STAKABADHI GHALANI KITANZI CHA WAKULIMA
Mkulima wa korosho katika kijiji cha kichonda mkoa wa Mtwara, akipalilia shamba lake.
Mbali ya mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa kero, pia umeamsha uhasama wa kijamii, kulazimisha wanavijiji kuhama makazi yao ya asili na sasa baadhi ya wakazi wa mikoa ya Mtwara na Ruvuma wanaishi kwa majuto.
Mpango wa stakabadhi ghalani kwa wakulima wa korosho unaoratibiwa chini ya Sheria Namba 10 ya Stakabadhi Mazao Ghalani ya mwaka 2005, unathibitika kuwa umeshindwa kuleta matokeo ya kuridhisha chanya kwa wakulima wa korosho.
NIPASHE ilifanya ziara ya uchunguzi wa kihabari kufika kwenye maeneo tofauti yenye wakulima wa korosho hususani Kusini mwa Tanzania.
Unapozungumza nao kuhusu hatima ya maendeleo na uchumi wao unaotegemea korosho, wanaonekana kukata tamaa, wakielekezea kidole kwa serikali kwa kushindwa kuwakomboa, badala yake kuwaacha wakiathiriwa kwa namna tofauti, mojawapo ikiwa ni pamoja na matumizi ya stakabadhi ghalani.
Bodi ya Korosho (CBT) inaeleza kuwa Tanzania ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa zao hilo barani Afrika, ikizalisha wastani wa tani za ujazo 100,000 kwa mwaka.
Mwaka jana pekee, Tanzania ilizalisha tani 127,939.42 za korosho, ikitanguliwa na Nigeria na Ivory Coast. Duniani, Tanzania inashika nafasi ya nane katika uzalishaji wa zao hilo.
Hii ina maana kwamba kama ufanisi katika utekelezaji wa sera, mikakati na mipango inayolihusu zao hilo ingefanikiwa, wakulima wake wangepiga hatua kubwa kiuchumi na nyanja nyingine za maendeleo.
KARAHA ZA STAKABADHI GHALANI
Mfumo wa stakabadhi ghalani ulipoanzishwa msimu wa mwaka 2006/2007 wakulima na wadau wa korosho waliupokea kwa matarajio ya kuwakomboa kiuchumi.
Mfumo huo ulisababisha mkulima kuuza korosho kwenye Ushirika ambao ungemlipa bei ya soko, wakati huo zao hilo likitafutiwa mnunuzi kwa njia ya zabuni, hali ambayo ingesababisha kuwapo kwa malipo ya pili.
Wakati wote huo korosho iliundiwa utaratibu wa kuwekwa kwenye vifaa bora (magunia) na kuhifadhiwa katika maghala ili pamoja na mambo mengine, iwe salama na isipoteze ubora wake.
Hivyo, mkulima alipaswa kugharimia mahitaji hayo ambayo hata hivyo, kutokana na utambulisho ulioonyesha kuwapo manufaa yanayotokana na stakabadhi ghalani, walikubali.
Kabla ya kuanzishwa kwa stakabadhi ghalani, wakulima wa korosho waliuza zao hilo kupitia biashara huria, hivyo kusababisha kupunjwa bei, ingawa walipata fedha kwa wakati.
Stakabadhi ya mazao ghalani ikaanzishwa kwa mujibu wa Sheria namba 10 ya mwaka 2005, lengo likiwa ni kusaidiana na mifumo mingine ya masoko ili kuwezesha uuzaji wa mazao ya wakulima katika masoko ya ndani na nje.
Wakulima kadhaa wameelezea kutoridhishwa na utekelezaji wa stakabadhi ghalani, kwa madai kuwa licha ya kuwacheleweshea malipo ya awali, hakuna awamu ya pili ya ulipaji fedha za ziada unaofanyika, hivyo kuamini kwamba wananyonywa stahili zao.
Hali hiyo imeibua kundi la wakulima wa korosho wanaoachana na kilimo cha zao hilo na kujishughulisha na mazao ya aina nyingine ikiwamo mpunga.
Mohamed Matoro ni mkulima wa korosho katika kijiji cha Kitanda kilichopo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, anasema ameamua kuwekeza zaidi katika kilimo cha mpunga na kuachana na korosho.
Kabla ya uamuzi huo, alikuwa anamiliki shamba la korosho lenye ukubwa wa ekari nne. Haikujulikana anamiliki shamba la mpunga lenye ukubwa gani.
“Sijalipwa malipo yangu ya pili kwa mauzo ya msimu wa 2012/13, kwa miaka ya nyuma nililipwa nusunusu, kwa sasa sioni umuhimu wa kuendelea kung’ang’ania zao hili, nimeamua kujaribu maisha katika zao la mpunga,” anasema.
Matoro ana watoto watano wawili wanasoma katika shule ya msingi Kitanda na watatu wapo nyumbani wameshindwa kuanza elimu ya msingi kutokana na kushindwa kupata fedha zinazokidhi mahitaji ya familia yake.
Wapo wakulima mbalimbali wanaoishuhudia hali kama ya Matoro, wakionekana kukabiliwa na uduni wa maisha unaotokana na kipato kidogo cha korosho ambayo ni zao kuu la biashara kwao.
Wengine miongoni mwa wakulima wa korosho wameamua kujishughulisha na kilimo cha ufuta, wakisema mfumo wa ununuzi wake unaofanyika kati ya mkulima na mfanyabiashara anayelipa fedha kabla ya kuchukua mazao, unawapa uhakika zaidi wa kipato.
Imebainika kwamba licha ya utajiri unaotokana na korosho, wakulima wa zao hilo wana maisha duni yanayowafanya washindwe hata kuchangia huduma za kijamii kwenye maeneo yao.
Mathalani, wakazi wa kijiji cha Azimio wilayani Tunduru, hawana huduma ya maji hususani ya visima, hivyo kusafiri umbali wa kilomita tatu ili kuyafuata.
Maji hayo ya mto Matinjira hayakutegemewa katika miaka ya 1980 kutokana na kuwapo kwa visima vilivyoanzishwa na wahisani, vikasimamiwa, kugharimiwa na kuendeshwa na wakulima, lakini hivi sasa vimekauka.
Sababu ni kushindwa kumudu gharama ya kuviendesha ikiwa ni pamoja na kugharimia utunzaji wa mazingira yanayovizunguka.Si suala la maji pekee, hata wanapohitaji kusafiri, wakulima wengi wa korosho hawawezi kumudu gharama ya safari moja inayotozwa Sh. 2,000, badala yake wanatembea kwa miguu.
Hatua ya wakulima kuachana na korosho imejitokeza katika vijiji vya Kichonda na Mbuli wilayani Liwale katika mkoa wa Lindi ambako sasa wanazalisha mazao mengine yanayohitaji gharama ndogo kuliko ilivyo kwa korosho.
Mustapha Ng’ahama na Kasimu Ngahama ni wakulima wa korosho katika kijiji cha Kichonda, wanasema kilimo cha ufuta kimesababisha baadhi yao (wakulima) kuyahama makazi ya kudumu kwenda kulima ufuta maeneo ya mbali.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Zuberi Mnyuke, anatoa mfano kuwa takribani kaya 150 kati ya 256 zilizopo kijijini humo, zimeyahama makazi yao walipojihusisha na kilimo cha korosho kwenda vijiji vya mbali kulima ufuta.
STAKABADHI GHALANI NA MALIPO DUNI
Hali ya kutoridhishwa na malipo yanayofanywa kupitia stakabadhi ghalani inajitokeza pia kwa wakulima wa maeneo ya Masasi, Liwale, Tambahimba na Newala.
Hoja ya kuwapo manufaa ya ununuzi huru wa korosho uliofanyika kabla ya kuanzishwa kwa stakabadhi ghalani, inaungwa mkono na mkulima wa kijiji cha Ilala wilayani Tandahimba, Rashid Njopa.
Wakulima Hemed Mnukwile wa kijiji cha Mbuli wilaya ya Liwale mkoa wa Lindi na Ablai Mkuka wa kijiji cha Namiyonga wilaya ya Newala, wanasema gharama za uzalishaji wa korosho ni kubwa kuliko kipato kinachotokana na uuzwaji wake.
Mnukwile mwenye shamba la ekari 24 anaeleza kuwa tangu aanze kulima korosho mwaka 2002, hajaona maendeleo ya maana kutokana na kilimo hicho.
“Desemba mwaka jana nililipwa Sh. 345,000 kama malipo ya awali ya korosho, lakini hadi sasa sijalipwa malipo ya pili yanayofikia Sh. 534,000,” anasema.
Anafafanua kuwa aliuza kilo 879 za korosho huku akitumia gharama ya Sh. 543,000 tangu maandalizi ya shamba hadi mavuno.
Mnukwile anamiliki nyumba anamoishi, ikiwa imejengwa kwa tofali za udongo na kuezekwa mabati yaliyochakaa yakionyesha kutanda kutu huku ikiwa na madirisha yaliyozibwa kwa vipande vya miti na kufunikwa.
