MNEC AWATAKA VIJANA KUFANYA KAZI
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya
Tanga (MNEC), Kasimu Kisauji, amewataka walezi na wazazi wilayani humo
kuwahimiza vijana kufanya kazi kwa bidii na kuacha kukaa vijiweni,
hatua inayochangia kutumia muda mrefu kufikiria vitendo viovu.
Kisauji alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumza na vijana
wa shina la Yebo Yebo, Kata ya Ngamiani Kusini jijini Tanga katika
ziara ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana Mkoa wa Tanga (UVCCM) iliyokuwa na
lengo la kuupa uhai umoja huo.
Alisema iwapo vijana watakuwa mstari wa mbele kuwajibika kwa kufanya
kazi itawasaidia kuwa na maisha bora ambayo yatawawezesha kuinua
familia zao na jamii kwa ujumla, hali ambayo inachangia kuongezeka kwa
pato lao.
Alisema vijana wamekuwa wakidanganyika kwa kuambiwa kuwa vijiweni ni
sehemu ya kubadilishana mawazo, hatua inayowafanya waonekane kama
ombaomba kila wakati.
“Maisha bora lazima yaendane na kufanya kazi na si kukaa vijiweni,
vibarazani na kuanza kupiga soga zinazorudisha maendeleo nyuma,”
alisema.
Akizungumzia suala la mikopo ya vijana na kina mama inayotolewa na
halmashauri, Kisauji aliwataka vijana kuacha kulalamika badala yake
wajiunge kwenye vikundi vitakavyowasaidia kuwezeshwa kupata mikopo
hiyo.
Aliwataka madiwani wa halmashauri ya jiji hilo kuhakikisha
wanasaidia kina mama na vijana ili waweze kupata mikopo hiyo bila
kuwepo usumbufu.