MATANGAZO YA WAGANGA WA JADI YAMKERA MKUU WA WILAYA YA TANGA
MATANGAZO ya waganga wa jadi wanaotibu ukimwi kwa dawa za asili,
yanawavunja moyo watafiti na wanasayansi wanaoendelea kutafuta tiba ya
ugonjwa huo.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego, wakati
wa uzinduzi wa kampeni ya kutokomeza maambukizi mapya ya virusi vya
ukimwi kutoka kwa mjamzito au anayenyonyesha kwenda kwa mtoto
uliofanyika viwanja vya Tangamano jijini hapa.
Alisema matangazo hayo yanawatia hofu wananchi na kuamini kuwa
serikali na wataalamu wa afya wameshindwa kutafuta tiba ya ugonjwa huo
huku yakichochea ngono.
“Tatizo hili limechangia kuongezeka kwa waathirika wengi wa ukimwi…
iwapo hatutachukua hatua za kudhibiti kwa haraka, kuna uwezekano wa
serikali kushindwa kuwahudumia waathirika wa ungonjwa huo,” alisema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita, alisema ni asilimia
21.9 ya wanaume ndio wanaohudhuria kliniki wakiongozana na wenza wao
kwa ajili ya kupima virusi vya ugonjwa huo hali inayoonyesha kuwa jamii
inahitaji msukumo katika hili.
“Natumia fursa hii kuwaomba waheshimiwa madiwani watusaidie
kuhamasisha wananchi wote kupima virusi vya ukimwi kwa hiari kwa kuwa
sasa hivi mtazamo ni afya chanya na kinga kwa sababu huduma za dawa za
kufubaza makali ya ugonjwa huo zinapatikana kwa urahisi kwenye vituo
vya afya,” alisema Dk. Mahita.
Chanzo;Tanznia Daima
Post a Comment