MWALIMU MKUU ANASWA NA MAGUNIA 6 YA BANGI.
MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Mukubu, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Silidion Kaiza (43), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na bangi gunia sita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 17, mwaka huu, shuleni hapo katika kata na kijiji cha Muganza majira ya saa tano asubuhi.
Alisema kuwa raia wema walitoa taarifa kituo cha polisi Rulenge kwamba kuna mwalimu anajihusisha na biashara ya kuuza dawa za kulevya, jambo walilohofia kuwa huenda akawaathiri wanafunzi wa shule hiyo kwani anazihifadhi shuleni.
Kalangi alifafanua kuwa baada ya polisi kupata taarifa hiyo walifika shuleni hapo na kumhoji mwalimu Kaiza, na alikiri kufanya biashara hiyo kisha akawapeleka katika moja ya darasa ambalo alikuwa akitunza bangi hiyo.
Kamanda alisema kuwa baada ya polisi kukamata bangi hiyo, waliifikisha kituoni na kwamba mwalimu huyo anaendelea kuhojiwa kisha atafikishwa mahakamani wakati wowote ili kujibu tuhuma hizo.
Aliwataka wananchi kuendelea kuwafichua wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya uuzaji wa dawa za kulevya ambavyo vimekuwa tishio kwa taifa.