Lembeli: Serikali iondoe VAT vifaa vya mradi
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira, James Lembeli, ameishauri serikali kuondoa kodi kwenye
vifaa vya mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu unaoendeshwa na
Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), ili kumuwezesha mwananchi wa hali ya
chini kuondokana na makazi duni.
Lembeli alitoa kauli hiyo juzi baada ya taarifa ya mradi huo
iliyosomwa mbele ya kamati hiyo na Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa
shirika hilo, Benedict Kilimba na kueleza kuwa kodi za serikali
zimesababisha bei ya nyumba hizo kuwa kubwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mfumo wa kuwataka wanunue vifaa vya
ujenzi kwenye maduka maalumu umeongeza gharama ya ujenzi huo na
kufikia sh milioni 31.3 kwa nyumba yenye vyumba viwili na sh milioni
35.3 hadi milioni 36.2 kwa nyumba yenye vyumba vitatu bila Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT).
Kilimba alisema mbali na changamoto hizo, shirika pia linalazimika
kuilipa serikali sh milioni 7 hadi 10 kama VAT kutokana na
manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa kila nyumba, jambo lililosababisha
kuuzwa sh milioni 40.7 kwa nyumba ya vyumba viwili na sh milioni 46.3
hadi milioni 48.2 kwa vyumba vitatu.
Akizungumza baada ya taarifa hiyo, Lembeli alisema ni wajibu sasa kwa
serikali kuonyesha moyo wa dhati katika kuwawezesha wananchi kumudu
kubadilisha maisha yao ikiwemo la makazi bora ambayo ni haki ya kila
mtu.
Aliahidi kubeba jukumu la kuishauri serikali kuondoa VAT kwenye
vifaa vya ujenzi wa nyumba zinazojengwa na mradi wa shirika hilo, hasa
zile zilizolengwa kwa ajili ya makazi bora kwa watu wa hali ya chini.
Post a Comment