwa karibu suala hilo na watachukua hatua stahiki, huku akisema hatahudhuria tena kikao chochote cha CCM wilayani humo.

“Kama chama hiki kimefika huku, kwamba kuna watu wana nguvu kuliko chama, kwamba wachache wanaweza kuwaonea wengine kwa kuwa wana vyeo na mamlaka ya kufanya hivyo na hakuna wa kuingilia kati na kusema ‘no’, basi sina haja ya kuendelea kupambana,” aliongeza.

Aliendelea: “Nimechoka, sintokata rufaa wala sintolalamika tena. Watekeleze hukumu hiyo. Sintojitetea na sintohudhuria kikao chochote kile kuanzia sasa, nimechoka kupambana na watu wenye nguvu, nimechoka. Ni bora kuwa mnyonge, lakini ukabaki na uhai, uzima, heshima na furaha yako”.

Kauli ya CCM Nzega

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nzega, Amos Kanuda alikiri Dk Kigwangwalla kujadiliwa katika vikao vya chama vya wilaya, ikiwamo Kamati ya Siasa.
0 comments

WABUNGE WAFUATILIA MIRADI YA WANAWAKE TANGA

WABUNGE WAFUATILIA MIRADI YA WANAWAKE TANGA



Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Mhe. Said Mtanga akitambulisha wajumbe wa Kamati yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bibi Chiku Ngalawa wakati wa ufuatiliaji wa fedha ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake katika mkoa wa Tanga, tarehe 21/1/2014. Picha na Erasto ching’oro WMJJW. IMG_2334 
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Mhe. Said Mtanga akisaini kitabu cha wageni cha Kikundi cha Maendeleo ya wanawake Vumilia kinacholima zao la mwani katika kijiji cha Saadani  kata ya Tongoni jijini Tanga tarehe 21/1/2014. Picha na Erasto ching’oro WMJJW. IMG_2352 
Mwenekiti wa Kikundi cha Maendeleo ya Wanake Bibi Hadija Saida akionesha zao la mwani linalolimwa baharini wakati alipotembelewa na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na baadhi ya viongozi wa juu wa Harimashauri ya jiji la Tanga tarehe 21/01/2014. Picha na Erasto ching’oro WMJJW. IMG_2394 
Mwenyekiti wa kikundi cha Sanaa Endelevu ‘Arts and Culture’ Bibi Mariam Makoko cha barabara ya 5 jijini Tanga (aliyeko katikati mlangoni) akitoa maelezo kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu matumizi ya fedha ya Mfuko wa Maendeleo ya wanawake katika kujiletea maendeleo. Picha na Erasto ching’oro WMJJW.
0 comments

CHANETA YAWANOA WALIMU TANGA

CHANETA YAWANOA WALIMU TANGA


CHAMA cha Netiboli (CHANETA) Mkoa wa Tanga, kimeanza kutoa semina ya walimu wa michezo kutoka wilaya zote, lengo likiwa ni kuwaandaa kwa ajili ya kufundisha kwenye michezo ya Umitashumta na Umisseta mkoani Tanga.
 
Akizungumza jijini hapa juzi, Katibu wa chama hicho, Julieth Mndeme, alisema semina hiyo ina lengo la kuwajengea uwezo washiriki na kuhamasisha mchezo huo ambao unaendeshwa na mkufunzi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Anna Kibira.
 
Mndeme alisema semina hiyo itaendeshwa kwa siku 11 na ilianza Januari 16 na itafikia tamati Januari 27 ikishirikisha wanawake na wanaume kwenye viwanja vya Bandari.
 
Katibu huyo alisema mikakati waliyokuwa nayo katika kuuendeleza mchezo huo ni kuanzisha ligi za vijana wadogo na kuweka msukumo kwenye mashindano mbalimbali yakiwemo ya wilaya na mkoa.
 
Mndeme alisema ni matumaini yake mafunzo hayo yatakapomalizika watapatikana walimu wazuri ambao watakuwa ni chachu ya kukuza maendeleo ya netiboli kwenye wilaya wanazotoka na mkoa kwa ujumla.

0 comments

BREAKING NEEEWZZZZ!!!!! NDEGE YA ZAN AIR YAANGUKA PEMBA

BREAKING NEEEWZZZZ!!!!! NDEGE YA ZAN AIR YAANGUKA PEMBA

Ndege ya shirika la Zan Air imeanguka Pemba jioni hii ikiwa imebeba jumla ya abiria 19, miongoni mwa abiria hao pia alikuwamo Waziri wa Habari na Katiba wa Zanzibar mhe. Abubakar Kahamis, abiria wote wametoka salama.
 
