Iilikuwa mfano wa nguvu ya umma iliyoelekezwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipofanya ziara katika eneo la Mloganzila–Kwembe, jijini Dar es Salaam jana.
P.T
Umati wa watu walijitokeza wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe tofauti, wakasimama barabarani kuukwamisha msafara wa Pinda, wakilalamikia kupunjwa fidia, dhuluma na unyanyasaji waliofanyiwa baada ya serikali kutwaa ardhi yao.
Mloganzila iliyoko nje kidogo ya Dar es Salaam, imetwaliwa na serikali ili kujenga Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Tiba, pamoja na hospitali kubwa ya kisasa. Hatua hiyo inakusudia kukifanya chuo hicho kikuu cha Muhimbili kujitegemea na kuondoka kwenye majengo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Eneo hilo ambalo ni mali ya kampuni ya kusindika nyama ya Tanganyika Packers, iliyofilisika miaka ya 1980, lilibaki pori na wananchi kuliendeleza kabla ya serikali kulitangaza kuwa kijiji cha Ujamaa na watu kumilikishwa ardhi. Eneo linakaliwa na wanakijini wapatao 2,000.
'PICHA' ILIVYOANZA
Katika tukio la jana asubuhi, wanaume, wanawake na watoto waliokadiriwa kufikia 300, walikusanyika eneo la Kabimita wakiwa na mabango ya kulalamika, kulaani na kuitaka serikali iwape haki yao.
Kisha, walisimama barabarani kuuzuia msafara wa Pinda, tukio lililodumu kwa takribani dakika tano, hali iliyomlazimu (Pinda) kushuka kutoka ndani ya gari ili kuzungumza nao.
Pinda, aliwaambia wakazi hao kuwa analifahamu tatizo lao na kwamba ziara yake, ililenga a kuwasikiliza na kuwaeleza jinsi walivyojipanga kuwafidia. Alisema, hapakuwa na sababu ya kumzuia, bali walipaswa kufika katika mkutano ili wasikilizane.
"Najua kudai fidia ni haki na wajibu wenu, maelezo ya matatizo yenu ninayo, njooni niwape maelezo jambo lenu linajulikana njooni mnisikilize," alisema. Taarifa za ndani zilidai kuwa wakazi hao walipanga kuususia mkutano wa Pinda, lakini kwa kauli yake (Pinda) walikwenda kumsikiliza.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
UJUMBE WA MABANGO
Miongoni mwa mabango yaliandikwa hivi;
"Tunachotaka ni haki ya ardhi, Mheshimiwa Pinda usidanganywe fidia ya ardhi hatujalipwa, tumeishi hapa kwa zaidi ya miaka 50."
"Nyerere na Kawawa fufukeni muone udhalimu huu." Baada ya Waziri Mkuu kutoa kauli za kuwaalika mkutano, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, aliwaambia wananchi waweke mabango vizuri ili Pinda ayasome. "Mengine nitamkusanyia aondoke nayo ili akayasome..." alisema Mahiza.
SABABU ZA KUZUIA MSAFARA
Wananchi hao walidai walilazimika kumzuia ili kumshinikiza awasikilize na kutoa hatma ya madai yao, kwani walihofu asingekutana nao kwa vile taarifa za ziara yake eneo hilo hazikutangazwa kwa uwazi.
Awali, walipanga kulala chini ili wamzuie baada ya kuambiwa kuwa angefika Mloganzila kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali hiyo.
Pia alitarajiwa kuzindua barabara inayojengwa kuanzia Kibamba CCM hadi Kisopwa sehemu iliyotwaliwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali na Chuo Kikuu kipya cha Muhimbili.
Hata hivyo, wakazi hao walimzuia Pinda kwenda kwenye hema ambalo liliandaliwa kwa ajili ya kuhutubia, likiwa limewekwa kwenye ofisi za Kabimita na kufanya askari kudhibiti ghasia hizo.
ULINZI WAIMARISHWA
Kutokana na tukio hilo na kuwapo dalili za kutokea vurugu zaidi, polisi na walinzi wake walilazimika kulizingira gari la Pinda ili kumuepusha na kadhia hiyo. Hata hivyo polisi hawakutumia silaha wala vitisho kuwatawanya watu, badala yake diplomasia na ushawishi ulitumiwa zaidi kuwasihi wananchi.
Kabla ya kuzuia msafara huo walimkwamisha Mkuu wa Kituo cha Polisi Kimara , aliyefahamika kwa jina la CD Papalika, aliyefuatana na maofisa wengine wa jeshi hilo. Walizuiwa kwenda kwenye hema na jukwaa lililoandaliwa kwa ajili ya mkutano wa Pinda.
Pia wakazi hao walizuia lori namba T 972 BYG lililokuwa limebeba chimbuo (excavator) na katapila kwa ajili kusawazisha eneo la hema ambalo mkutano huo uliandaliwa. Kadhalika walizuia magari ya kikosi cha mbwa na maofisa wa polisi waliokuwa na mbwa hao wakitishia kuwa endapo watawashusha wangewaua.
Licha ya magari hayo kuzuiliwa hata msafara wa Waziri Mkuu uliokuwa na magari zaidi ya 26 likiwamo la Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Shukuru Kawambwa, Naibu Waziri wa Afya, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza nayo pia yalikwamishwa.
FIDIA KUANGALIWA UPYA
Akizungumza na wananchi hao, Pinda, alisema serikali imeamua kuwalipa fidia ya maendelezo ambayo ni gharama walizotumia kuendeleza sehemu zao, ikiwa ni pamoja na mazao na majengo , lakini hawatafidiwa ardhi kwa kuwa ilikuwa mali ya serikali.
Alisema kutokana na watu kumsihi kuwa fidia ni ndogo, iliyoanzia Sh 6,000 hadi 100,000, suala hilo litatazamwa upya na kuona kama serikali inaweza kuwasaidia.
CHANZO: NIPASHE