Serikali kuendeleza viwanda nchini
SERIKALI
imeahidi itaendelea kusaidia sekta ya viwanda, hususani vya ndani kwa
kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, ili kuhakikisha vinasaidia kutoa
mchango katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii.
Akizumgumza katika sherehe ya kukabidhiwa nyumba mbili za kisasa
zilizotolewa msaada na Kampuni ya Saruji Tanga (TCCL) kwa ajili ya
watumishi wa gereza la Maweni, mkoani hapa mwishoni mwa wiki, Waziri wa
Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, alisema wizara yake
itahakikisha viwanda vya ndani vinapata faida, ili viweze kuchangia
maendeleo ya jamii zinazowazunguka.
Alisema serikali inafahamu viwanda vya uzalishaji nchini vinachangia
kwa kiasi kikubwa maendeleo ya jamii kupitia programu za huduma za
kusaidia jamii, na kwamba katika siku za karibuni vimeonyesha matokeo
chanya.
“TCCL wamekuwa mstari wa mbele kusaidia na kuchangia jamii kwa madhumuni ya kupunguza umaskini, hasa katika maeneo ya vijijini.
“Tanga Cement wameonyesha mifano ya wazi kabisa kwamba viwanda vya
wazawa na wageni wanaokuja kuwekeza nchini wanaweza kuwa na mahusiano
mazuri na wenyeji wanaozunguka kiwanda husika,” alisema Dk. Kigoda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji Tanga (TCCL), Reinhardt
Swart, alisema kampuni yao wanaelewa programu ya huduma ya kusaidia
jamii ni kurudisha fadhila kwa jamii baada ya kufanya au kuwauzia bidhaa
zao.
Alisema mwaka jana kupitia programu za huduma za kusaidia jamii, TCCL
wametumia takribani sh milioni 327 kwa kujenga na kukarabati shule,
zahanati na kusaidia miradi mbalimbali ya jamii nchini.
Aliongeza kuwa hivi karibuni kampuni hiyo imemalizia ujenzi wa
maabara ya sayansi kwa Shule ya Sekondari Pongwe na wanatarajia
kukabidhi maabara hiyo kwa uongozi wa shule.
Kamishina Msaidizi Mwandamizi (SACP) wa Jeshi la Magereza, Augustino
Mboje, alisema jeshi hilo mkoani Tanga linawashukuru viongozi na
wafanyakazi wa kiwanda hicho kwa msaada huo kwa sababu utachochea
ufanyaji kazi kwa maofisa wa magereza
Chanzo;Tanzania Daima
Posted by
Unknown
10:14 PM