Dk Ngasongwa: CCM inababaika
Ni kutokana na viongozi wake kusema hadharani bila ya kutumia vikao vya chama
Dar es Salaam. Waziri wa zamani katika
Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa na katika Awamu ya Nne
ya Rais Jakaya Kikwete, Dk Juma Ngasongwa amesema kuwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kinababaika katika kutekeleza majukumu yake.
Vilevile, chama hicho kimekumbwa mgawanyiko kati ya watendaji wake na Serikali na kwamba taifa lina ombwe la uongozi.
Kutokana na hali hiyo, Dk Ngasongwa
ambaye pia ni kada wa CCM amemshauri Rais Kikwete kuwa mkali katika
kusimamia watendaji wake anaowateua ndani ya chama na Serikali yake na
kufuatilia na kupima utekelezaji wa yanayokubaliwa .
Alikuwa akizungumza katika mahojiano
maalumu na gazeti hili nyumbani kwake mkoani Morogoro anakoendesha
maisha yake kwa kilimo cha mpunga baada ya kustaafu.
Dk Ngasongwa alisema kuwa mgawanyiko
huo kati ya watendaji wa Serikali na CCM, umeondoa umoja siyo tu katika
vyombo hivyo, bali pia miongoni mwa wabunge wa chama hicho tawala.
Alisema kuwa hali hiyo inasababisha
kutokea mambo mengi ikiwamo matukio ya mawaziri kushinikizwa kujiuzulu
kama ilivyotokea hivi karibuni na kwamba kwa Serikali ya Awamu ya Nne hali hiyo imekuwa ikijirudia.
"Chama tawala kinababaika sana, tena
hata watendaji wa CCM, wanawasema vibaya mawaziri hadharani, wakati wote
ni wateuliwa wa Rais (Jakaya Kikwete) na ndiye mwenyekiti wetu wa CCM.
Hii inakigawa chama. CCM ina utaratibu wake, kwa nini wasiitwe
wakahojiwa ndani ya chama, badala ya kutajana hadharani:
"Sielewi kwa nini CCM inababaika.
Inachotakiwa ni kuwa na mshikamano kwa wabunge wake kukutana mara kwa
mara na kujenga msimamo. Hii ni kazi ya mawaziri na wabunge pia,"
alisema Dk Ngasongwa na kuongeza:
"...Tatizo uongozi haufanyi kazi
vizuri, ndani ya chama chetu kuna mgawanyiko mkubwa hata katika
Serikali, mfano Mwanasheria Mkuu (AG) anaposema baadhi ya mawaziri
hawamsikilizi, hii 'No' (hapana), lazima kanuni za uendeshaji wa
Serikali zifuatwe, hii ni muhimu."
Alisema hali hiyo inaonekana hata kwenye Baraza la Mawaziri na kwamba mgawanyiko pia upo ndani ya Bunge kwa wapinzani.
"Lakini kugawanyika kwa upinzani ni
afadhali kuliko CCM, kwani matokeo yake ni kupunguza imani ya watu kwa
Serikali yao na chama tawala," alisema.
Akinukuu maneno ya Baba wa Taifa,
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dk Ngasongwa alisema: "Nyerere
alisema, bila CCM madhubuti nchi itayumba na ndiyo yanayotokea sasa.
"Msingi wa yote yanayotokea ni
ubinafsi, ubepari...; turudi kwenye Ilani ya chama, tuzungumze, tufikie
mwafaka, siyo kutukanana hadharani. CCM itoe mwongozo siyo kugawa
wananchi."
Ngasongwa aliyeshika nyadhifa
mbalimbali za kisiasa katika CCM na Serikali ikiwamo ujumbe wa Kamati
Kuu (CC), ubunge wa Ulanga Magharibi, Waziri wa Maliasili na Utalii na
baadaye Waziri wa Mipango, Viwanda na Uwezeshaji, alifafanua kwamba kuna
ombwe la uongozi katika chama tawala, upinzani, Serikali hata bungeni.
"Kuna ombwe la uongozi siyo tu kwa
wapinzani, hata sisi chama tawala CCM, Serikali, hata bungeni pia kuna
mchanganyiko na yanaonekana waziwazi. Tunaona Spika anavyodharauliwa na
wabunge. Bunge linaonyesha picha ya hali halisi ya nchi yetu
ilivyo,"alisema Dk Ngasongwa.
Alipotakiwa kuzungumzia zaidi
tukio
la hivi karibuni la Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri
wanne walioshinikizwa kujiuzulu kutokana na Ripoti ya Kamati ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, alieleza
kuwa hajaisoma kwa undani ripoti hiyo, lakini inaonyesha kuwa
utekelezaji wake ulikuwa mbaya.
Hata hivyo, alisema kuwa kamati hiyo
ilitakiwa kuainisha makosa ya watendaji wa operesheni hiyo na kuwaacha
mawaziri wajipime na kujiuzulu wenyewe.
Alisema kwamba hatua ya wabunge na
kamati kushinikiza mawaziri hao wajiuzulu iliwachongea kwa Rais Kikwete
aliyeamua kuwafukuza kazi kwa lugha ya kistaarabu, hali ambayo alielezea
kuwa inaweza kujenga uhasama baina ya wabunge, kamati na mawaziri
walioondolewa.
Hivi karibuni Rais Kikwete alitengua
uteuzi wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamshi Vuai Nahodha, Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi pia Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya
Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo baada ya wizara zao kutajwa kushindwa
kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyopoteza maisha ya watu,
mifugo na vitendo vya ukatili kwa binadamu.
Kuhusu kubadilika kwa mawaziri, Dk
Ngasongwa alieleza kuwa jambo hilo siyo baya, lakini akasema kwamba
likifanyika mara kwa mara linadumaza wizara kwa kukosekana mwendelezo wa
utendaji.
"...Ikitokea mara kwa mara inadumaza
utendaji, hupati 'continuity' (mwendelezo mzuri), kwani mawaziri
huhitaji kujifunza na utekelezaji huhitaji muda. Continuity ni muhimu
kwa mawaziri, hata watendaji wengine," alisema.
Hii ni mara ya tatu kufanyika kwa
mabadiliko ya Baraza la Mawaziri tangu kuingia madarakani kwa Serikali
ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, likiwamo lililotokea baada ya
aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu. Chanzo: Mwananchi
Posted by
Unknown
11:47 PM