JK katika mtihani wa Katiba Mpya;
Wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa
asaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013
ili kuwa sheria kamili, wasomi, wanasiasa na wanaharakati wamemshauri
asifanye hivyo, wakisema itapatikana Katiba Mpya isiyo na tija.
Wananchi hao kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar walisema kwa nyakati tofauti kuwa, Rais Kikwete anatakiwa
kutumia busara ya kushauriana na kupata maoni ya watu wa kada mbalimbali
ili kujua nini kifanyike, kabla ya kuamua kusaini muswada huo.
Mjadala wa muswada huo uliopitishwa
Ijumaa iliyopita na wabunge wengi wakiwa wa CCM, ulizua tafrani bungeni
iliyosababisha Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) kutolewa nje na askari. Katika
tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na
maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa
Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
Wapinzani walisema Serikali iliubadili
kwa nguvu muswada huo kwa kuondoa maoni muhimu ya wadau, pia
walilalamikia kitendo cha wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala
ya Bunge kutokwenda Zanzibar kuchukua maoni ya upande huo wa muungano.
Wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Gaudence Mpangala alisema mchakato wa kuandikwa kwa
Katiba Mpya ulikuwa ukienda vizuri... "Lakini umebadilika vibaya, tena
katika kipindi muhimu. Kupitishwa kwa muswada na kusubiri saini ya Rais
kunaweza kuleta Katiba Mpya, ikawa siyo ile ambayo Watanzania
wanaitarajia." Alishauri busara itumike kabla ya kusainiwa kuwa sheria
kamili.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tunguu
Zanzibar, Ali Uki alisema hakuna haja ya muswada kukimbiliwa kusainiwa
kwani katiba ni mali ya wananchi na kuupitisha ili uwe sheria bila
kuyashirikisha makundi mengine, kutaendeleza malalamiko na kurudisha
nyuma malengo ya kupatikana kwake. Uki alisema upo wasiwasi kwamba
Katiba Mpya itatokana na utashi wa kisiasa badala ya matakwa ya
wananchi, jambo ambalo alisema linaweza kuathiri malengo ya kuandikwa
kwake.
"Utashi wa vyama umeanza kujitokeza,
huku chama kimoja kikiwa na uwakilishi mkubwa kwenye Bunge hilo, chama
kimoja kina uwakilishi wa asilimia 72 katika Bunge la Katiba," alisema
Uki.
Alikosoa Kifungu cha 8 na Kifungu
kidogo cha 4 na 5 cha muswada huo kwamba vina kasoro kwa kuruhusu
wabunge wa Bunge la Katiba kufanya uamuzi kwa wingi wa kura badala ya
kutumika utaratibu wa theluthi mbili kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Profesa mwingine wa UDSM, Chris Peter
Maina alisema ikiwa kuna nia njema ya kupata Katiba bora, lazima suala
la uwiano wa idadi ya wabunge katika Bunge la Katiba litazamwe upya.
"Rasimu ya pili ikishatolewa na
kukabidhiwa kwa Bunge la Katiba, kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ndiyo itakuwa imekwisha. Sasa inakuwaje Bunge linajadili Rasimu ya
Katiba huku waliyoiandaa hawapo, hiki kitu kinashangaza," alisema
Profesa Maina.
Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Dk
Frank Tilly alisema hakuna umuhimu wa kukimbiza muswada kutiwa saini
wakati kuna mambo mengi ya msingi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi...
"Watanzania hawajakubaliana kwa pamoja, ili jambo liwe zuri ni lazima
pande mbili au zaidi zenye masilahi na kitu husika zikubaliane, sasa
hilo halijafanyika tunakimbilia wapi?" alihoji.
Mhadhiri wa UDSM, Bashiru Ally alisema
mchakato mzima wa Katiba umeshaingia doa kwa kupitishwa muswada
unaolalamikiwa na kwamba manung'uniko ya wananchi hayajajibiwa.
Alisema busara zisipotumika,
itapatikana Katiba isiyokuwa na uhalali wa kisiasa... "Nasema hivi kwa
sababu wanasiasa hawajakubaliana katika kupitisha sheria itakayounda
Bunge la Katiba".
Vyama vya kiraia
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano
Zanzibar, Hassan Nassor Moyo alisema Rais anapaswa kutafakari kwa
umakini kabla ya kusaini muswada huo na kuwa sheria mpya kwa kuwa bado
kuna manung'uniko.
"Hakuna mantiki ya kuupitisha muswada
ukawe sheria wakati kuna manung'uniko. Wakati umefika misimamo ya vyama
kuwekwa kando ili malengo yenye manufaa na tija yaweze kufikiwa kutokana
na mahitaji ya wananchi."
Moyo alisema ushirikishwaji wa
Wazanzibari ulikuwa finyu kwani waliopata fursa ya kutoa maoni yao
walikuwa ni viongozi wa Serikali pekee.
"Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
umetokana na washirika wawili, Zanzibar si mtoto wa kambo, ni mshirika
na mdau mkuu katika kupata Muungano uliopo," alisema Mzee Moyo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kitendo cha
kupitishwa muswada wenye kasoro ni wazi kuwa kitazalisha Katiba isiyo na
tija kwa taifa.
"Muswada umepitishwa na wabunge wa CCM
kwa asilimia 80, sidhani kama hii ni sawa katika hatua muhimu kama hii
na haitoi picha kamili ya mwelekeo chanya wa kupata katiba stahiki,"
alisema Dk Bisimba.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu
Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alisema: "Ukipitisha sheria kinyemela
maana yake ni kwamba unataka ifanye kazi kinyume na matakwa ya watu
wengi, jambo ambalo ni hatari kiuchumi na kielimu."
Alisema Rais Kikwete anatakiwa kutumia
busara katika suala hilo, kwa maelezo kuwa, amebakiza muda mfupi
kumaliza kipindi chake cha utawala, hivyo aache Katiba yenye tija kwa
Watanzania.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi (Tucta), Nicolaus Mgaya alisema: "Ikiwezekana muswada
uliopitishwa usisainiwe na urejeshwe bungeni na kupitiwa upya ikiwa ni
pamoja na pande zote mbili za Muungano kutoa maoni sambamba na
kurekebishwa kwa kasoro zilizopo."
Alisema watu wataondoka lakini
Tanzania itaendelea kuwapo, hivyo ni jambo la busara kama ikipatikana
Katiba itakayokuwa na masilahi kwa wakati huu na ujao.
Wanasiasa
Katibu Mkuu wa TADEA, Juma Ali Khatib
alisema muundo wa Bunge la Katiba ndio unaozua malalamiko kutokana na
wanasiasa kupewa nafasi kubwa, jambo ambalo alisema linaweza kutanguliza
dhima ya kisiasa na kuweka kando masilahi ya kitaifa na utaifa.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba alisema kitendo cha Zanzibar kutoshirikishwa ni kosa kwani
Katiba hiyo ni ya Jamhuri ya Muungano... "Namshauri Rais asisaini
muswada huu kwani utakuwa ni majanga. Namshauri akutane na watu
walioonyesha wasiwasi na sheria hiyo ili kusikiliza mawazo yao, huenda
wakamshauri jambo la msingi la kufanya na iwapo atasaini bila kufanya
hivyo mchakato mzima hautakuwa wa taifa, bali wa CCM."
Chanzo:Mwananchi
Posted by
Unknown
11:28 PM