Featured Post Today
print this page
Latest Post

ZAHANATI YA ITIMBO HAINA DAKTARI

Mwenye suti nyeusi ni Mzee Gwelino Chang'a maarufu kwa jina la Matekeleza na kushoto ni ofisa mtendaji wa kijiji cha Itimbo Kata ya Rungemba Wilaya ya Mufindi katika Mkoa wa Iringa Abson Mangula wakiwa nje ya zahanati iliyojengwa na Matekeleza kijijini Itimbo.



ZAHANATI ya kijiji cha Itimbo Kata ya Rungemba Wilaya ya Mufindi katika Mkoa wa Iringa inahitaji daktari kwa ajili ya kuwezesha utabibu kwa wagonjwa.

Akizungumza na mtandao huu ofisini kwake, nesi na muuguzi wa zahanati hiyo Olesta Mahanga amesema daktari anahitajika mapema kutokana na aliyekuwapo kuhamishwa bila kubadilishwa mwingine.

Amesema daktari ananafasi yake ndiyo maana anahitajika kwa haraka ili kuwezesha shughuli za utabibu kufanyika kwa wagonjwa mbalimbali wanaofika kupata matibabu.

“Umuhimu wa daktari upo kwa sababu ana nafasi yake. Daktari aliyekuwapo alihamishwa lakini hajabadilishwa mwingine hata wa kuja kuripoti tu. Hivyo, kwa kweli daktari anahitajika” amesema Mahanga.

Pamoja na uhitaji wa daktari Mahanga amewataka wananchi kuwa waelewa kwa kile wanachoelezwa kuhusiana na shughuli za afya kwa kuwa ni muhimu kwa ustawi wao na uwajibikaji mzuri wa watendaji wao.

Akifafanua zaidi amesema wananchi wamekuwa na kawaida kuwataka wahudumu kufanya kazi kwa muda wa masaa 24 bila kupeana zamu jambo ambalo linahatarisha uwajibikaji kutokuwa mzuri.

“Uelewa wa watu bado ni mdogo. Mtu anapofanya kazi anatakiwa kupumzika ili aifanye kazi vizuri lakini watu wetu hapa wakimuona muhudumu mmoja tu wanaanza maneno na tumekuwa na kawaida ya kupeana zamu ili kupata nafasi ya kupumzika.

“Wao wanataka muda wote hata usiku tuwe kazini bila kupeana zamu. Kiafya siyo vizuri kufanya kazi bila kupumzika na kibaya zaidi ukiwaeleza hali inavyokuwa wanaanza lawama na wengine kutukana bila kujua ni nini wanakifanya. Tuwaombe tu kuwa na uelewa pale tunapowapa maelekezo wajue” amesema.


Ofisa mtendaji wa kijiji hicho Abson Mangula alipotakiwa kutoa maelezo juu ya utendaji kazi wa wahudumu wa zahanati hiyo amesema licha ya kuwa wawili tu, wamekuwa na utaratibu mzuri wa kutoa huduma kwa kuhakikisha muda wote anakuwepo muhudumu.

Amekiri kuwepo na maneno ya watu juu ya wahudumu hao kuwataka watoe huduma kwa muda wa masaa 24 bila kupumzika na kusema kuwa hata wao ni binadamu ambao wanahitaji kupumzika kama wao wanavyolala majumbani kwao na hivyo kuwataka wasiingilie mipango yao na kupokea huduma kwa mhudumu ye yote watakayemkuta wakati wakihitaji huduma.

Alipoulizwa juu ya upatikanaji wa dawa, Mahanga alisema dawa zipo za kutosha lakini tatizo lililokubwa ni kufanya kazi katika giza nyakati za usiku.

“Tatizo lililokubwa ni nishati kwa sababu nyakati za usiku anaweza kuja mgonjwa hasa akina mama wanapokuja kujifungua lakini wanaweza wasije na taa na hapa hatuna taa za kutosha. Tungetamani kama tungepata hata kasola ili tuweze kufanya kazi kwa urahisi.

“Tatizo lingine ni maji japo kuwa sasa kisima kinachimbwa tunategemea kikiisha tunaweza tukajikomboa suala la maji” amesema.

Wakati huo huo mkulima maarufu wa miti katika Wilaya hiyo Gwelino Chang’a maarufu kwa jina la Matekeleza ameahidi kusimamia suala la uchimbaji kisima cha maji katika zahanati hiyo ili kurahisisha wagonjwa na wahudumu kupata maji kwa urahisi.

Ofisa mtendaji wa kijiji hicho Mangula amesema endapo Matekeleza atasimamia kama alivyokusudia, utakuwa ni mwendelezo wa utekelezaji wake kwa kuwa hata zahanati hiyo alijenga mwenyewe kwa kusaidiana na nguvu ya wananchi.


“Alipewa jina la “Matekeleza” kwa kuwa ni mtu wa utendaji siyo ahadi. Zahanati hiyo pamoja na ofisi ya kijiji alijenga mwenyewe kwa hiyo tunaimani kuwa atafanya wala hatuna wasiwasi naye juu ya ahadi hiyo. Kila wakati yeye mwenye huwa ni mtu wa utekelezaji ndiyo maana tulimpa jina hilo” amesema Mangula.


Chanzo: www.gustavchahe.blogspot.com
0 comments
 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger