KUNA UGUMU GANI SIMBA NA YANGA KUCHEZESHWA NA MAREFA WA KIGENI?
WAKATI leo nyasi za Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam zinatarajiwa kuwaka moto kwa mpambano mkali wa watani wa
jadi, Simba na Yanga katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, tayari
mizengwe imekwishaanza kuibuka kuhusu marefa.
Yanga
SC wanadai hawana imani na refa Israel Mujuni Nkongo, kwa madai aliwahi
kuwaonea katika mechi dhidi ya Azam FC msimu uliopita.
Nakumbuka,
wachambuzi na watangazaji wa SuperSport waliwahi kuiingiza mechi ya
Simba na Yanga katika orodha ya mechi tatu kali za wapinzani wa jadi
Afrika - nyingine zikiwa ni kati ya Orlando Pirates na Kaizer Chiefs za
Afrika Kusini na Al Ahly dhidi ya Zamalek za Misri.
Lakini mimi naongeza mechi ya
wapinzani wa Ghana, Hearts Of Oak na Asante Kotoko, ingawa Kenya nako
upinzani wa Gor Mahia na AFC Leopard umeanza kuja juu tena, baada ya
kuporomoka miaka ya karibuni, kutokana na kuyumba kwa timu zenyewe.
Hakuna
ubishi upinzani wa Ahly na Zamalek huo ni dunia nzima - ni zaidi ya
upinzani, lakini kwa Afrika fuatilia ligi nyingi, utagundua Simba na
Yanga ni mechi yenye mvuto wa kipekee na ndiyo maana hivi sasa
SuperSport wamekuwa wakionyesha mfululizo mechi za watani hao, ingawa
hawana mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wa kuonyesha mechi
za Ligi Kuu.
Unaweza kutilia
shaka kiwango cha soka cha timu hizo, lakini si upinzani wao kwa maana
ya upinzani. Upinzani wao ni sehemu ya burudani na kama iko siku
zitakuwa imara na kucheza soka ya kuvutia, basi burudani itakuwa mara
mbili.
Hata hivyo kuna mambo mawili au matatu ambayo kwa kiasi fulani yamekuwa yakipunguza ladha ya mechi za watani hao wa jadi.
Awali
tatizo kubwa lilikuwa Uwanja mdogo wa Uhuru, lakini tangu kukamilika
kwa Uwanja wa Taifa ambao tumeshuhudia mechi zote zilizochezwa hapo,
haijatokea mechi hata moja mashabiki wakajaza viti, mambo yamekuwa
mazuri.
Matatizo mawili
yaliyobakia ni viwango vya timu kuboreshwa, ili ifike wakati pamoja na
upinzani, kukamiana lakini watazamaji washuhudie soka safi.
Tatizo
la pili ni marefa, kweli ilipofikia na kama kweli lengo ni kuiongezea
msisimko zaidi mechi ya watani, waamuzi wa Tanzania wawekwe kando na
watumike waamuzi kutoka nje ya nchi, tena ikibidi nje kabisa ya nchi
tatu za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.
Rejea
mchezo wa kufunga pazia la Ligi Kuu msimu wa 2011/2012, Mei 6, 2012,
refa alitoa penalti tatu na kadi moja nyekundu kwa Yanga, ikichapwa 5-0
na Simba.
Hii si sahihi katika
mechi za wapinzani wa jadi, dhahiri refa huyu alishindwa kuumudu mchezo
wa watani hata kama alifuata sheria 17. Katika mechi ya wapinzani wa
jadi, ukishatoa kadi moja nyekundu kwa timu moja, unajifikiria sana
kurudia kutoa kadi ya pili kwa timu hiyo hiyo.
Katika
mechi za wapinzani wa jadi, ukishatoa penalti moja kwa timu moja,
unajifikiria sana kutoa penalti ya pili kwa timu hiyo hiyo. Unafikiria
mengi. Tena mengi sana.
Haya ni mambo ambayo umefika wakati sasa, TFF wanapoingia kwenye mechi ya watani, wanatakiwa kuyafikiria.
Rejea
mechi ya Machi 5, mwaka 2011 Uwanja wa Taifa, refa Orden Mbaga
aliivuruga mno mechi hiyo, kutokana tu na pengine mchecheto ama kutaka
kufanya kile ambacho kinaitwa 'kubalansi' mchezo au kukwepa lawama,
matokeo yake anafanya madudu.
Dakika
ya 58 Juma Said Nyosso alimkwatua Davies Robby Mwape kwenye eneo la
hatari akawapa penalti Yanga na kilichofuatia wengi walijua beki huyo wa
Simba atatolewa nje kwa kadi nyekundu, badala yake akampa kadi ya
njano.
Ngumu kuamini Mbaga,
refa mwenye beji ya Shrikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hajui alipaswa
kufanya nini kwa Nyosso, lakini kwa sababu ni refa wa nyumbani na
aliongoza wapinzani wa jadi katika mechi ya nyumbani, alihofia kumtoa
mchezaji kwa kadi nyekundu angeshushiwa lawama nzito. Marefa hufanyiwa
fujo na kupigwa na mashabiki, labda alihofia hali hiyo pia.
Dakika
ya 73 Simba walipata bao safi la kusawazisha lililofungwa kwa kichwa na
Mussa Hassan Mgosi, aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Yaw Berko
kufuatia shuti la mpira wa adhabu, lililogonga mwamba wa juu na
kudondokea nyavuni kabla ya kuokolewa na mabeki wa Yanga.
