MAKAMBA AMWAGA VIFAA VYA MICHEZO VYENYE THAMANI YA SH.MILIONI 2,JIMBONI KWAKE.
Na Rais Said,Lushoto.NAIBU Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Technologia,Januari Makamba amemwaga vifaa vya michezo jimboni kwake vyenye thamani ya sh.milioni 2 lengo likiwa ni kuhamasisha vijana kupenda mchezo wa mpira wa miguu.
Vifaa vilivyotolewa na Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bumbuli ni mipira 50 kwa vijana ikiwa ni harakati za kuhamasisha kuinua sekta ya michezo jimboni humo na kupata timu ambayo baadae itakuja kuwa tishio kwenye medani ya soka mkoani hapa.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya mbunge,Katibu wa Mbunge huyo ,Hozza Mandia alisema vifaa vilivyotolewa ni katika kutekeleza ahadi zake alizozitoa kwa vijana jimboni humo kuwa atainua michezo kwa kutoa misaada kwa timu mbalimbali hasa za vijana.
Katibu huyo ambaye ni diwani wa kata ya Milingano alisema jitihada zinazofanywa na Makamba zinapaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali wa soka jimboni humo lengo likiwa kuwapa fuksa vijana kushiriki kwenye michezo.
“Kama unavyojua michezo ni ajira ambayo inaweza kuwainua vijana na ni fursa ya kipekee kwao hivyo tunamshukuru Mh,Naibu Waziri kwa msaada huu kwani utaweza kuwaondoa vijana kukaa vijiweni ambapo muda mwingi hufikiria kufanya vitendo viovu badala yake watakuwa wakishiriki michezo kutokana na kuwa na vifaa vya kuchezea “Alisema Hozza.
Aidha katibu huyo alitoa wito kwa vilabu vya Mgambo Shooting na Coastal Union kuweka utaratibu wa kutembelea Jimboni humo ili kuweza kuangalia wachezaji wenye viwango vya hali ya juu ambao wanapatikana wilayani kuliko kuchukua wachezaji nje ya mkoa ambao wakati mwingine wanashindwa kuipa mafanikio timu hizo.