WAWILI WAPANDISHWA KUZIMBANI KWA KUTAKA KUMPA RUSHWA DC KILINDI.
Na Oscar Assenga, Kilindi.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga,Edson Makala alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 12 mwaka huu mara baada ya taasisi hiyo kuweka mtego ambao uliwekwa na ofisi ya mkuu huyo wa wilaya na kufanikiwa kuwakamata wahusika hao.
Makala alisema watuhumiwa hao walitenda kosa la kujihusisha na vitendo vya kushawishi na kutoa hongo ya kiasi cha sh.milioni moja na laki moja kwa mkuu wa wilaya hiyo ili kulifanya jambo la eneo hilo lifanikiwe kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Kamanda Makalo aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Sharrif Lemanda Lemteka mkazi wa Lesoit Kiteto na Emanuel Ole Kileli mkazi wa Elerai kata ya Kibirashi wilayani Kilindi na kufunguliwa kesi ya jinai Na CC 228/2013 ambapo washtakiwa wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa kinyume na kifungu cha 15(b) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na 11/2007.
Alisema washtakiwa wote wawili walisomewa mashtaka na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa George Magoti mbele ya hakimu wa wilaya ya Handeni Patrick Maligana ambapo washtakiwa wote wawili walipata dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa na mahakama wakati kesi hiyo ikipangwa kutajwa tena mahakamani hapo Novemba 28 mwaka huu.
Aliongeza kwa kutoa wito kwa wananchi kuzingatia maadili na kutojikujihusisha na vitendo vya rushwa kwani kufanya hivyo watakuwa wameingia matatani.