0 comments

RAIS KIKWETE NA NAIBU RAIS WA KENYA MHE WILLIAM RUTO

RAIS KIKWETE NA NAIBU RAIS WA KENYA MHE WILLIAM RUTO

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitambulishwa kwa baadhi ya viongozi wa Kenya na Naibu Rais wa Kenya Mhe William Ruto walipowasili kwa pamoja katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi leo Ijumaa January 24, 2014.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka sahihi katika kitabu cha wageni huku akishuhudiwa na   Naibu Rais wa Kenya Mhe William Ruto na balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe Batilda Buriani  walipowasili kwa pamoja katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi leo January 24, 2014. 
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea  na   Naibu Rais wa Kenya Mhe William Ruto walipowasili kwa pamoja katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi leo
Viongozi hawa walikutana jijini Amsterdam, Uholanzi,  na kupanda ndege moja kuelekea nyumbani. Rais Kikwete, aliyetua Nairobi kwa muda,  alikuwa akitokea Davos, Uswisi, alikokuwa kwenye ziara ya kikazi ambayo  ameikatisha ili kujiunga na wananchi wa jimbo la Chalinze katika msiba wa Mbunge wa jimbo hilo Marehemu  Said Bwanamdogo, ambaye amefariki dunia alifariki dunia Januari 22, 2014  katika wodi ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi) alikokuwa akitibiwa. Mazishi yamepangwa kufanyika leo nyumbani kwa marehemu Miono, Bagamoyo.
PICHA NA IKULU
0 comments

WABUNGE WAFUATILIA MIRADI YA WANAWAKE TANGA

WABUNGE WAFUATILIA MIRADI YA WANAWAKE TANGA


Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Mhe. Said Mtanga akitambulisha wajumbe wa Kamati yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bibi Chiku Ngalawa wakati wa ufuatiliaji wa fedha ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake katika mkoa wa Tanga, tarehe 21/1/2014. Picha na Erasto ching’oro WMJJW. IMG_2334 
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Mhe. Said Mtanga akisaini kitabu cha wageni cha Kikundi cha Maendeleo ya wanawake Vumilia kinacholima zao la mwani katika kijiji cha Saadani  kata ya Tongoni jijini Tanga tarehe 21/1/2014. Picha na Erasto ching’oro WMJJW. IMG_2352 
Mwenekiti wa Kikundi cha Maendeleo ya Wanake Bibi Hadija Saida akionesha zao la mwani linalolimwa baharini wakati alipotembelewa na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na baadhi ya viongozi wa juu wa Harimashauri ya jiji la Tanga tarehe 21/01/2014. Picha na Erasto ching’oro WMJJW. IMG_2394 
Mwenyekiti wa kikundi cha Sanaa Endelevu ‘Arts and Culture’ Bibi Mariam Makoko cha barabara ya 5 jijini Tanga (aliyeko katikati mlangoni) akitoa maelezo kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu matumizi ya fedha ya Mfuko wa Maendeleo ya wanawake katika kujiletea maendeleo. Picha na Erasto ching’oro WMJJW.
0 comments

Chaneta Tanga yatoa semina kwa walimu wa mchezo huo

Chaneta Tanga yatoa semina kwa walimu wa mchezo huo

Na Safari Chuwa,Tanga.
 
CHAMA cha Mpira wa Pete Mkoa wa Tanga,(Chaneta)kimeanza kutoa semina ya walimu wa mchezo toka wilaya zote za mkoa wa Tanga lengo likiwa ni kuwaanda walimu hao kwa ajili ya kufundisha kwenye michezo ya Umitashumta na Umiseta mkoani Tanga.

Akizungumza jijini Tanga, Katibu wa chama hicho,Julieti Mndeme alisema semina hayo ina lengo ya kuwajengea uwezo washiriki na kuhamasisha mchezo huo ambayo yanaendeshwa na mkufunzi wa toka Chama hicho Taifa Anna Kibira.


Mndeme alisema semina hiyo itaendeshwa kwa muda wa siku kumi na moja  yalianza Januari 16 na  yanatarajiwa kuhitimishwa Januari 27 mwaka huu na yanashirikisha wanawake na wanaume yakifanyika kwenye viwanja vya bandari mkoani hapa.

Katibu huyo alisema mikakati waliokuwa nayo katika kuuendelea mchezo  huo ni kuanzisha ligi za vijana wadogo na kuweka msukumu kwenye mashindano mbalimbali yakiwemo ya wilaya na mkoa ili kuupa maendeleo mchezo huo.

