Diwani aliyewekwa ndani na DC ajiuzulu

Diwani aliyewekwa ndani na DC ajiuzulu 


DIWANI wa Kata ya Mswaha-Darajani, Tarafa ya Mombo, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga (CCM), Aweso Kipaku (34), amejiuzulu nafasi hiyo akipinga hatua ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Mrisho Gambo, kumuweka ndani.

Akizungumza na mwandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Kipaku alisema Bw. Gambo aliagiza awekwe ndani Januari 24 mwaka huu, saa 11 jioni na kupata dhamana saa nne usiku.
Alisema polisi walimkamata, kumpeleka Kituo cha Korogwe lakini Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani, alikwenda kumuwekea dhamana na kufanikiwa kutoka.
Mbali ya Kipaku, wengine waliokamatwa na kuwekwa ndani ni Ofisa Mtendaji Kijiji cha Mswaha-Darajani, Bw. Abbas Siafu na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mswaha-Darajani, Bw. Said Kijiwa.
Chanzo cha kukamatwa kwao ni tuhuma zilizotolewa dhidi yao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya wakidaiwa kuchochea mgogoro wa wakulima na wafugaji kwenye Kijiji cha Mswaha-Darajani.
"Juzi tuliitwa kwa Mkuu wa Wilaya na viongozi wenzangu, baada ya kumalizika Kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Wilaya (Gambo) alimuamrisha OC-CID anichukue na kuniweka ndani hadi nilipopata dhamana usiku.
"Najiuliza mimi kiongozi wa wananchi nadhalilishwa kwa kufungwa pingu, kukaa chini tena nikisukumwa, je, wananchi wangu wapo salama kiasi gani... nimeamua kujiuzulu nafasi ya udiwani kwa vile nimedhalilishwa sana," alisema.
Kipaku alisema tayari ametoa taarifa ya kujiuzulu kwake kwa Katibu wa CCM mkoani humo, Gustav Muba jana ambapo zaidi ya wanachama 300 wa chama hicho wanaomuunga mkono wamerudisha kadi.
Aliongeza kuwa, sababu iliyomfanya awekwe ndani ni kitendo cha kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Kijiji uliofanyika Januari 21 mwaka huu na kudaiwa anachochea mgogoro wa wakulima na wafugaji.
"Wakulima wanataka wafugaji waondoke wakidai mifugo yao inakula mazao...Gambo aliahidi angekwenda kusimamia kazi ya kuwaondoa wafugaji kwenye eneo husika lakini hakufanya hivyo mara tatu, leo hii anasema sisi viongozi wa kata ndiyo tufanye kazi hiyo kana kwamba tuna Jeshi la Polisi," alisisitiza.
Alisema Januari 22 mwaka huu, watu wasiojulikana walikwenda kuchoma moto mazizi ya wafugaji lakini chanzo si viongozi wa kata ni viongozi wa Wilaya na Mkoa ambao wamechelewa kuchukua hatua za kumaliza mgogoro husika.
Juhudi za Majira kumpata Bw. Gambo kuzungumzia sakata hilo zilishindikana ambapo juzi alipigiwa simu lakini ilipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Alhajj Majid Mwanga akidai wapo Tanga kwenye kikao na kuhoji mnataka kuzungumza na Mkuu wa Wilaya kwa suala lipi.
Jana simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa ambapo Katibu wa CCM mkoani humo, Muba alikiri kupokea taarifa ya kujiuzulu diwani huyo lakini hakuwa tayari kuzungumza lolote akidai bado hawajajadili uamuzi wake kama wamkubalie au wamkatalie.
"Nimepewa taarifa hiyo lakini tunasubiri barua rasmi, sisi kama chama lazima tumjadili na turidhike na kile kilichofanya ajiuzulu, kama hakina mashiko tunajadiliana na kumuomba aendelee kuwa diwani," alisema Muba

Chanzo;Majira

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger