HALI YA USALAMA YAZIDI KUZOROTA JAMUHURI YA AFRIKA YA KATI
Waasi wa kundi la kikristo la Anti Balaka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wametishia kuwaua mamia ya waislamu wanaojificha katika kanisa moja kama hawataondoka nchini humo katika kipindi cha wiki moja ijayo.
Wanajeshi wa kulinda amani wapatao 30 kutoka Cameroon walilazimika hapo jana kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya wapiganaji wa Anti Balaka waliokuwa wamekusanyika nje ya kanisa hilo la Kikatoliki wakipania kuwaua waislamu hao ambao wamekimbilia katika kanisa hilo kuokoa roho zao.
Milio hiyo ya risasi iliwaogofya watoto waliokimbia kujinusuru na vilio vya watu hao waliojawa na uoga vilisikika vikirindima katika kanisa hilo.Wanajeshi hao wa kulinda amani kwa sasa ndiyo tegemeo la pekee kwa waislamu hao wapatao 800 dhidi ya kushambuliwa na magenge yanayotaka kuwaua.
Wapiganaji wa Anti Balaka tayari walionekana wakiwa na mitungi ya lita 40 ya petroli ambayo wametishia kutumia kulichoma kanisa hilo.Kasisi wa kanisa hilo Justin Nary ambaye anatoa hifadhi kwa waislamu hao anajua analengwa na waasi hao.
Waasi walizingira kanisa kuwasaka waislamu
Kasisi Nary amesema wapiganaji hao wa Anti Balaka wamemtishia maisha mara nne kwa kumulekezea mtutu wa bunduki na wamempigia simu kumuonya kuwa punde tu wanajeshi wa kulinda amani wataondoka,watamuua.
Baadhi ya wanaotafuta hifadhi katika kijiji hicho cha Guen wametoroka baada ya kiasi ya waislamu 70 kuuawa katika siku za hivi karibuni.Waislamu na wakristo walikuwa wakiishi kwa amani tangu jadi hadi kundi la waasi la kiislamu kutoka Kaskazini mwa nchi hiyo lilipoipindua serikali na kulitumbukiza taifa hilo katika ghasia.
Kundi hilo la kiislamu la Seleka linashutumiwa kwa mauaji katika vijiji vya wakristo katika taifa hilo.Viongozi waliosaidiwa na Seleka kuingia madarakani walipoondolewa madarakani mwezi Januari,ilichochea mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa kundi lililoibuka la Anti Balaka.
Mauaji yaripotiwa katika miji mingine
Mji mkuuu Bangui ambao ulikuwa ni kitovu cha maasi na ghasia tangu mwezi Desemba kwa sasa hali inaonekana kudhibitiwa kwa kiasi fulani lakini mauaji yanayofanywa kwa misingi ya kidini yanaendelea kuripotiwa katika miji mingine nchini humo.
Majeshi ya Ufaransa na ya umoja wa Afrika yaliyoko nchini humo kudhibiti hali hayatoshi kukidhia mahitaji ya kiusalama na kiulinzi yanayohitajika kwa dharura.
Umoja wa Mataifa umeiomba Jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kabambe na za dharura kuisaidia Jamhuri ya Afrika ya Kati kujikwamua kutoka kwa mzozo mbaya unaotishia kulisambaratisha taifa hilo.
Bunge la Ufaransa hii leo linatarajiwa kupiga kura kuidhinisha kuendelea kusalia kwa jeshi lake nchini humo hadi mwezi Februari mwaka ujao wakati ambapo Jamhuri ya Afrika ya Kati itafanya chaguzi.
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean Yves Le Drian amekiri kuwa itachukua muda mrefu kuliko walivyotarajia kurejesha udhabiti nchini humo kutokana na kiwango cha juu cha uhasama na ghasia.Maelfu ya watu wameuawa tangu Desemba na zaidi ya watu milioni moja wameachwa bila makaazi.
Chanzo, dw.de.com/swahili. R.M