Vigogo wilayani Handeni wafikishwa mahakamani kwa ufisadi wa Milioni 600
Watuhumiwa
kadhaa walijitetea kuwa wanamatatizo hivyo wanaomba kusaidiwa kupata dhamani
lakini hakimu alisema kuwa haiwezekani kutokana na vifungu vilivyotajwa
vinambana kutoa ruhusa hiyo. waliofikishwa mahakamani walikuwa tisa kutokana na
kwamba Mosha amelazwa katika hospitali ya wilaya baada ya juzi kukamatwa kisha
kupata mshituko uliosababisha alazwe hospitali, huku Tatala ametolwa taarifa
kwamba amelazwa Muhimbili na Lyimo hajapatikana na anatafutwa huku hakimu
akisisitiza watu hao watafutwe.
Na Mwandishi Wetu, Handeni.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
wilayani Handeni mkoani Tanga,imewapandisha kizimbani watumishi 12 wa
halmashuri hiyo wakiwatuhumu kutumia nyaraka mbalimbali ambazo ni hati za
malipo (payment voucher) na kujipatia fedha isivyo halali. Watumishi
waliofikishwa mahakamani ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo
Mpangalukela Tatala, Erasto Vicent ambaye alikuwa injinia wa maji,
Mkurugenzi
wa kampuni iliyokuwa ikifanya utafiti wa kutafuta maji Beda Joseph, Julius
Mhando ofisa maendeleo ya jamii, Ofisa Afya wa wilaya Benson Bundala na Maajabu
Kambi aliyekuwa mhasibu wa halmashauri hiyo.
Wengine ni fundi bomba Shabani Mfundo na Ahmad Buraa,
Raphael Nkoba aliyekuwa ofisa Afya na sasa ni ofisa afya halmashauri ya mji
Handeni, Michael Mosha mkaguzi wa ndani, Hemed Kandarua aliyekuwa dereva na
Violeth Swai ambaye ni ofisa elimu sayansi Kimu.
Akiwasomea mashitaka hayo Mwendedsha Mashitaka wa
Takukuru Samwel Gabriel akisaidiwa na Sweetbert Rwegasira mbele ya hakimu mkazi
mfawidhi wa mahakama ya wilaya Handeni Patrick Maligana, alisema kuwa katika
mwaka 2005 hadi 2007 kwa nyakati tofauti watumishi hao walitumia hati za
malipo,(payment voucher) na kujijazia na kumdanganya mwajiri wao kuwalipa pesa
kwa ajili ya kazi mbalimbali wakati kazi hizo hazikufanyika kama walivyoomba.
Mwendesha mashitaka huyo alisema kuwa kutokana na
kitendo hicho watuhumiwa hao waliisababishia serikali hasara ya Sh.
654,944,492.37 kwa kutumia hati za malipo ya uwongo wakiwa na lengo la
kumdanganya mwajiri wao.
“Mheshimiwa hakimu kutokana na kitendo hicho
watuhumiwa hawa waliisababishia serikali hasara ya Sh. 654,944,492.37 kwa
kutumia hati za malipo ya uwongo wakiwa na lengo la kumdanganya mwajiri wao
ambapo pesa hizo ni miongoni mwa fedha ambazo zilitolewa na benki ya Dunia kwa ajili
ya kufadhili mradi wa kuchimba visima virefu wilaya Handeni,” alisema.
Baada ya watuhumiwa hao kusomewa makosa mbalimbali 49
na la 50 la jumla la kuchukua fedha za safari zikiwa hewa, mwanasheria huyo
alisema dhamana ipo wazi na masharti ya dhamana lazima yazingatiwe chini ya
kifungu cha 148 (5) cha sheria ya uhujumu uchumi chenye mashariti ya kuwa
mtuhumiwa anatakiwa kutoa kiasi sawa na thamani ya mali ya kesi inayomkabili,
hivyo kutakiwa watoe milioni 54 kila mmoja.
Alisema kila mshitakiwa anatakiwa kulipa nusu ya mali
anayotuhumiwa nayo ikiwa ni kuanzia shilingi milioni 10 atatakiwa kulipa nusu
yake hivyo washitakiwa hao kwa kuwa wanadaiwa kiaisi cha shilingi milioni 600
walitakiwa kila mmoja kulipa shilingi milioni 54 papo hapo na mdhamini pia
anatakiwa kutoa fedha hiyo.
Baada ya wanasheria hao kuwasilisha maombi hayo,
hakimu Maligana, alisema kwamba kutokana na vifungu vya sheria ya dhamana
vilivyotolewa na takukuru inambidi kuchukua siku saba kusoma sheria hiyo kabla
ya kutolea uwamuzi wake, hivyo watumiwa hao walirejeshwa rumande hadi 13 mwezi
huu.
Washitakiwa wote walikana mashitaka lakini
walirudishwa tena rumande kutokana na hakimu kuomba muda wa kupitia sheria hiyo
na kusema kuwa hawezi kutoa jibu la papo kwa hapo ni lazima afuatilie katika
kesi kama hizo kuwa ni maamuzi gani yanachukuliwa.
“Kwanza naomba kuagiza washitakiwa wasiokamatwa
wakamatwe haraka,waliohospitali watasomewa mashitaka yao huko huko na mliobaki
hapa siwezi kusema mtapata dhamana au hapana kwani nahofia kufanyakazi
kiholelaholela ila nipate muda wa kujiridhisha na na vifungu hivi harafu baadae
ndio nitoe maamuzi hivyo watuhumiwa wote watarudi rumande hadi tarehe 13 mwezi
huu,”alisema Maligana.