Mndeme alisema kuwa ni matumaini yake mpaka mashindano hayo
yatakapomalizika watapatikana walimu wazuri ambao watakuwa ni chachu ya kukuza maendeleo ya mchezo huo kwenye wilaya wanazotoka na mkoa kwa ujumla.
0 comments

MAMIA WASHIRIKI MAZISHI YA MAMA WA MZEE MAKAMBA

MAMIA WASHIRIKI MAZISHI YA MAMA WA MZEE MAKAMBA

 
Mzee Yusufu Makamba akishauriana jambo na mwanae January Makamba wakati wa shughuli za mazishi zikiendelea.
Mzee Yusufu Makamba amefiwa na mama yake mzazi aliyefahamika kama Mariam Masau Kivugo  kilichotokea tarehe 21 January 2014.
Mzee Yusufu Makamba akiwa na mwanae January Makamba wakitafakari jambo baada ya kupata msiba mkubwa  wa kufiwa na Mama mzazi wa Mzee Yusufu Makamba, Mariam Kivugo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Ndugu Abdallah Majura Bulembo akitoa salaam za pole kwa wafiwa wakati wa mazishi ya Bibi Mariam Masau Kivugo.
 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akitoa salaam za pole kwa niaba ya Chama  kwa Mzee Yusufu Makamba na Familia yake wakati wa mazishi ya Mama wa Mzee Yusufu Makamba.
 Mamia ya watu wakimsikiliza Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia Ndugu January Makamba wakati akitoa salaama za shukrani kwa niaba ya familia kwa wananchi wote waliojitokeza kwenye mazishi ya Bibi yake Marehemu Mariam Masau Kivugo yaliofnyika Mehazangulu,Tanga.(P.T)

 Mwili wa Marehemu Mariam Kivugo ukipelekwa msikitini kwa ajili ya kuombewa kabla ya kuelekea makaburini.
 Watu wakiwa kwenye nyuso za huzuni wakati wa mazishi ya Bibi Mariam Kivugo ambaye pia ni mama wa Mzee Yusufu Makamba.
 :
Katibu wa NEC itikadi na Uenezi Nape Nnauye akishiriki kuweka udongo kwenye kaburi la mama wa Mzee Yusuf Makamba aliyefariki tarehe 20 Januari 2014.
0 comments

MAMA KIKWETE ASISITIZA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI KUTOKA KWA MAMA KWENDA KWA MTOTO

MAMA KIKWETE ASISITIZA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI KUTOKA KWA MAMA KWENDA KWA MTOTO

img_0858_04a5f.jpg
Na Magreth Kinabo – Maelezo

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka Watanzania kuongeza juhudi za kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi(VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ili katika Tanzania iweze kuwa na kizazi kisichokuwa na VVU na ugonjwa wa Ukimwi.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wakati akifungua mkutano wa kitaifa wa wadau wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Aidha mama Kikwete aliwataka Watanzania kuchangia sh. 100 katika kupambana na tatizo kwa mchango utawapa nguvu wadau wengine kuwaunga mkono.

Aliwataka wadau wamaendeleo kuendele kuunga mkno katika juhudi za kuondokana na tatizo hilo.

" Lazima juhudi za makusudi zifanyike bila kuchoka kwa maeneo yote Serikali, NGO's, taasisi za dini mashirika ya kiraia na watu binafsi . Hii itasaidia kunusuru kizazi chetu na kuwa na nguvu kazi iliyobora, kizazi kisichokuwa na maambukizi na VVU na Ukimwi," alisema Mama Kikwete huku akisisitiza Tanzania bila Ukimwi inawezekana.

Aliongeza kuwa mikakati imara na endelevu ni lazima iwepo kama vile kutoa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU na Ukimwi kwa kushirikisha jamii na kutoa tiba kikamilifu zinaweza kupunguza maambukizi hayo.


Alisema asilimia 98 ya wakina mama wajawazito wanahudhuria kiliniki angalau mara moja na asilimia 43 mara nne wakati wa ujauzito kati ya hao, asilimia 81 wanapimwa VVU.

Aliwataka wakina mama wajazito kuhudhuria kiliniki wakati wa ujauzito kuanzia siku ya kwanza hadi watakapoajifungua ili idadi ya wanahudhuria kiliniki iweze kufikia asilimia 100.

Naye Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid alisema hivi sasa Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi hayo kwa asilimia 15 mwaka 2012 kutoka asilimia 19 mwaka 2011 na lengo ni kufikia asilimia 5 ifikapo mwaka 2015.

