SUMATRA TANGA YATOA ONYO KALI KWA WAMILIKI WA VYOMBO VYA USAFIRI MAJINI
MAMLAKA ya Udhibiti na Usimamizi wa Usafiri wa nchi kavu na Majini (Sumatra)Mkoani Tanga umewapa muda wa wiki mbili wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini mkoani hapa kuhakikisha vyombo hivyo vinakaguliwa na kuwa salama kabla ya kuanza kazi zao ili kuweza kupunguza ajali zisizo za lazima.
Wito huo ulitolewa na Afisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Tanga,
Walukani Luhamba wakati akizungumza na Mtandao huu ambapo alisema kuwa kwa atakayekaidi agizo hilo atachukulia hatua kali ikiwemo kufutiwa leseni.
Alisema dhamira yao kubwa ya kuhakikisha vyombo hivyo vinakaguliwa ni kupambana na wimbi la ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya wananchi ambao hawana hatia kutokana na uchakavu wa baadhi ya vyombo hivyo.
Sambamba na hilo,Afisa huyo alisema kuwa watafanya ukaguzi wa vyombo vidogo vidogo na vikubwa vinavyotoa huduma za usafiri ndani na nje ya mkoa wa Tanga kwa kuvitaka vijisalimishe vyenyewe kabla ya hatua kali hazijachukuliwa dhidi yao.
Hata hivyo alisema kuwa halmashauri mbalimbali mkoani hapa kwa
kushirikiana na wakurugenzi wao hawana budi kuweka utaratibu wa kubandika viwango vya nauli kwenye mabango yaliyopo kwenye stendi za mabasi ili kuweza kuwapunguzia usumbufu wasafiri wao.
“Hii nadhani ndio njia sahihi ya kuepusha ulanguzi kwa abiria kwa sababu wapo baadhi ya vyombo vya usafiri vyenye kutaka kutoza viwango vikubwa vya nauli kuliko viwango vilivyowekwa na mamlaka husika“Alisema Luhamba.
Akizungumzia suala la baadhi ya mabasi yanayofanya safari zake mkoani hapa kushindwa kutoa tiketi kwa wasafiri, Afisa huyo alisema kuwa kutokutoa tiketi ni kosa hivyo kwa atakayebainika atatozwa faini ya kuanzia shilingi laki moja.
Post a Comment