Serikali kuendeleza viwanda nchini

Serikali kuendeleza viwanda nchini

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda 
SERIKALI imeahidi itaendelea kusaidia sekta ya viwanda, hususani vya ndani kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, ili kuhakikisha vinasaidia kutoa mchango katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii.
Akizumgumza katika sherehe ya kukabidhiwa nyumba mbili za kisasa zilizotolewa msaada na Kampuni ya Saruji Tanga (TCCL) kwa ajili ya watumishi wa gereza la Maweni, mkoani hapa mwishoni mwa wiki, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, alisema wizara yake itahakikisha viwanda vya ndani vinapata faida, ili viweze kuchangia maendeleo ya jamii zinazowazunguka.
Alisema serikali inafahamu viwanda vya uzalishaji nchini vinachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya jamii kupitia programu za huduma za kusaidia jamii, na kwamba katika siku za karibuni vimeonyesha matokeo chanya.
“TCCL wamekuwa mstari wa mbele kusaidia na kuchangia jamii kwa madhumuni ya kupunguza umaskini, hasa katika maeneo ya vijijini.
“Tanga Cement wameonyesha mifano ya wazi kabisa kwamba viwanda vya wazawa na wageni wanaokuja kuwekeza nchini wanaweza kuwa na mahusiano mazuri na wenyeji wanaozunguka kiwanda husika,” alisema Dk. Kigoda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Saruji Tanga (TCCL), Reinhardt Swart, alisema kampuni yao wanaelewa programu ya huduma ya kusaidia jamii ni kurudisha fadhila kwa jamii baada ya kufanya au kuwauzia bidhaa zao.
Alisema mwaka jana kupitia programu za huduma za kusaidia jamii, TCCL wametumia takribani sh milioni 327 kwa kujenga na kukarabati shule, zahanati na kusaidia miradi mbalimbali ya jamii nchini.
Aliongeza kuwa hivi karibuni kampuni hiyo imemalizia ujenzi wa maabara ya sayansi kwa Shule ya Sekondari Pongwe na wanatarajia kukabidhi maabara hiyo kwa uongozi wa shule.
Kamishina Msaidizi Mwandamizi (SACP) wa Jeshi la Magereza, Augustino Mboje, alisema jeshi hilo mkoani Tanga linawashukuru viongozi na wafanyakazi wa kiwanda hicho kwa msaada huo kwa sababu utachochea ufanyaji kazi kwa maofisa wa magereza
 
Chanzo;Tanzania Daima 
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger