Bunge la Marekani lafikia makubaliano
Serikali ya Marekani imefungua milango yake leo baada ya
bunge kupitisha sheria inayomaliza kufungwa shughuli za serikali na
kuepusha dakika za mwisho nchi hiyo kushindwa kulipa madeni yake.
Baraza la seneti lilipiga kura kuidhinisha hatua hiyo kwa kura 81 za ndio na 18 zilizokataa na kulipeleka suala hilo katika baraza la wawakilishi ambalo linadhibitiwa na chama cha Republican , ambalo nalo liliidhinisha hatua hiyo usiku wa jana Jumatano kwa kura 285 dhidi ya 144.
Spika wa baraza la wawakilishi kutoka chama cha Republican John Boehner
Mswada huo sasa unaifungua serikali hadi tarehe 15 mwezi Januari mwakani na unaruhusu wizara ya fedha kukopa hadi Februari 7 mwaka ujao ama huenda kwa muda wa mwezi mmoja zaidi.
Hatua hiyo haijumuishi chochote ambacho wabunge wa chama cha Republican walikidai wakitaka kufutwa ama kupunguzwa kwa mpango wa rais Obama wa kufanyia mageuzi mpango wake wa bima ya afya.
Rais Barack Obama
Marekani imekwisha wahi kuwa katika hali kama hiyo hapo kabla, ikisubiri kupata muafaka kuhusu suala la bajeti bila ya kuwa na matokeo ya uhakika. Lakini hii ilikuwa mara ya kwanza katika miaka 17 kwa serikali ya Marekani kufunga baadhi ya shughuli zake muhimu . Kiongozi wa wabunge wa chama cha Democratic katika baraza la wawakilishi Nancy Pelosi aliita hatua hiyo kuwa ni siku 16 za hatari ya kifahari ambayo imeugharimu uchumi wa Marekani karibu dola bilioni 24.
Spika wa baraza la seneti la Marekani Harry Reid wa chama cha Democratic amesema kuwa hiyo ni hatua muhimu kwa Marekani.
"Tumeona leo jinsi bunge lilivyofikia makubaliano ya kihistoria kwa vyama vyote, ili kuiwezesha serikali kufanya kazi zake tena na kuwezesha kulipa madeni yake."
Wafanyakazi wa serikali ya Marekani wakiandamana
Mkurugenzi mkuu wa shirika la fedha la kimataifa IMF Christine Lagarde ameyakaribisha makubaliano hayo lakini amesema uchumi wa Marekani unaoyumba yumba unahitaji uimara wa muda mrefu wa bajeti yake.
China na Japan ambazo kila moja inamiliki kiasi cha dola trilioni moja katika hazina ya Marekani, ziliitolea mwito nchi hiyo hapo kabla kufikia makubaliano haraka.