World Vision Waacha Wosia Ulinzi Kwa Watoto.
Shirika
lisilo la Kiserikali la World vision Tanzania cluster ya Korogwe limeiomba
jamii kuendeleza juhudi za shirika hilo walizozifanya kwa miaka kumi na tano
katika tarafa ya Magoma wilayani Korogwe za kumlinda mtoto kwa kuhakikisha
anapata huduma na haki zake zote za msingi.
Ombi
hilo limetolewa jana na mratibu wa mradi
uliokuwa ukishughulikia maendeleo ya Magoma( Magoma ADP) George Banyenza katika hafla ya kutia saini
hati za makabidhiano iliyohudhuriwa na Watendaji wa World vision, watendaji wa
halmashauri ya wilaya Korogwe,Diwani wa kata ya Magoma,Maafisa tarafa na
Mtendaji wa kata hiyo, wenyeviti wa vijiji vya kata hiyo na wanufaika wa mradi
huo iliyolenga kukabidhi rasmi majengo ya ofisi yaliyokuwa yakitumiwa
na mradi huo kwa Serikali .
Banyenza
alieleza kuwa kwa muda wa miaka kumi na tano World Vision kwa ufadhili wa watu
wa ujerumani imekuwa ikiisaidia jamii ya tarafa ya Magoma kupitia watoto kupata
huduma za elimu,afya na maji sambamba na kupinga ukatili dhidi ya watoto na
kuhakikisha wanapata huduma zote za msingi.
“ADP
Magoma imefikia tamati sasa lakini kwa kipindi chote tumekuwa tukiisaidia jamii
kupitia watoto hivyo tunaomba jengo na
rasilimali zake tunazoacha ziwe chachu kwa jamii kuendeleza ulinzi na usalama wa mtoto wa
Magoma.” Alieleza Banyenza.
Katika
hatua nyingine Meneja miradi Mwandamizi wa World vision kanda ndogo ya Korogwe Sylvester Masanja,
alimuomba Mkurugenzi Mtendaji kuwa mlezi wa asasi ya jamii ya UKIMAMA iliyokuwa
ikilelewa na mradi huo sambamba na kuwapatia chumba kimoja katika jengo hilo
kwa ajili ya shughuli za asasi hiyo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Korogwe Lucas Mweri
aliyepokea hati za makabidhiano ya jengo na rasilimali zake aliahidi kutunza
rasilimali hizo na kuhakikisha zinatumika kwa matumizi yenye tija kwa jamii.
Magoma ADP imeikabidhi Serikali jengo lenye
thamani ya Tsh 68,480,000/- walilolijenga mwaka 2010 kwa ajili ya kutekeleza
miradi ya kusaidia watoto na jamii tarafa ya Magoma ambayo imefikia mwisho wa
utekelezwaji wake. Stori & picha na Fatna Mfalingundi-Afisa habari
Halmashauri ya Wilaya Korogwe