Alisema asilimia 90 ya wakina mama wajawazito wamepimwa VVU kati yao asilimia 64 wamegundulika wanaishi na VVU , pia asilimia 55 ya watoto wanapatiwa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.(ARV's).

Kaimu Mkurugenzi wa Kinga kutoka wizara hiyo , Dk .Neema Rusibamayilla alisema alisema awamu ya pili ya kupambana na tatizo hilo itaanza Januari mwaka huu katika mikoa mingine 16.
Mratibu wa huduma hiyo kutoka Malawi, Dk. Michael Eliya alisema ni muhimu kuweza katika utoaji wa huduma, kuboresha miundombinu ,ikiwemo rasilimali fedha na watu katika kufanikisha malengo hayo.
Mwisho.
0 comments

SHOMARI KAPOMBE ANUKIA YANGA, WAKALA WAKE AFUNGUKA KWA MARA YA KWANZA

KAPOMBE AKIWA AS CANNES NA GALLAS
Baada ya chenga za hapa na pale, kila kitu sasa kimewekwa hadharani kwamba beki wa zamani wa Simba, Shomari Kapombe, ametaka mkataba wake na AS Cannes ya Ufaransa uvunjwe na imeelezwa anataka kubaki nchini na kujiunga na Yanga.


Habari za uhakika kutoka ndani ya AS Cannes nchini Ufaransa na kuthibitishwa na wakala wake anayeishi nchini Uholanzi, zimeeleza Kapombe amefanya mazungumzo na Yanga ambao wamemshawishi kubaki nchini.

Mmoja wa viongozi wa AS Cannes ameliambia Championi Jumatatu kwamba: “Shomari amesusa kuja na anataka mkataba wake uvunjwe, lakini bado hatujaelewa hasa tatizo ni nini, ila tunajua amefanya mazungumzo na timu ambayo ni mabingwa wa Tanzania (Yanga), kitu ambacho si sahihi.

“Amesema anataka kubaki Tanzania, kidogo inatushangaza kwa kuwa kesi yake moja kuhusiana na kutaka kulipwa fedha imefika Fifa, lakini ajabu kabisa hatukuwahi kukataa kumlipa, badala yake tulisimamisha malipo kutokana na kuchelewa kwake. Huo ndiyo ukweli, ila sipendi jina langu liandikwe gazetini.”

Blogu hii ilikuwa ya kwanza kuandika kuwa Kapombe amekwama nchini na yuko mkoani Morogoro licha ya kuripotiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba alishaondoka kwenda Ufaransa.

Juhudi za kumpata wakala wake, Dennis Kadito akiwa nchini Uholanzi anakoishi zilizaa matunda jana na akasema ana taarifa za Yanga pamoja na Azam FC kufanya naye mazungumzo.

“Kweli kuna hizo taarifa, si nzuri kwa kuwa ni kukiuka utaratibu. Tayari Kapombe amesema anataka mkataba uvunjwe, kama umesikia hivyo ni sahihi. Nawashauri Yanga au Azam kama wanamtaka waje nizungumze nao tukae na AS Cannes, basi tumalizane.

“Mkataba wake ni wa miaka miwili, hivyo wasitumie njia ya mkato kwa kuwa mambo yako wazi na mimi au AS Cannes hakuna mwenye shida,” alisema.

Kapombe alitokea Simba na kujiunga AS Cannes bure, Simba ikitegemea kupata fedha kama atauzwa katika timu nyingine za Ulaya, lakini mgogoro ulianza baada ya kutolipwa mshahara wake kutokana na kutokuwa na akaunti ya benki za kule Ufaransa lakini baadaye alilipwa baada ya kumaliza utata huo.
“Kweli kuna fedha anadai, utaona katika miezi minne aliyokuwa Ufaransa hajalipwa mwezi mmoja. Hii inatokana na ile ishu ya kuchelewa alipokuwa katika timu ya taifa. Halafu, awali alichelewa kulipwa kutokana na suala kutokuwa na kibali cha kazi kilichochelewesha ashindwe kufungua akaunti ya benki.

“Ila AS Cannes ambao walikasirishwa na Kapombe kuchelewa Tanzania walitaka TFF ndiyo wamlipe mshahara kwa kuwa ndiyo walimchelewesha, sasa kesi yake iko Fifa. Ninaamini atashinda na mimi niko upande wake maana ndiyo wakala wake.

“Lakini bado nasisitiza kuwa lazima Yanga wafuate utaratibu maana taarifa za kuzungumza naye ninazo na ni za uhakika,” alisema wakala wake huyo.