Kadhalika kitanda anacholalia kwenye nyumba hiyo ya vyumba viwili anavyovitumia na familia yake ya mke na watoto wawili wanaosoma katika shule ya msingi Mbuli, kimesokotwa kwa kamba za katani.
Naye mkulima Mkuka mwenye shamba la ekari 20, anasema Desemba mwaka jana alivuna kilo 3,500 za korosho zenye thamani ya Sh. 3,500,000, lakini aliambulia Sh. 650,000 kwa malipo ya awali.
Anasema hadi kufikia Februari mwaka huu, alikuwa hajalipwa fedha zilizobaki, huku akitaja gharama alizozitumia kwa kilimo zilifikia Sh. 932,500.
Hali ya kimaisha ya Mkuka ni duni, ikithibitika kwa kuishi kwenye nyumba ‘iliyochoka’ huku akishindwa kununua chakula cha kuhifadhi kwa ajili ya familia yake.
Mkulima mwingine, Ally Kamkole anakidai chama cha msingi cha kijiji cha Azimio Sh. 212,100. Alipata malipo ya awali ya Sh. 515,100 kutokana na kuuza kilo 606 za korosho. Gharama za uzalishaji wake zilikuwa Sh. 312,000.
Naye Abdallah Haji anakidai chama cha msingi Shilingi 907,900 tangu Desemba 22, 2011. Alipata malipo ya awali ya Sh. 2,204,900, kutokana na kuuza kilo 2,594, bei ya kilo moja ikiwa ni Sh. 1,200.
Wakulima hao kwa nyakati tofauti, wanasema Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Chande Nalicho, aliwatangazia wakulima kuwa hawatalipwa malipo hayo kutokana na mauzo kufanyika kwa hasara.
Hata hivyo, Nalicho alipofuatwa kulielezea suala hilo, alisema: “Kwa sasa sina muda, ninaenda kwenye maafa, nenda kwa Mkurugenzi wa wilaya atakupa majibu.”
Mkurugenzi wa wilaya hiyo aliielekeza NIPASHE ionane na Ofisa Kilimo Msaidizi Mkuu wa Tunduru, Fidelis Francis Nyakunga.
Nyakunga anakana na kusema: “Si kweli mkuu wa wilaya aliwatangazia wakulima kuwa hawatapata malipo yao ya pili.”
VIONGOZI: MAZINGIRA DUNI YANAKWAMISHA KILIMO CHA KOROSHO
Viongozi kadhaa wa serikali, wanathibitisha kuwapo mazingira yanayokwamisha ustawi wa wakulima wa korosho, hivyo kufifisha jitihada za kuliboresha zao hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Ephraim Mmbaga, anasema wapo wakulima wa korosho wanaoyahama makazi yao kwenda vijiji vya mbali kulima ufuta, wakiachana na kilimo cha korosho.
Mmbaga anasema miongoni mwa sababu zinazotajwa kwa ushawishi huo ni mazingira duni kwa kilimo cha korosho wakati zao kama ufuta, halihitaji gharama kubwa katika maandalizi, kulima na uvunaji wake.
Kwa mfano, anasema bei ya ufuta kwa msimu uliopita ilikuwa kati ya Sh. 2,000 hadi 2,800 kwa kilo moja, fedha zinazolipwa pasipo makato ama gharama kama zinazotozwa kupitia stakabadhi ghalani.
Pia Mmbaga anasema ufanisi duni wa mfumo wa stakabadhi ghalani unachangiwa na hujuma zinazofanywa na baadhi ya watendaji serikalini, lakini hawataji majina.
“Watendaji wachache wanatokea na kuwaibia wakulima, mfumo wenyewe ni mkombozi wa wakulima, hivyo hauna tatizo, tatizo ni watendaji,” anasema Mmbaga.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Farida Mgomi anasema stakabadhi ghalani bado haijaeleweka vizuri kwa wakulima na kwamba wengi wao (wakulima) wanadhani kuwa unawanyonya.
“Kinacholeta msuguano juu ya mfumo wa stakabadhi ghalani ni elimu ndogo waliyonayo wakulima, pamoja na hatua ya ukopaji wa vyama vya ushirika katika benki,” anasema.
Anasema moja ya sababu zinazochochea uelewa duni ni kushindwa kwa maofisa ugani kuwatembelea wakulima vijijini.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kichonda, Mnyuke anasema robo tatu (sawa na watu 264) ya wakazi wa Kichonda wanaokadiriwa kuwa 350 ‘wamekimbilia’ katika vijiji vya Milui, Kiangale, Kipelele, Naujombo, Kimumbi, Zinga, Likawage na Nanjilinji ili kushiriki kilimo cha ufuta.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment