Wakurugenzi 70 Vinara Mtandao wa Ufisadi.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda
KAMATI ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),
imebaini mtandao wa ufisadi unaoshirikisha wakurugenzi 70 wa halmashauri
mbalimbali hapa nchini ambao wanashirikiana na baadhi ya watendaji wa
Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kitengo cha
Hazina.
Baadhi ya halmashauri hizo ni pamoja na Wilaya ya Monduli, Arusha, Mwanza, Mbeya na Ilala.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mohamed Mbarouk alisema keshokutwa
atataja majina ya wakurugenzi hao ili wananchi waweze kuwafahamu.
Mbarouk alisema kuwa Tanzania Bara ina halmashauri 134, kwa hiyo ina
maana zaidi ya nusu ya wakurugenzi wanajihusisha na mambo hayo.
“Baadhi ya wakurugenzi hao walihamishwa kwenye vituo vyao vya kazi
kutokana na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali, lakini bado
wanajihusisha na mambo haya,” alisema Mbarouk.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imepanga kukutana kesho na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia ili
kuzungumzia suala hilo.
“Kuna zaidi ya wakurugenzi 70 wako kwenye mtandao wa ufisadi kwa
kushirikiana na watendaji wa Hazina na Tamisemi, jambo ambalo
limesababisha halmashauri zao kupata hati chafu kwa miaka mitano
mfululizo,”alisema Mbarouk.
Aliongeza wakurugenzi hao wamekuwa wakishirikiana na wahasibu wao
katika kutumia vibaya fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya
kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri zao.
Akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe ambapo
halmashauri yake imefanya vibaya katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini hajachukuliwa hatua na badala
yake amekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Alisema mbali na halmashauri hiyo, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Rhoda Nsemwa ambaye alisimamishwa
kazi kutokana na tuhuma za ufisadi, lakini bado anaendelea kupata
mshahara na stahiki zake kama mtumishi aliye kazini.
“Tumeshangaa kuona kuwa, aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Bagamoyo bado anaendelea kulipwa mshahara, kodi ya nyumba na
marupurupu mengine kama ofisa aliye kazini wakati ana kesi ya matumizi
mabaya ya fedha za Serikali,” alisema.
Alibainisha kamati hiyo pia imebaini kuwa Takukuru inajihusisha moja
kwa moja na vitendo vya rushwa, kutokana na kupotosha ukweli wa taarifa
za watuhumiwa na kuchelewesha kuwasilisha jalada mahakamani.
“Ukiangalia kesi zilizoko mahakamani ambazo upelelezi wake bado
unaendelea utaona wazi kuwa Takukuru ni miongoni mwa watu wanaopokea
rushwa, jambo ambalo limesababisha kuchelewesha upelelezi au kupindisha
ukweli,” aliwatuhumu.
Akizungumzia tuhuma hizo, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema,
“Hazina kuna taratibu na sheria kuhusu matumizi ya fedha na kama jambo
hilo limefanyika kweli ni wazi kuwa litakuwa kinyume na sheria na
taratibu zilizopo.”
Alisema licha ya kuwa mpaka sasa hajasikia malalamiko yoyote,
aliahidi kufuatilia jambo hilo ili kubaini ukweli na kwamba kama kuna
mtu atabainika atachukuliwa hatua stahiki. Alisema, “Ngoja tufuatilie
ili kujua ukweli.”
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim
Majaliwa aliomba atafutwe leo kwa maelezo kuwa atakuwa ameshapata
maelezo ya kutosha kuhusu tuhuma hizo.
“Sijajua hizo halmashauri ni zipi, pamoja na idara ambazo zipo chini
ya wizara hii, ngoja kwanza nizungumze na wahusika ambao pia najua
watanieleza kilinachoendelea, nitafute kesho (leo) nitatoa ufafanuzi wa
kina,” alisema Majaliwa.
Kamati yawabana Mambo ya Nje
Katika hatua nyingine; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
Kuu (PAC), imemwagiza CAG kufanya ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha
katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hasa katika
uendeshaji wa mikutano ya kimataifa.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gaudence Kayombo alisema jana
alipokutana na viongozi wa wizara hiyo kuwa kuna matumizi makubwa ya
fedha katika uendeshaji wa mikutano ya kimataifa.
“Kamati itamwandikia CAG, afanye ukaguzi maalumu ili kubaini utata
unaoonekana katika matumizi ya fedha ya wizara hiyo hasa kwenye eneo la
mikutano,” alisema Kayombo.
Kayombo alisema kutokana na utata huo, kamati imeona haiwezi
kuijadili ripoti hiyo ya fedha ya mwaka 2012/13 hadi CAG atakapofanya
ukaguzi maalumu.
Aidha, Kayombo aliwataka viongozi hao wataje gharama za Ukumbi wa
Mwalimu Nyerere uliojengwa kwa mkopo na msaada wa Serikali ya China,
lakini Katibu Mkuu wa wizara hiyo, John Haule alisema ataitaja baadaye
baada kujiridhisha.
“Tunataka kufahamu gharama za ujenzi wa jengo hilo, vifaa
vilivyosamehewa kodi ili kamati iweze kujua, kwa sababu hadi sasa
haieleweki umegharimu kiasi gani,” alisema Kayombo.
Hata hivyo, alisema asilimia 46 ya gharama za ujenzi wa jengo hilo ni
msaada wa Serikali ya China huku asilimia 54 ikiwa ni mkopo.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz