wapinzani kusimamisha mgombea mmoja 2015
UPEPO wa mabadiliko ya kisiasa
unaovuma kuelekea kambi ya upinzani, sasa unaonekana kuwaamsha viongozi
wa vyama hivyo baada ya kutolewa kwa taarifa kuwa wanafikiria
kusimamisha mgombea mmoja wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
(HM)
Taarifa zilizolifikia gazeti hili
kabla ya kuthibitishwa na mmoja wa viongozi hao, zilieleza kuwa hatua ya
vyama hivyo imekuja baada ya ushirika wao waliouunda kupinga upungufu
uliokuwemo kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kuzaa matunda.
Pamoja na hilo, inaelezwa kuwa maamuzi
hayo magumu ya wapinzani yametiwa chachu na kauli aliyoitoa Rais Jakaya
Kikwete ya hivi karibuni ya kukitabiria anguko Chama Cha Mapinduzi
(CCM), katika uchaguzi wa mwaka 2015 au ule wa 2020, kutokana na kile
alichodai kuwa viongozi wa chama hicho kuendekeza rushwa.
Mmoja wa viongozi wanaounda ushirika
huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia
alithibitisha taarifa hizo huku akisisitiza kuwa nia ya kufanya hivyo ni
kuhakikisha wanaiondoa madarakani CCM mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Mbatia, walichokifanya
kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba si nguvu
ya soda na badala yake wataendeleza hadi kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Mbatia alisema kuwa uongozi wa vyama
vya upinzani unatarajia kuungana na kumsimamisha mgombea mmoja, ili
kuhakikisha wanaiondoa madarakani CCM.
Mbatia ambaye alikuwa akizungumza
katika mahojiano maalumu na RAI Jumatano, alisema hatua hiyo pamoja na
ushirika wao unalenga kudumisha amani na uzalendo kwa kuweka utaifa
mbele.
Alisema umoja wanaoendelea kuuonyesha
kwenye mchakato wa Katiba Mpya, ambao unalenga kuweka mbele maslahi ya
Taifa ili kuhakikisha inapatikana Katiba bora yenye kushirikisha
Watanzania wote, wataufanya pia kwenye chaguzi mbalimbali.
"Ili jambo lolote litokee lazima
kuwepo na chanzo, mwanzo wetu wa ushirikiano ulioanza Septemba mwaka huu
ndani ya ukumbi wa Bunge, tutauendeleza.
"Tupo kwenye maridhiano zaidi, hata
muungano wetu wa Tanzania bara na Zanzibar si wa kisheria, viongozi wetu
Nyerere na Mzee Karume walikaa na kuzungumza, hata sisi tunafanya
hivyo, tunatakiwa kuzungumza kwa maslahi ya nchi," alisisitiza Mbatia.
Alisema vyama vyao viliamua kuwa na ushirikiano wa pamoja kutokana na kubaini kwamba, bila umoja hakuna kitakachofanikiwa.
"Tumeshaanza kuzungumza kwa mapana juu ya ushirikiano wetu, ukweli ni kwamba kuna mwelekeo mzuri," alisema.
Alisema hatua ya vyama kujadili kwa
pamoja mchakato wa Katiba ni dalili njema za kuelekea kwenye mafanikio
na ndio maana wanaona ipo haja ya kuuendeleza ushirika huo hadi kwenye
chaguzi mbalimbali nchini.
"Tunapaswa kuvifanya vyama vyetu viwe vya maslahi mapana kwa taifa, ili visionekane vipo kwa ajili ya maslahi ya viongozi.
"Kwa kuwa tumeweka maslahi ya taifa
mbele kwenye suala la Katiba, tumeona tuwe na mfumo ambao utalisaidia
taifa, ndio maana hata tulipotoka Ikulu tumekubaliana kuwa Tanzania
kwanza vyama baadaye, naamini kwa nia njema hata ule ushirikiano wetu
utaendelea mbele zaidi kwa maslahi mapana ya taifa letu, tunategemea
hivyo... tuna mategemeo mazuri, lazima tufikirie chanya," alisema
Mbatia.
Kauli ya Mbatia imeungwa mkono na
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro ambaye ameeleza kuwa chama
chao hakina tatizo kwenye suala la kumsimamisha mgombea mmoja na wako
tayari kwa sababu ushirikiano ni suala la msingi na lenye maana.
"Kulingana na upepo wa kisiasa ulivyo
sasa, ni dhahiri tunahitaji kushirikiana ili kukiondoa chama tawala
madarakani, kwa sababu mahali tulipo sasa ni pagumu.
"Tunachosubiri sasa ili kukamilisha
muungano wetu ni tamko la pamoja kutoka kwa viongozi wa juu wa vyama
vyote, lakini naamini nia ya kusimamisha mgombea mmoja itakubalika bila
kupingwa," alisema Mtatiro.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara
ya Habari kutoka Chadema, John Mnyika, alisema ushirikiano kwa sasa
umejikita kwenye suala la kunusuru mchakato wa Katiba na kuwezesha nchi
kupata Katiba bora.
Alisema ushirikiano katika masuala
mengine ikiwamo pendekezo la kushirikiana katika uchaguzi,
litatafakariwa kwa kuzingatia mafanikio katika ushirikiano kwenye suala
la mchakato wa Katiba Mpya ambao tunaendelea nao kwa sasa.
"Huu ndio msimamo ambao naamini pia viongozi wote wanao.
"Kwa kuzingatia kauli zilizotolewa na
wenyeviti wote watatu Septemba 15 mwaka huu kwenye mkutano na waandishi
wa habari, wakati wa kutoa tamko la pamoja la ushirikiano," alisema.
Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya
siasa nchini, Dk. Benson Bana ameukosoa uamuzi huo kwa kudai kuwa
hawawezi kuungana kwa sababu hawana kiwango cha kuing'oa CCM madarakani.
Dk. Bana aliweka wazi kwamba, hadhani
kama vyama hivyo vitafaulu kuitoa CCM madarakani, kwa sababu havina
mtaji wa kutosha wa wanachama.
Alieleza kuwa vyama vyote vitatu
vinavyojiona vinaisumbua CCM, ambavyo ni CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi,
havijafanya utafiti wa kutosha kubaini mtaji wa wapiga kura walio nao.
Alisema Chadema ina nguvu ndogo Bara
hasa kwenye maeneo ya mijini, CUF ina nguvu Zanzibar na NCCR-Mageuzi
haina nguvu ya aina yoyote jambo linaloashiria udhaifu wa vyama hivyo,
ambapo alivitaka kujipa muda wa kujipanga kabla ya kufikiria kuing'oa
CCM.
Wenye mtazamo tofauti na huo wanasema
kuwa endapo hatua hiyo ya vyama vya upinzani itafanikiwa, ni wazi
itathibitisha kauli ya Mwenyekiti wa CCM kwamba chama hicho kijiandae
kung'oka mwaka 2015 au 2020.
Hata hivyo bado kuna shaka juu ya
maamuzi hayo ya vyama vya upinzani, kutokana na yale ambayo yamepata
kushuhudiwa katika chaguzi nyingine zilizotangulia hususani zile za viti
vya ubunge.
Imeshuhudiwa katika chaguzi kadhaa
vyama hivyo vikisigana kufikia maamuzi ya kuachiana maeneo ya
kusimamisha wagombea wenye nguvu.
Mwaka 2010 kwenye uchaguzi Mkuu, CUF
kilikitaka Chadema kutosimamisha mgombea kwenye Jimbo la Tunduru
kutokana chama chao kuwa na nguvu, hata hivyo wenzao walikataa.
Hali hiyo pia ilijitokeza kwenye Jimbo
la Kiteto, Chadema iliitaka CUF kutosimamisha mgombea jambo ambalo
halikutekelezwa. Chanzo: mtanzania
Posted by
Unknown
11:27 PM