KAMATI YAPITIA USAJILI, NGASA KUCHEZEA YANGA
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imepitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya
Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngasa kuchezea timu ya Yanga baada ya
kukamilisha usajili wake.
Hata
hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini
kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho
alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea
(sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya
fedha hizo kwa Simba.
Kamati
pia imemfungia mechi sita za mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya
Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha
kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa
fedha hizo.
Vilevile
Kamati imepitia pingamizi zote zilizowasilishwa kuhusu usajili wa
wachezaji, kukatiza mikataba ya wachezaji na kuzitaka klabu husika ziwe
zimetatua masuala hayo hadi Alhamisi (Agosti 22 mwaka huu).
Kwa
upande wa wachezaji wa kigeni, Kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza
hadi watakapopata Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) pamoja na vibali
vya kufanya kazi nchini (work permits).
Kamati
hiyo itakutana tena Ijumaa (Agosti 23 mwaka huu) ili kupata ripoti za
pingamizi ilizoagiza ziwe zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 mwaka huu na
kutoa uamuzi kwa pande ambazo hazikuafikiana.
UCHAGUZI TFF SASA KUFANYIKA OKTOBA 27
Kamati
ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa
kuzingatia mamlaka iliyonayo katika kifungu cha 10(6) cha Kanuni za
Uchaguzi za TFF inasogeza mbele tarehe ya uchaguzi wa TFF kutoka Oktoba
20 mpaka Oktoba 26 na 27 mwaka huu.
Sababu
za kusogeza mbele uchaguzi ni kutokana na ukweli kuwa Oktoba 20 mwaka
huu uongozi wa TFF utakuwa na shughuli nyingi za maandalizi ya mechi ya
Simba na Yanga, na hivyo haitawezekana kusimamia shughuli za Mkutano
Mkuu wa Uchaguzi kwa wakati mmoja na mchezo huo.
Siku ya mwisho ya kampeni itakuwa Oktoba 25 mwaka huu. Ukiondoa mabadiliko
hayo ya tarehe ya uchaguzi wa viongozi wa TFF, ratiba ya mchakato wa
uchaguzi na itabaki kama ilivyotangazwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF
katika mkutano wake na waandishi wa habari Agosti 24 mwaka huu.
Pia Kamati imeamua kuwa uchaguzi wa Bodi ya Ligi utabakia kuwa Oktoba 18 mwaka huu kama ilivyopangwa awali.
Kamati
imesema inaamini wahusika wote watapokea vizuri mabadiliko hayo na
inasikitika kwa usumbufu utakaosababishwa na mabadiliko hayo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)