PINDA, MAWAZIRI HATARINI KUNG'OLEWA
Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na mawaziri wake wawili; Khamisi Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo David wameingia matatani kutokana na shinikizo linalowataka wang’oke katika nafasi zao.Pinda pamoja na mawaziri hao wanatakiwa kuachia ngazi kama hatua ya kuwajibika kutokana na matukio ya vifo na baadhi ya watu kujeruhiwa, katika matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili kwa upande mwingine.
Jana wabunge walicharuka na kuwataka mawaziri waliohusika katika Operesheni Tokomeza Ujangili wawajibishwe wakieleza kutoridhishwa na maelezo waliyoyatoa mapema jana, baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Kelele za wabunge zilizuka baada ya wabunge kuanza kuchangia maelezo ya Serikali kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima, hifadhi za wawekezaji na maelezo ya Serikali kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili.
Aliyekuwa wa kwanza kuchangia mjadala huo ni Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola (CCM) ambaye katika hitimisho lake alitoa hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kile ambacho alikiita kuwa ni unyanyasaji wa wafugaji na uporaji wa mifugo yao.
Profesa Msola alielekeza shutuma zake kwa Serikali kuwa ilifanya operesheni zake kwa pupa bila kufanya maandalizi hivyo kuwaathiri wananchi wasiokuwa na hatia.
Spika wa Bunge, Anne Makinda kabla ya kuahirisha kikao cha Bunge jana mchana aliridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji, wakati ‘madudu’ ya Operesheni Tokomeza Majangili yatachunguzwa kupitia Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Chimbuko la hoja
Jana asubuhi kabla ya Bunge kuanza kikao chake, Spika Makinda alitoa taarifa kwamba Kikao cha Kamati ya Uongozi kingekutana wakati kipindi cha maswali na majibu kikiendelea, kwa lengo la kutoa mwelekeo wa mjadala wa hoja za dharura.
Hoja hizo ni zile zilizotolewa na wabunge wawili kwa nyakati tofauti; Alphaxard Kangi Lugora wa Mwibara (CCM) kuhusu Operesheni Tokomeza Majangili na Saidi Nkumba wa Sikonge (CCM), kuhusu vita baina ya wakulima na wafugaji.
Kamati hiyo ilikutana baada ya kipindi cha maswali na majibu na Spika Makinda alitoa taarifa za kusitisha shughuli nyingine, ili wabunge waweze kujadili masuala hayo ambako kabla ya kuanza mjadala aliwaita mawaziri kutoa taarifa zao.
Alianza Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki ambaye katika maelezo yake alihitimisha kwa kutangaza kusitisha Operesheni Tokomeza ili kupitia mpango huo na kufanya maboresho ili kuondoa upungufu uliopo.
Licha ya kueleza sababu nyingi zilizofanya Serikali kuendesha operesheni hiyo, alisema ina manufaa makubwa katika kuokoa wanyama aina ya tembo, lakini waziri alihitimisha kwa kusema itakuwa ni busara kuifanyia tathmini wakati ikiendelea, hivyo kutangaza kuisitisha mara moja.
Kwa upande wake Dk Mathayo alitoa maneno ya kuomba radhi na kuwapa pole watu waliopatwa na usumbufu ikiwa ni pamoja na kupoteza mali zao na mifugo.
Mathayo aliwaeleza wabunge kuwa Serikali imepanga kujenga malambo katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji kupata maji ili kupunguza safari za kuhamahama kutoka eneo moja kwenda jingine.
Shinikizo kwa Pinda
Baada ya kumaliza hotuba zao, wabunge kadhaa walipata nafasi ya kuchangia maelezo hayo huku wengi wakielekeza shutuma zao kwa mawaziri hao na wenzao wa Mambo ya Ndani ya Nchi na yule wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Wabunge wawili wa Chadema, Paulina Gekul (Viti Maalumu) na John Shibuda (Maswa Mashariki) walitaka Waziri Mkuu Pinda ajiuzulu kutokana kushindwa kwake kudhibiti mauaji na mateso kwa wananchi.
Gekul alisema kinachotokea sasa ni utekelezaji wa kauli ya Pinda aliyoitoa bungeni akisema wahalifu wapigwe tu pamoja na ile ya Kagasheki aliyoitoa mjini Arusha akisema majangili watakaokamatwa wamalizwe hukohuko kwenye hifadhi.
Mbunge huyo alieleza operesheni hiyo kwamba imesababisha mauaji ya watu wasio na hatia ikiwemo mama Emiliana ambaye alifuatwa akiuza nyanya, lakini akateswa hadi kufa na hadi sasa mwili wake bado uko katika Hospitali ya Babati baada ya wananchi kugoma kuuzika.
Shibuda kwa upande wake alisema Pinda anapaswa kufungua milango kwa mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu haraka, kutokana na kulea uzembe ambao umesababisha madhara makubwa kwa wafugaji.
Shibuda alisema kuwa Wizara ya Mifugo imekuwa na mtazamo hasi lakini akasisitiza kuwa uzembe wa viongozi wa ngazi za mikoa, wilaya hadi vijiji unatokana na ukimya wa Pinda ambaye anashindwa kuchukua hatua yoyote dhidi yao.
Wabunge wengine
Kwa upande wake Nkumba aliunga mkono kuundwa kwa kamati teule, lakini akasisitiza kuwa mawaziri hao wanne wana hoja za kujibu ndani ya chama tawala CCM na kwa Rais, vinginevyo Serikali haipaswi kuendeshwa na viongozi wazembe wa aina hiyo.
-Mwananchi