WABUNGE WA TANZANIA NAO WASUSIA KIKAO CHA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI.
Kikao cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA), jana kilivunjika kwa mara ya pili baada ya Wabunge wa Tanzania, kutoka ndani ya ukumbi wakipinga kanuni kuvunjwa juzi.Baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje, Spika wa Bunge hilo, Margareth Zziwa aliahirisha Bunge kwa dakika 15 ili kuweka mambo sawa, lakini jitihada za kuwashawishi ziligonga mwamba na kuamua kuahirisha Bunge hadi leo.
Awali,
Mbunge Abdullah Ali Hassan Mwinyi alitoa msimamo wa wabunge wa Tanzania
kuwa walitoka, kupinga kitendo cha wabunge wengine kudharau kiti cha
Spika juzi na kutoka nje ili kushinikiza hoja yao.
Mwinyi
alisema ili kushinikiza kuheshimiwa kiti cha Spika, wameamua kutoka nje
ya ukumbi huo kwa kuonyesha hawaungi mkono, tabia ya baadhi ya wabunge
kushinikiza hoja zao, kujadiliwa na Bunge hata kwa kukiuka kanuni na
taratibu.
“Jana(juzi)
ilikuwa ni mara ya pili wenzetu, kudharau kiti cha Spika na kutaka
kutoa hoja na kujadiliwa bila kufuata kanuni, sasa tumeona ni vizuri na
sisi kwa kupinga kuvunjwa kanuni, tutoke ili kuonyesha tunapinga mchezo
huu,” alisema Mwinyi.
Mwinyi
alisema kitendo cha wabunge wenzao kutoka nje ya ukumbi kwa kukataliwa
kuvunja taratibu, kinadhalilisha kiti cha Spika na hata wabunge wenyewe.
Mbunge
mwingine wa Tanzania, Twaha Taslima alisema kanuni zipo wazi kuwa kama
mbunge ana hoja na kutaka Bunge lijadili mambo ambayo si ya dharura ni
lazima aiwasilishe saa 24 kabla kwa Spika.
“Sasa
jana(juzi), Mbunge wa Kenya, Peter Mathuki alitaka hoja yake ya kutaka
utaratibu wa kufanyika bunge kwa mzunguko ijadiliwe kitu ambacho
hakikuwa sahihi,” alisema Taslima.
Muthuki, juzi aliungwa mkono na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), isipokuwa Tanzania.
Jana aliwasilisha hoja hiyo kwa kufuata utaratibu lakini haikujadiliwa baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje.
Katika
hoja hiyo, msimamo wa wabunge wa Tanzania na Kamati ya Uongozi ya Bunge
ni kuwa vikao vyote vifanyike katika ukumbi wa Bunge, Arusha baada ya
kukamilika.
Wabunge wa Tanzania ambao jana walitoka ni Shyrose Bhanji, Profesa Nderakindo Kessy na Taslima. Wabunge wanne hawakuwapo.
Kwa
mujibu wa kanuni za Bunge hilo, kama wabunge watatu wa nchi moja,
wakitoka nje kupinga jambo lolote basi kikao kinaahirishwa kwa dakika 15
na wasiporejea bunge linaahirishwa.
Akizungumzia
mgogoro huo, Ofisa Habari wa EALA, Bobi Odiko alisema kilichotokea jana
si ukiukwaji wa taratibu na kuongeza kuwa ana imani mambo yatakuwa sawa
na vikao vitaendelea leo kwa amani.