Mandela aendelea kupambana kitandani
Bi Makaziwe ameliambia Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini, SABC kuwa mpinzani huyo wa siasa za ubaguzi wa rangi, "bado yupo nasi, imara, na anatia moyo".
"Hata kwa kukosa neno zuri zaidi... Akiwa bado kitandani anatufundisha somo-somo la subira, upendo, uvumilivu," amesema, Makaziwe.
Bwana Mandela, mwenye umri wa miaka 95, anaendelea kupata huduma ya matibabu akiwa nyumbani kwake.
Aliruhusiwa kutoka hospitali mwezi Septemba mwaka huu baada ya kutibiwa kwa karibu miezi mitatu kufuatia maambukizi yanayojirudiarudia katika mapafu yake.
Bwana Mandela anaheshimika kwa kiasi kikubwa kutokana na namna alivyopambana dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na baada ya kuachiliwa huru kutoka gerezani mwaka 1990 aliwasamehe wazungu wa zamani waliomkamata na kumfunga.
Alifungwa miaka 27 jela na alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini mwaka 1994.
Bwana Mandela mara baada ya kumaliza kipindi kimoja cha miaka mitano ya urais, hakutaka kugombea tena nafasi hiyo.
Mwezi uliopita mke wa zamani wa Bwana Mandela Winnie Madikizela-Mandela alisema Bwana Mandela hakuweza kuzungumza kwa sababu ya mipira iliyoko kinywani ili kuvuta maji maji yaliyoko katika mapafu.
Ofisi ya rais wa Afrika Kusini mara kwa mara imekuwa ikielezea hali ya Bwana Mandela kuwa ni mahututi lakini imara.