Halikuwa
bao lenye shaka yoyote, hakukuwa na kuotea wala dosari yoyote, lakini
haieleweki kwa nini Mbaga alilikataa bao hilo awali.
Ilikuwa
offside au mpira haukutinga nyavuni hadi akalikataa kwanza?
Haijulikani, lakini alilikubali baada ya wachezaji wa Simba kumuambia
aangalie kwenye TV iliyokuwapo uwanjani marudio ya tukio lile na baada
ya hapo akaenda kujadiliana na msaidizi wake, ndipo akalikubali.
Mbaga alichemsha- lakini si Mbaga tu, marefa wengi wa Tanzania waliwahi kutokota kabla yake na nitakumbushia baadhi ya mechi.
Machi
31, mwaka 2002 katika fainali ya Kombe la Tusker, Simba ikishinda 4-1,
refa Abdulkadir Omar 'Msomali' aliivuruga mechi na kuvuruga amani
uwanjani pia kwa madudu yake.
Kwa
nini? Katika mechi hiyo ya fainali iliyohudhuriwa na rais mstaafu wa
awamu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi,
chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka Suleiman kufunga bao
ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter,
aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa.
Rais
wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara
wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi
mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa
Yanga. Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo
akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia
mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania,
(FAT), sasa TFF kabla ya kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo baadaye.
Agosti
18, mwaka 2002 Simba na Yanga zikitoka sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi
Kuu, refa Victor Mwandike aliwaacha mashabiki wa Simba midomo wazi kwa
kuwapa Yanga penalti dakika ya 89 na ushehe, ambayo Sekilojo Chambua
aliitumia vema kuisawazishia bao timu yake, baada ya Simba kutangulia
kufunga kupitia kwa Madaraka Suleiman dakika ya 65.
Oktoba
24, mwaka 2007, refa Osman Kazi alikataa mabao matatu yaliyofungwa na
Yanga, yote akidai kipa Juma Kaseja alisukumwa na wachezaji wa Yanga,
lakini kwa yeyote atakayerudia kuangalia DVD ya mchezo ule, hawezi kuona
ukweli wa madai ya Kazi.
Awali
ya hapo, Kazi aliwahi kupuliza filimbi ya kumaliza dakika 45 za kipindi
cha kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la Tusker mwaka 2005 mjini
Mwanza, wakati mchezaji wa Yanga, Said Maulid 'SMG' amekwishawatoka
mabeki wa Simba na anakwenda na mpira mbele yake amebaki Juma Kaseja tu.
Refa
ni mwamuzi wa mwisho- lakini kwa wana Yanga walijutia mno tukio lile
kwenye mchezo ambao mwishowe walifungwa 2-0, kwa mabao ya kipindi cha
pili ya Emmanuel Gabriel na Mussa Mgosi.
Aprili
19, mwaka 2009, Jerry Tegete aliifungia Yanga bao la kusawazisha kwa
mkono na kutengeneza sare ya 2-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Refa
makini asingeweza kukubali bao lile, hivyo kwa haya yote lazima tukubali
marefa wa Tanzania hawawezi tena kuchezesha mechi za watani wa jadi.
Sababu
nyingine za marefa wetu kuzishindwa mechi hizo ni mapenzi yao kwa moja
ya timu hizo, kitu ambacho Misri wamekiepuka na mechi ya Zamalek na Ahly
inachezeshwa na marefa kutoka nje ya nchi yao.
Nakumbuka
refa kutoka Uganda, Dennis Bate aliyechezesha Nusu Fainali ya Kombe la
Tusker mwaka 2009 kati ya Simba na Yanga, aliiongoza vizuri mechi hiyo
na akadhibiti ujanja wote wa wachezaji kutaka kumdanganya na hatimaye
aboronge.
Kuna wachezaji
wanaitwa wazoefu wa mechi za Simba na Yanga na hawa wamekuwa
wakiwapoteza sana marefa kwa uzoefu wa kucheza mechi hizo, lakini kama
marefa watatoka nje ya Tanzania, tena wa kiwango cha beji za FIFA,
uhondo wa mechi za watani utaongezeka maradufu.
Zaidi
ya mara mbili sasa naandika juu ya mechi za watani wa jadi
kubadilishiwa marefa, lakini wakubwa wameendelea kukaa kimya- labda
wanajua wanachokifanya, ila ukweli ulivyo kwa sasa, marefa wetu
hawaziwezi tena mechi hizi.
Sioni
kuna tabu gani TFF kualika marefa wa nchi jirani kuja kuchezesha mechi
hii, ili kuondoa hofu kwa timu zote kabla ya kuingia uwanjani juu ya
marefa. Wana hoja, kwa sababu uzoefu unawapa wazi kwa asilimia kubwa
marefa wa hapa nyumbani huzishindwa mechi hizo, iwe kwa bahati mbaya,
kurubuniwa au utashi.
Wadhamini
wa Ligi Kuu, Vodacom wanataka ligi hii iwe bora na mfano wa kuigwa,
sidhani kama hawatakuwa tayari kutenga bajeti ya marefa wa kigeni kwa
ajili ya mechi mbili kila msimu.
Simba
na Yanga, zote zinadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, ambao
dhahiri wanataka nembo yao itangazwe na kitu chenye thamani na hadhi
kubwa, sidhani kama hawatakuwa tayari kusaidia kuziwezesha mechi hizo za
watani zichezeshwe na marefa wa nje. Kwa kifupi, sijui tatizo liko
wapi.
Chanzo:http://bongostaz.blogspot.com
Posted by
Unknown
12:59 AM