Kamati
ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeshindwa
kusikiliza pingamizi mbili zilizowasilishwa mbele yake dhidi ya waombaji
uongozi wawili baada ya kukosa sifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za
TFF.
Kwa
mujibu wa Ibara ya 11 (3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, pingamizi ni
lazima iwekwe na mwanachama wa TFF (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa,
vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) au kiongozi wa kuchaguliwa wa TFF.
Pia
pingamizi yoyote ni lazima iwe kwa maandishi ikieleza wazi sababu za
pingamizi pamoja ushahidi wa kuunga mkono pingamizi hilo, jina kamili,
anuani ya kudumu na kusainiwa na mweka pingamizi au Mwenyekiti/Katibu wa mwanachama husika.
Pingamizi
hizo ziliwasilishwa na Shamsi Rashid Kazumari na Samwel Nyalla dhidi ya
Wallace John Karia anayeomba kuwania nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF na
Vedastus Kalwizira Lufano anayeomba kuwania ujumbe wa Kamati ya
Utendaji kupitia Kanda Namba Mbili ya mikoa ya Mara na Mwanza.
Kwa
upande wa Kazumari ambaye alikiri hata kutowahi kuiona Katiba ya TFF
pamoja na Kanuni za Uchaguzi, pingamizi lake halikusikilizwa kwa vile si
mwanachama wa TFF wala kiongozi wa kuchaguliwa wa TFF. Wakati pingamizi
la Nyalla halikusikilizwa kwa vile hakukuwa na ushahidi wowote
uliowasilishwa, hivyo kushindwa kukidhi matakwa ya Ibara ya 11(3) ya
kanuni husika.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Posted by
Unknown
6:16 AM