Featured Post Today
print this page
Latest Post

Habari zaidi juu ya kifo cha Dr. Sengondo Mvungi

Habari zaidi juu ya kifo cha Dr. Sengondo Mvungi

Mvungi_01_2d4e9.jpg

Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania imepata pigo baada ya mmoja wa wajumbe wake Dr. Sengondo Mvungi kufariki dunia nchini Afrika Kusini, ambako alikuwa akitibiwa.

Dr. Mvungi, alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi baada ya kuvamiwa na watu wanaoaminika kuwa majambazi nyumbani kwake mjini Dar, es Salaam, wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Bw. Assaa Rashid Dkt. Mvungi alifariki majira ya saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini akiwa katika Hospitali ya Milpark.

"Kwa masikitiko makubwa, Tume inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini amefariki dunia leo Jumanne, Novemba 12, 2013 saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini," amesema Bwana Rashid katika taarifa yake fupi.

Amesema taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Afrika Kusini kuja nchini Tanzania kwa mazishi zinaendelea.
Marehemu Dkt. Mvungi alisafirishwa siku ya Alhamisi, Novemba 7, 2013 kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) alipokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake.

Dkt. Mvungi pamoja na kuwa ni mwanasheria aliyebobea katika fani ya Katiba, pia ni mwanasiasa ambaye aliwahi kugombea urais mwaka 2005 kupitia chama cha NCCR Mageuzi.
0 comments

DC Muhingo ashikia bango la kuozeshwa kwa wanafunzi wilayani Handeni

DC Muhingo ashikia bango la kuozeshwa kwa wanafunzi wilayani Handeni

Na Rajabu Athuman, Handeni
ONYO limetolewa kwa viongozi mbalimbali wa halmashauri ya wilaya ya Handeni watakaojihusisha na kushiriki kuwaozesha wasichana walioko shuleni ya kuwa yeyote atakae bainika amefanya hivyo adhabu kali itachukuliwa juu yake kutokana na wimbi la kuwaozesha wanafunzi wa kike wilayani humo.

Onyo hilo limetolewa jana na mkuu wa wilaya ya Handeni Muhingo Rweyemamu kwa kusema kuwa hataweza kuvumilia baadhi ya viongozi kushiriki kuwaachisha wasichana shule na kuwatafutia wanaume waolewe kwa kusema kuwa mwanafunzi sio mke aachwe asome kwanza ili wajikomboe kimaisha.
Alisema kuwa kwa kuanza zoezi hilo tayari mtendaji wa kijiji cha Pozo ameshakamatwa kwa kosa la kushiriki kuwezesha kuolewa kwa mwanafunzi Sikujua Mganga mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Pozo ambapo mtendaji huyo alishiriki mchakato mzima wa mwanafunzi huyo hadi kumsafirisha na kumpeleka Dar Es Salaam.

“Kiongozi yeyote wa halmashauri ya wilaya ya Handeni akigundulika amehusika na kuozesha mwanafunzi adhabu kali juu yake lazima ipite,inasemekana kuna wakuu wa shule,viongozi wa dini na baadhi ya viongozi wengine wanahusika katika hili kwakweli siwezi kuvumilia nikikugundua siwezi kukuacha naanza na huyu mtendaji wa kijiji cha Pozo wengine mtafuata”alisema Rweyemamu.

Mkuu huyo wa wilaya amewataka pia viongozi wa dini kuzingatia sheria za nchi kwa kutowafungisha ndoa watu ambao wanawasiwasi nao na iwapo watabaini mhusika ni mwanafunzi watoe taarifa haraka katika vyombo husika ili mhusika akamatwa huku akimuagiza afisa elimu wa shule za msingi kufuatilia suala hilo.

Aidha alizitaja shule ambazo zinaongoza kwa utoro wilayani humo kuwa ni shule ya msingi Mazingara,Kweditiribe na Pozo ambapo mkakati wa kuitisha mkutano wa wazazi unafanyika ili kuweza kuwaelimisha wazazi umuhimu wa elimu kwa watoto wao.

