HUYU NDIYE MTOTO ALIPIGWA NA BABA YAKE MZAZI NA KULISHWA KINYESI CHA MTU MZIMA:
MWALIMU wa Shule ya Msingi Morotonga, wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara, Karata Mugunda, anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani hapa, kwa tuhuma za kumpiga na kumlisha kinyesi mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 10.
Mwenyekiti Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Wilaya ya Serengeti, Samwel Mewama, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtoto huyo alilishwa kinyesi alichokuwa amejisaidia ndani ya nyumba yao.
Kwa mujibu wa Mewana, tukio hilo la kusikitisha lilitokea Agosti 14, mwaka huu saa 12 alfajiri.
“Chanzo cha tukio hili la kikatili ni mtoto huyo kujisaidia haja kubwa ndani ya nyumba, baada ya kuogopa kutoka nje usiku wa manane.
“Baada ya kujisaidia, baba yake ambaye ni mwalimu, alikasirika na kuamua kumwadhibu kwa kumchapa fimbo sehemu za makalio na kumsababishia majeraha ya kutisha.
“Pamoja na kumwadhibu kwa fimbo, alimlazimisha ale kinyesi chote alichojisaidia kisha akamlazimisha anywe maji kwa wingi,” alisema Mewana.
Akizungumzia jinsi alivyopata taarifa za tukio hilo, alisema ofisi yake ilipigiwa simu na mwalimu mmoja anayefundisha shule moja na mtuhumiwa.
Baada ya taarifa hiyo, alifuatilia ili kujua ukweli wake ndipo alipomkuta mwanafunzi huyo akiwa amejeruhiwa vibaya makalio yake.
“Kwa kweli nilimkuta ana hali mbaya, kwa hiyo nilichokifanya nilimchukua na kumpeleka Kituo cha Polisi Mugumu nikapewa PF 3 kwa ajili ya matibabu hospitalini,” alisema.
Aliongeza kwamba, baada ya polisi kupata taarifa hiyo na kushuhudia majeraha aliyokuwa nayo mwanafunzi huyo kupitia dawati lao la kijinsia, walikwenda kumkamata mwalimu huyo ili hatua zaidi ziweze kufuata.
Daktari wa Zamu katika Hospitali ya Nyerere DDH, Dk. Ohoka Joseph, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo.
Alisema mtoto huyo alijeruhiwa vibaya kwenye makalio yake na kwamba ameathirika kisaikolojia.
“Huyo mtoto ameathirika kisaikolojia, kwa hiyo, kuna haja akafanyiwe uchunguzi kutokana na athari za kipigo na tukio alilofanyiwa.