CHAMA cha Netiboli (CHANETA) Mkoa wa Tanga, kimeanza kutoa semina
ya walimu wa michezo kutoka wilaya zote, lengo likiwa ni kuwaandaa kwa
ajili ya kufundisha kwenye michezo ya Umitashumta na Umisseta mkoani
Tanga.
Akizungumza jijini hapa juzi, Katibu wa chama hicho, Julieth Mndeme,
alisema semina hiyo ina lengo la kuwajengea uwezo washiriki na
kuhamasisha mchezo huo ambao unaendeshwa na mkufunzi, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Anna Kibira.
Mndeme alisema semina hiyo itaendeshwa kwa siku 11 na ilianza Januari
16 na itafikia tamati Januari 27 ikishirikisha wanawake na wanaume
kwenye viwanja vya Bandari.
Katibu huyo alisema mikakati waliyokuwa nayo katika kuuendeleza
mchezo huo ni kuanzisha ligi za vijana wadogo na kuweka msukumo kwenye
mashindano mbalimbali yakiwemo ya wilaya na mkoa.
Mndeme alisema ni matumaini yake mafunzo hayo yatakapomalizika
watapatikana walimu wazuri ambao watakuwa ni chachu ya kukuza maendeleo
ya netiboli kwenye wilaya wanazotoka na mkoa kwa ujumla.
Post a Comment