Mwalimu Julius Nyerere akiwa na mgeni wake Nelson Mandela (kushoto) na
Winnie Mandela kwenye gari la wazi wakati wakiwasili kwenye Uwanja wa
Taifa, jijini Dar es Salaam. Mandela alifanya ziara nchini mwaka 1990
baada ya kutoka gerezani.Picha na Maktaba.
DAR ES SALAAM.
SIKU 23 tu baada ya Nelson Mandela
kuachiwa huru kutoka gerezani, Februari 11, 1990 aliwasili hapa nchini
kwa ziara fupi iliyokuwa na msisimko wa aina yake.
Aliwasili nchini Machi 5, 1990 na kulakiwa kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam (Sasa Uwanja wa Julius
Nyerere) na Mwalimu Nyerere.
Baada ya kuwasili, alikagua gwaride kama ilivyo
kawaida, lakini kikubwa ilikuwa ni hamasa ya Watanzania hasa wakazi wa
Dar es Salaam na vitongoji vyake, maelfu kwa maelfu kujipanga barabarani
kumlaki kiongozi huyo katika njia zote alizopita kuanzia Uwanja wa
Ndege.
Pamoja na mvua za masika zilizokuwa zinanyesha, hakuna aliyejali hali hiyo. Kila mmoja alikuwa na shauku ya kumwona Mandela.
Ilielezwa kuwa Mandela na ujumbe wake angewasili
mapema zaidi, saa 4:00 asubuhi, lakini ratiba ilibadilika kuwa
angewasili saa 11 jioni, lakini watu hawakupungua barabarani,
walijipanga mapema kuanzia Uwanja wa Ndege, Barabara ya Pugu (sasa
Nyerere) na maeneo mengine kumlaki mpigania uhuru huyo.
Wakati huo Dar es Salaam ilikuwa na tatizo kubwa
la usafiri, lakini hakuna aliyejali. Mara baada ya Mandela kutua,
ilinyesha mvua kubwa, watu walikubali kulowa lakini hadi wamwone
Mandela.
Mandela alipata mapokezi makubwa na ya aina yake
jijini Dar es Salaam. Kikubwa ni kwamba, Mandela alikuwa akizungumzwa
sana na vyombo vya habari, kuonwa kwenye magazeti lakini wengi walitaka
kumwona Mandela na mkewe Winnie uso kwa uso.
Baada ya shughuli za Uwanja wa Ndege kukamilika na
mvua kukatika, Mandela aliyefuatana na mkewe, Winnie walipanda gari ya
wazi aina ya Rolls Royce wakiwa na Mwalimu Nyerere kwa pembeni.
Maelfu kwa maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam
walijipanga kuanzia Uwanja wa Ndege, Barabara ya Pugu, Uhuru, Kariakoo,
Stesheni, Luthuli hadi Ikulu na watu wote hao walikuwa na shauku ya
kumuona Mandela walitimiza kiu yao. Kila mmoja alifurahi baada ya
kumuona Mandela aliyekuwa akipunga mkono muda wote.
“Ndoto yangu imetimia”, “Siamini, nimemwona
Mandela?”, “Safi”, “Naweza kufa kwa amani...nimemwona Mandela” zilikuwa
kauli za watu mbalimbali waliokuwa wamejipanga barabarani kumlaki
Mandela akiwa na Winnie walipokuwa wakipita.
Siku iliyofuata, hali ilikuwa zaidi ya siku ya
mapokezi. Watu waliombwa kufika kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa
Uhuru) na ilikuwa mminyano wa aina yake. Zaidi ya watu 100,000
wanasadikiwa walifurika uwanjani kusikiliza hotuba ya pili ya Mandela
tangu atoke gerezani.
Mandela alitoa hotuba ya kwanza akiwa City Hall
nchini Afrika Kusini. Aliwahutubia wafuasi wa ANC wapatao 50,000
waliokuwa wakimsubiri kwa hamu kumuona baada ya kifungo cha miaka 27
jela, ambako pamoja na yote alionyesha furaha yake kulakiwa na maelfu ya
wapenzi na wafuasi wake hao. MWANANCHI
Posted by
Unknown
11:38 PM