Kauli hiyo ya mkuu wa wilaya inakuja baada ya kugundua kuwa idadi ya wanafunzi watoro katika shule za msingi imeongezeka zaidi na kubainika kuwa wengi wa wanafunzi hao niwakike na imebainnika kuwa wameozeshwa.Wilaya hiyo iliathirika zaidi mwaka jana kwa tatizo la mimba ambapo ilikuwa ni asilimia 11 lakini kwasasa ni asilimia 0.1 na kumezuka suala la kuwaozesha tena wanafunzi.
0 comments

DIWANI ATAKA SOKA LA DEEPSEA LIVUNJWE

DIWANI ATAKA SOKA LA DEEPSEA LIVUNJWE



NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
DIWANI wa Viti Maalumu Kata ya Chumbageni jijini Tanga kupitia chama  cha Mapinduzi (CCM)Saida Gadafi amelishauri baraza la madiwani kuridhia soko la kuuzia samaki la deepsea livunjwe kuliko kila mwaka litengewe sh.milioni 50 kwa ajili ya ukarabati wake.
Gadafi alitoa kauli hiyo  wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa mipango miji jijini Tanga ambapo alisema fedha hizo zinazotengwa hazionekani zinafanyia kazi gani kwa sababu ukarabati wenyewe hauonekani kama umefanyika.
Alisema kitendo hicho kinapelekea kurudisha nyuma kasi ya maendeleo ya halmashauri hiyo na kueleza kwa maslahi yake inabidi soko hilo livunjwe lakini mchakato huo uendane na kuwashirikisha wataalamu ili waweze kuamua nini kifanyike.
Diwani huyo alisema lazima madiwani wahakikishe wanakuwa mstari wa mbele kusimamia maslahi ya wananchi wanaowaongoza ili kuondoa kero zao lengo likiwa ni kuwapa maendeleo.
  “Kila mwaka zilikuwa zikitengwa milioni 50 kwa ajili ya ukarabati wa soko hilo lakini watu walikuwa hawazisema ila hizo milioni 11 kwa ajili ya kupewa mtathimini zimekuwa zikileta maneno naamini wataalamu tunao kwenye halmashauri waamue nini cha kufanya pale lakini hilo soko bora livunjwe “Alisema Gadafi.
Akizungumza suala hilo,Mjumbe wa Kamati wa Fedha,Shehe Fadhili Bwanga alisema masuala ya kuvunjwa soko hilo ni kutokana na kuona kuwa halikidhi haja ya kuendana na hadhi ya jiji na wao kupitia kamati ya fedha wameona zifuatwe sheria za nchi ikiwemo kuthaminiwa na kampuni zinazotambulika kiserikali ili ziweze kutoa idhini ya uvunjwaji wa jengo hilo.
Bwanga aliongeza kuwa uamuzi wa kuvunja soko hilo pia utatokana na gharama zake za sh.milioni 11 lakini sheria za uvunjwaji zilizowekwa inabidi zifuatwe kabla ya kuachukua maamuzi wa uvunjwaje wake.
0 comments

ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA KUOA BINTI WA MIAKA 18

ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA KUOA BINTI WA MIAKA 18

Na Oscar Assenga,Tanga.
MZEE wa Miaka sabini anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuoa binti mwenye umri chini ya miaka kumi na nane Mosa Hamisi kinyume cha sheria zilizopo hapa nchini.
Mkasa huo ulitokea Novemba 10 mwaka huu majira ya saa kumi na moja jioni ambapo mzee huyo tayari alishafunga ndoa na binti huyo lengo likiwa ni kuishi naye kama mke na mume.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,Constatine Massawe alithibitisha kutokea tukio hilo na kueleza tayari jeshi linamshikilia mtuhumiwa huyo pamoja na mama mzazi wa binti huyo.
Massawe alimtaja mzee huyo kwa jina la Abdallah Tuppa (70)mkazi wa barabara kumi mbili na mama mzazi binti huyo Batuli Tupa (35)ambaye anaishi barabara kumi na nne jijini Tanga.
Alisema tukio hilo liligunduliwa na wasamaria wema baada ya kuona binti huyo anaozeshwa ndipo walipoamua kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ambapo wakati polisi walipofika eneo hilo walimkuta mzee huyo akidai mke wake ndipo walipomkamata.
Kamanda Massawe alisema askari walifanikiwa kumuhoji binti huyo ambapo alisema umri wake ni zaidi ya miaka kumi na saba hali ambayo ilipelekea kumuambia alete cheti chake cha kuzaliwa ili kuthibiti umri huo.
Wakati huo huo,mtu mmoja amekufa baada ya kugongwa na gari akiwa anaendesha baiskeli katika barabara ya Segera –Chalinze.
Kamanda Massawe alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 3 za usiku na kumtaja dereva aliyesababisha ajali hiyo kuwa ni Abdallah Msangi (30) wa gari hilo aina ya fuso lenye namba T390 DCB.
Massawe alimtaja aliyefariki katika ajali hiyo kuwa ni Hamisi Saidi mkazi wa Michungwani ambapo alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva.
0 comments
 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger