NAIBU WAZIRI MAKAMBA ATAKA WANAWAKE KUJIUNGA NA VIKUNDI
Raisa Said, Bumbuli.
MBUNGE wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba
amewataka wanawake na vijana wa Jimbo hilo kuanzisha vikundi vya ujasiriamali
ili waweze kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali likiwemo shirika la
Maendeleo la Bumbuli.
Akizungumza kwa niaba ya Makamba,Makamu
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bakari Kavumo wakati wa
uzinduzi wa kikundi cha Tumaini (VIKOBA)
kilichopo kata ya Soni alihimiza uanzishwaji wa vikundi na
kwamba kufanya hivyo kutawarahisishia upatikanaji mikopo na misaada kwa
wahisani.
Pia Mbunge huyo alichangia shilingi 3.
milioni kama mtaji wa kuendesha kikundi
hicho ambacho kimezinduliwa katika jimbo lake lengo kubwa kuwakomboa wanawake na umaskini.
Alisema ni vema wananchi hao wakaanzisha vikundi
maalumu ambavyo vitafahamika kisheria na hivyo kuwa njia mbadala ya
kujinasua na umasikini badala ya kutegemea shughuli za mtu mmoja mmoja.
Makamba ambae pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano
Sayansi na Teknolojia aliahidi kusimamia vikundi hivyo na
kuhakikisha kuwa akinamama na vijana waliyojiunga wanapata mikopo kutoka
Shirika hilo la Maendeleo ya Jimbo la Bumbuli (BDC).
Alisema atatekeleza hayo ikiwa ni miongoni mwa ahadi zake
alizozitoa wakati wa kuomba ridhaa ya ubunge kwa wakazi wa Jimbo hilo na kwamba
licha ya mikopo hiyo atahakikisha kuwa sekta zote muhimu zinapata mabadiliko
huku akiwa na nia kuwakwamua wana bumbuli
kiuchumi.
Shirika
la Maendeleo la Bumbuli lilianzishwa rasmi mwaka juzi na Mbunge wa Jimbo
hilo, January Makamba kwa ajili kuratibu na kuharakisha maendeleo kwa wananchi
wa jimbo hilo.
Taasisi
ya Utoaji Mikopo ya shirika hilo, BDC-MFI imeanzishwa kama chombo cha kuziba
pengo lililopo la ukosefu wa mitaji na vyombo vya utoaji mikopo kwa ajili ya
wajasiriamali wa kawaida.
MWISHO