Kiongozi wa AS Cannes alisema wametumia mamilioni ya fedha kumtibu Kapombe, lakini wanashangazwa na mambo yanavyokwenda.

“Suala lake tutalishughulikia baadaye, tulikuwa na mechi muhimu na ngumu za FA. Tumeitoa St Etienne inayoshiriki ligi kuu, sasa tutarudi kushughulikia suala lake ingawa tunaweza kulifanyia kazi zaidi baada ya Fifa kutoa hukumu.”

Yanga wamekuwa wakikataa katakata kulizungumia suala la Kapombe kwa hofu ya kuingia kwenye adhabu ya kuzungumza na mchezaji mwenye mkataba.

“Najua sasa Yanga hawawezi kukubali, ila wanawasiliana naye na walishakaa wakamalizana kwa mazungumzo ya awali na sasa kuna mambo kadhaa wanamsaidia,” alisema rafiki yake aliyetoa siri kwa mara ya kwanza kuwa yuko Morogoro.

Taarifa zinaeleza Yanga wamelenga kumjumlisha kwenye dirisha la Caf kama watasonga mbele au mwanzoni mwa msimu mpya, mara tu baada ya dirisha kufunguliwa.

Kabla ya kuondoka nchini na kujiunga na AS Cannes inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Ufaransa, Kapombe alikuwa nahodha msaidizi wa Simba.
0 comments

MAMIA YA WAMZIKA DEUSDEDIT MTAMBALIKE

MAMIA YA WAMZIKA DEUSDEDIT MTAMBALIKE

 
Jaji Mstaafu Mark Bomani,Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa Nape Nnauye  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Mh.Stephen Wassira ni miongoni mwa viongozi mbali mbali walioshiriki mazishi ya kada maarufu ambaye pia alishawahi kuwa Mkuu wa Wilaya katika Wilaya mbalimbali nchini.
Mama Anna Mkapa,Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka na Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini Elizabeth Minde wakiwa miongoni mwa mamia ya Watanzania waliojitokeza kumzika kada wa siku nyingi Deusdedit Mtambalike.
Waombolezaji wakiwa kwenye nyuso za huzuni wakati wa mazishi ya mpendwa wao Deusdedit Mtambalike.
Sala ya kumuombea Marehemu Deusdedit Mtambalike aliyefariki tarehe 15 Januari 2014 nchini Afrika ya Kusini ilisomwa nyumbani kwake kabla ya Mazishi.

Wanandugu wa Marehemu Deusdedit Mtambalike wakiwa wamebeba mashada ya maua .
Mwanasiasa wa siku nyingi na ambaye alishawahi kushika nyazfa mbalimbali za serikali Balozi Paul Rupia akitoa salaam za pole kwa familia ya marehemu Deusdedit Mtambalike na kumuelezea marehemu kama mtu aliyemwema na asiyechoka kushauri kwenye jambo lolote alotakiwa kushauri.
Jaji Mstaafu Mark Bomani akimuelezea marehemu Deusdedit kama mtu ambaye hakusita wala kuwa na woga katika kuzungumzia jambo lenye manufaa kwa jamii.
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akitoa salaam za rambirambi kwa niaba ya CCM Makao Makuu wakati wa mazishi wa aliyekuwa Kada wa Chama Cha Mapinduzi Marehemu Deusdedit Mtambalike.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(Mahusiano na Uratibu) Mheshimiwa Stephen Wassira akitoa salaam za pole kwa niaba ya Serikali kwenye mazishi ya Ndugu Deusdedit Mtambalike yaliofanyika nyumbani kwa marehemu Kimara Bonyokwa.
Watoto wa Marehemu Deusdedit Mtambalike wakiwa wenye nyuso za simanzi na huzuni pamoja na Mama yao na Ndugu wa karibu wakati wa sala ya mwisho kabla ya mazishi ya Baba yao mpendwa.
Sehemu ya watu waliojitokeza kwenye mazishi ya Deusdedit  Mtambalike
Profesa Mahalu akiweka mchanga kama ishara ya kumzika rafiki yake Marehemu Deusdedit Mtambalike
Mke wa Marehemu Deusdedit Mtambalike akiweka shada la maua juu ya kaburi .
Watoto wa marehemu wakiweka shada la Maua kwenye kaburi la baba ya mpendwa Marehemu Deusdedit Mtambalike aliyefariki dunia tarehe 15 Januari 2014 nchini Afrika ya Kusini.
0 comments
 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger