Featured Post Today
print this page
Latest Post

Harufu ya ufisadi yabainika halmashauri za Tanga

Harufu ya ufisadi yabainika halmashauri za Tanga

 
Jiji la Tanga
 
Kamati  ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa( LAAC) imeagiza kuchukliwa hatua kali  na kusimamishwa kazi Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Korogwe, Sadiki Kallaghe, kwa tuhuma za kusaini mkataba  wa kumpa tenda ya kukusanya ushuru wa halmashauri  mzabuni bila kumshirikisha mwanasheria wala mkurugenzi wa halmashauri hiyo.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa LAAC, Rajabu Mbarok, katika majumuisho ya ziara yao katika ofisi za mkuu wa mkoa  wa Tanga na kushirikisha wakuu wa idara, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya.

Mbarok  alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bendkito Ole Kuyani, kuunda kamati ya kuchunguza suala hilo huku akitaka mwenyekiti huyo asimamishwe kazi ili kuepuka kuharibu uchunguzi.

Mbarok alisema wametembelea miradi sita katika halmashauri hiyo ikiwamo soko la kimataifa linalojengwa maeneo ya Makuyuni na kwamba miradi hiyo hairidhishi na kutolea mfano choo kilichojengwa kwa thamani ya Sh. milioni saba ambacho hakilingani na thamani halisi ya fedha.

Alisema halmashauri ya Korogwe imekuwa ikipata hati chafu kwa muda wa miaka mitano sasa na zaidi ya Sh. bilioni moja hazikutumika.

Kuhusu halmashauri ya Mji Mdogo wa Korogwe, alisema walikagua miradi mitano, lakini miradi yenye nafuu ni miwili tu hiyo mingine ipo chini ya viwango huku akimpa onyo mkurugenzi wa mji wa Korogwe kwa kuikimbia kamati hiyo na kwenda kujificha na kuwa wamekaidi agizo la  mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa hawawapandishi vyeo walimu na kuwaongezea mishahara mpaka sasa.

Katika Jiji la Tanga alisema walikagua mradi wa bwawa la umwagiliaji liliyopo Mabaayani lakini aligundua ufisadi mkubwa na kusema kuwa mradi huo ni wa watendaji na sio wananchi kwani mpaka sasa zaidi ya MSh. mlioni 300katika mradi huo zimeliwa na wajanja.
0 comments

Tanga sasa hatarini kupoteza hadhi ya Jiji

Tanga sasa hatarini kupoteza hadhi ya Jiji

Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Chiku Gallawa 

Halmashauri  ya Jiji la Tanga inaweza kushushwa hadhi kuwa manispaa kutokana na kushindwa kukusanya mapato.
Hayo yalibainishwa jana na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) wakati wa majumuisho ya ziara yao.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajabu Mbaruk, alisema kamati inakwenda kuishauri serikali kushusha hadhi ya kuwa jiji na kurudi katika hadhi ya manispaa kwa kuwa imeshindwa kukusanya mapato.

Alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Tanga inatia aibu kwani inakusanya mapato ya Sh. bilioni 3.5 kwa mwaka ambayo ni madogo kulinganisha na ya Jiji la Mwanza ambalo linakusanya Sh. bilioni 10 kwa mwaka.

Alisema cha kusangaza, Halmashauri ya Jiji la Tanga ina vyanzo vingi vya mapato, lakini mapato hayakusanywi na kusema kuwa hiyo ni aibu na haifai kuwa na hadhi ya jiji.

Mbarok alisema kuwa madiwani na watendaji hawana uchungu na halmashauri ya jiji la Tanga. “Sasa kamati inakwenda kuishauri serikali kushusha hadhi jiji la Tanga kuwa manispaa kama zamani,” alisema.

Alisema kuwa Mkoa wa Tanga una wilaya tisa, lakini cha kushangaza ni kuwa mkoa mzima wanakusanya Sh. bilioni nane tu na kuzidiwa na Jiji la Mwanza.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kiasi cha Sh. bilioni mbili za mapato zimepotea kutokana na jiji hilo kutokuwa na uwezo wa kutunza vizuri kumbukumbu za mahesabu.

Alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na lini LAAC itakutana na serikali ili kuwasilisha pendekezo la kulishusha hadhi Jiji la Tanga, alisema  kamati yake inaandaa taarifa ya mapendekezo na ili kuipeleka  Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi).
 
CHANZO: NIPASHE
0 comments

Waziri Kigoda mgeni rasmi tamasha la Handeni Kwetu 2013



Waziri Kigoda mgeni rasmi tamasha la Handeni Kwetu 2013



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
 
WAZIRI wa Viwanda na Biashara ambaye pia ndio mbunge wa Handeni, Dkt Abdallah Kigoda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Utamaduni, lililopangwa kufanyika Katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni mkoani Tanga, Desemba 14 mwaka huu.
 
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Abdallah Kigoda, pichani.
Tamasha hilo linafanyika kwa mara ya kwanza wilayani hapa, huku likitarajiwa kuwa la aina yake kutokana na maandalizi yanayoendelea kushika kasi.
Akizungumza jana mjini Handeni, Mratibu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema maandalizi yamezidi kushika kasi kwa kuangalia mazoezi ya vikundi kadhaa vitakavyotoa burudani katika tukio hilo.
“Tunashukuru Mungu kuona mambo yanazidi kuwa mazuri kwa kuhakikisha kuwa Desemba 14 mwaka huu tunafanya tamasha lenye mguso na kila mmoja wetu kufaidishwa.

