Meneja
Uendelezaji Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited
(MCL), Theophil Makunga na wenzake wawili, wamepatikana na kesi ya
kujibu katika kesi ya makala ya uchochezi inayowakabili.
Makunga
na wenzake Absalom Kibanda na Samson Mwigamba wanakabiliwa na kesi ya
uchochezi dhidi ya askari wa majeshi ya ulinzi kwa kuchapisha makala
kwenye Gazeti la Tanzania Daima yenye maneno yaliyolenga kuwashawishi
wasiwatii viongozi wao.
Makala
hayo ya Novemba 30, 2012 yaliyokuwa na kichwa cha habari 'Waraka maalumu
kwa askari wote' yaliandikwa na mshtakiwa wa kwanza, Mwigamba ambaye ni
mwandishi wa makala katika safu yake ya 'Kalamu ya Mwigamba' katika
gazeti hilo.
Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Warialwande Lema jana
aliwaamuru washtakiwa hao kujiandaa kupanda kizimbani kujitetea baada ya
upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake.
Wakili wa
Serikali Beatha Kitau, alisema upande wa mashtaka haukuwa na shahidi
mwingine zaidi hivyo kuiomba mahakama kufunga ushahidi wao. Kabla ya
kufunga ushahidi wake, upande wa Jamhuri uliwaita mashahidi watatu kutoa
ushahidi.
Mashahidi
hao ni pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Usajili wa Magazeti, Raphael,
Hokororo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza (ACP) kutoka Kitengo
cha Sheria cha jeshi hilo, George Mwambashi na Mrakibu Mwandamizi wa
Jeshi la Polisi (SSP), David Hizza.
Baada ya
Jamhuri kufunga ushahidi wake, mawakili wa utetezi wakiongozwa na Isaya
Matambo waliiomba mahakama iwapatie mwenendo wa kesi hiyo kwa ajili ya
kuandaa hoja kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la.
Mbali na
Matambo, mawakili wengine wa utetezi ni Nyaronyo Kicheere na John Mhozya
ambao wote watatu wanawatetea Mwigamba na Kibanda na Imam Daffa kwa
niaba ya Makunga.
Hata
hivyo, Hakimu Lema aliwakatalia akisema kuwa hawezi kutoa nafasi ya
kufanya majumuisho ya hoja kama washtakiwa wana kesi au la.
Hata
hivyo, Hakimu Lema hakufafanua sababu ya kukataa ombi hilo, badala yake
alitoa uamuzi papo hapo kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.
"Baada ya
prosecution (upande wa mashtaka) kufunga ushahidi wake na kwa
kuzingatia ushahidi ulioko mahakamani, Mahakama hii imeona kuwa
washtakiwa wote wana kesi ya kujibu na wanatakiwa wajiandae kwa
utetezi," alisema.
Kutokana
na uamuzi huo, Hakimu Lema aliamuru washtakiwa waanze kujitetea Septemba
3, mwaka huu.Wakati uamuzi huo ukitolewa, mshtakiwa wa kwanza, Mwigamba
hakuwepo mahakamani, badala yake aliwakilishwa na mdhamini wake Rose
Moshi ambaye alisema mshtakiwa huyo hakuweza kufika mahakamani kwa kuwa
ni mgonjwa na amelazwa Hospitali ya St. Thomas Arusha.
Makunga
ambaye ni mshtakiwa wa tatu aliunganishwa katika kesi hiyo kutokana na
gazeti hilo kuchapisha makala hayo katika mitambo ya uchapaji ya Kampuni
ya MCL, wakati alipokuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji.
Wakili wa
Serikali, Elizabeth Kaganda alidai kuwa Novemba 30, 2011, Makunga
akikaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications
ilichapisha waraka wenye kichwa cha habari "Waraka Maalum kwa askari
wote".
Kibanda
ambaye ni mshtakiwa wa pili, anakabiliwa na mashtaka ya kuruhusu makala
hayo kuchapishwa katika gazeti hilo, wakati huo akiwa Mhariri Mtendaji
wa Gazeti la Tanzania Daima.
Upande wa
mashtaka unadai kuwa makala hayo yaliyotoka katika gazeti la Tanzania
Daima Toleo Na. 2552 ni kinyume na kifungu cha 32 (1) (c) na 31 (1) (a)
cha Sheria ya Magazeti, Sura ya 229, iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
Unadai
kuwa makala hayo yalilenga kuwashawishi askari wa Jeshi la Wananchi
(JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi, Magereza na Mgambo
kutokutii amri za viongozi wa majeshi hayo na Serikali kwa jumla.
:CHANZO MWANANCHI