“Huu ni wakati wa kila mtu kujipanga ili aje kushiriki kwa namna moja ama nyingine, ukizingatia kuwa juhudi hizi zote zipo kwa ajili ya kujenga ushirikiano kwa watu wote,” alisema Mbwana.
Wadhamini katika tamasha hilo ni pamoja na gazeti la Mwananchi, Clouds Media Group, ni Phed Trans, Clouds Media Group, Grace Products, Screen Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles & Construction Ltd, Katomu Solar Specialist, PLAN B SOLUTIONS (T) LTD, Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group duka la mavazi la Chichi Local Ware, Smart Mind & Arters chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog na Taifa Letu.com, huku likipangwa kuanza saa 2 za asubuhi hadi saa 12 za jioni.
0 comments

CHADEMA TANGA YAPONGEZA UAMUZI WA KUVULIWA UONGOZI KATIBU MSAIDIZI

CHADEMA TANGA YAPONGEZA UAMUZI WA KUVULIWA UONGOZI KATIBU MSAIDIZI

Na Oscar Assenga, Tanga
SIKU Chache baada ya Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Taifa (Chadema) kuamua kumvua uongozi ndani ya chama hicho aliyekuwa katibu Msaidizi Zitto Kabwe chama hicho mkoani hapa kimeipongeza hatua hiyo kwa kusema italeta umakini mkubwa kwa viongozi waliobaki.
Uamuzi huo ulitolewa kwa mujibu ibara ya 7.7.16 kifungu (V) ambayo inaeleza kuwa kamati hiyo ina mamlaka ya kumwachisha ujumbe wa kamati kuu mjumbe mteule ambaye ataenda kinyume cha katiba, kanuni na maadili au kushindwa kukidhi matakwa ya kuteuliwa kwake.
Akizungumza na Tanga Raha,Katibu wa Chadema Mkoa wa Tanga,Jonathan Bahweje alisema suala hilo lilipaswa kufanywa na kamati hiyo kwa sababu ni sahihi kwa mtu yoyote anayekiuka kanuni na taratibu za uongozi ndani ya chama hicho.
Bahweje alisema hatua ya Zitto kukiri kuwa alikosea na kupewa adhabu ya siku kumi na nne kujitetea kwa kamati kuu ya chama hicho alitumia busara kubwa sana na kuwataka wanachama kuwa na utulivu wakati mchakato huo ukiendelea.
  “Maamuzi ya kamati kuu yaliyofanywa sidhani kama yanaweza kuingiliwa na upande mwengine hivyo napenda kuwaasa viongozi wa ngazi za chini kuacha kuingilia suala hilo kwani tayari limeshapata muafaka “Alisema Bahweje.
Alisema wanaiomba kamati kuu ya chama hicho kumaliza mgogoro uliopo huo mapema ili kuweza kujiandaa na uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa mwaka 2014  kwani wamedhamiri kuhakikisha wanashinda katika chaguzi hizo.
Katibu huyo aliitaka kamati hiyo kukemea viongozi ambao wanapiga maamuzi yao kwani wao ndio chombo cha mwisho ambacho kinauwezo wa kufanya jambo lolote ambalo linaweza kuleta mgawanyiko ndani ya chama hicho.
   “Naishauri kamati kutumia nafasi yao kuwaonya viongozi kuanzia ngazi za chini na kuweza kuleta mshikamano wa pamoja ambao utaweza kuleta mafanikio katika chama chetu kwani uongozi imara ndio utakiwezesha kuwatumikia wananchi “Alisema Bahweje
0 comments

PANGANI YAZINDUA UTARATIBU WA UTOAJI VIBALI SHUGHULI ZA UFUGAJI MDOGO

PANGANI YAZINDUA UTARATIBU WA UTOAJI VIBALI SHUGHULI ZA UFUGAJI MDOGO

Na Burhan Yakub,Pangani.

Wilaya ya Pangani imezindua rasmi cha kitabu cha utaratibu wa
utoaji wa vibali vya shughuli za ufugaji mdogo wa viumbebahari ambao utawawezesha wakazi wa mwambao wa pwani kufanya shughuli za uzalishaji mali bila kuathiri mazingira.

Kitabu hicho  kilichozinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Hafsa Mtasiwa hivi karibuni kikiwa kimeandaliwa na mradi ujulikanao “Pwani Project”kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho,Mkurugenzi wa mradi wa Pwani,Baraka Kalangahe alisema yaliyoandikwa ni hali halisi ya sasa ya ufugaji mdogo wa viumbebahari na matatizo yanayoikabili tasnia ya maendeleo ya ufugaji mdogo wa viumbe bahari katika Wilaya ya Pangani.

Mengine yaliyoandikwa ni taarifa muhimu za maeneo yanayofaa kwa ufugaji mdogo wa viumbebahari katika Wilaya ya Pangani, maeneo yanayofaa kwa vijiji vya Buyuni, Mkwaja, Mikocheni, Sange,Kipumbwi, Mikinguni,Stahabu,Ushongo Bweni , Mkwajuni,  Pangani Magharibi, Mwembeni,Msaraza na   Kigurusimba.

Mkurugenzi huo pia alisema Kitabu hicho kinatoa mwongozo wa utoaji wa vibali, ufuatiliaji na udhibiti.

Akizungumza baada ya kuzindua kitabu hicho,Mkuu wa Wilaya alisema mradi huu utasaidia kuongeza thamani ya bahari nakuonya kuwa mtendaji atakayesababisha kuzorota katika eneo lake atamuwajibisha.
0 comments
 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger