Featured Post Today
print this page
Latest Post

Ashindwa Kwenda Shule Kwa Kukosa Ada

Ashindwa Kwenda Shule Kwa Kukosa Ada

Mwenjuma M. Magalu (kulia) akiwa na Bibi yake nyumbani kwao Kijiji cha Msasa, wilayani Handeni

 Mwanafunzi Mwenjuma M. Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Komnyang’anyo wilayani Handeni akimuonesha mwandishi fomu ya kuitwa shuleni

Na Joachim Mushi, Handeni

LICHA ya Serikali kuliarifu Bunge la Tanzania kuwa wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba mwaka 2011 kutoka mikoa 12 tayari wamejiunga na kidato cha kwanza, imebainika bado kuna wanafunzi wameshindwa kujiunga na shule kutokana na kipato duni cha familia zao.

Mwenjuma M. Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Komnyang’anyo wilayani Handeni ni miongoni mwa wanafunzi walioshindwa kujiunga na sekondari kutokana na mama yake kushindwa kumgharamia mahitaji ya shule.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni kijijini Msasa, wilayani Handeni, katika utafiti uliofanyika kwa ushirikiano na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), mama wa mtoto huyo Hadija Magalu aliyetelekezwa na mumewe kwa muda mrefu alisema ameshindwa kumsomesha mwanaye kutokana na kipato duni alichonacho.

Magalu alisema alipata taarifa za kufaulu kwa mwanae tangu Desemba 12, 2011 na kuanza kujikusanya taratibu lakini hadi muda wa kwenda shule ulipofika (Januari 9, 2012) alikuwa hajakamilisha baadhi ya vifaa vinavyohitajika shuleni vikiwemo fedha ya ada na michango mingine.

“Naweza kukuonesha hata baadhi ya vitu ambayo nilikuwa tayari nimenunua kama sare, kwanja na mahitaji mengine madogo madogo…aliyenikwamisha na kunivunja moyo ni babayake (baba wa mtoto), ambaye awali niliwasiliana naye kupitia kwa ndugu zake na kuahidi angenisaidia ada lakini hakufanya hivyo hadi muda wa kwenda shule ulipofika,” alisema Magalu.

Mume wa Magalu (jina tunalo) ametelekeza familia yake (watoto wanne) pamoja na mkewe kwa zaidi ya miaka minne sasa kwa kisingizio kwamba amekwenda nje ya Wilaya ya Handeni kutafuta maisha, huku mkewe akibaki akiangaikia familia hiyo.

“Tumekuwa tukisikia tu kwamba ameonekana kijiji fulani lakini ukifuatilia humpati, na mara nyingi anapowasiliana na ndugu zake ndio wanatupa taarifa zake…nami niliwasiliana naye mara ya mwisho nikimpata taarifa za mtoto kufaulu lakini hakutekeleza ahadi yoyote juu ya kunisaidia ada ya mtoto.

Michango iliyomkwamisha mwanafunzi Mwenjuma Magalu kujiunga na kidato cha kwanza ni ada ya sh. 20,000, fedha ya taaluma sh. 10,000, fedha ya madawati 15,000, fedha ya sweta sh.10,000, kitambulisho sh. 5,000, ulinzi sh. 5,000, tahadhari 5,000 pamoja na fedha kwa ajili ya nembo ya shule sh. 2,000.

Akihutubia Mkutano wa Saba wa Bunge la Tanzania lililomalizika hivi karibuni, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kutoka mikoa 12 ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mara, Morogoro, Mwanza, Lindi, Kilimanjaro, Pwani, Ruvuma  na  Tanga, wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba wamefanikiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Hata hivyo mwanafunzi Magalu kwa sasa anafanya vibarua kwa moja ya kampuni za Kichina zinazofanya ujenzi wa barabara inayopita Kijiji cha Msasa, kwa madai anatafuta fedha za ada na endapo akikamilisha atahakikisha anaendelea na elimu ya sekondari hapo baadae.

Mwandishi wa habari hizi alipojaribu kuzungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni, Hassan Mwachibuzi alisema ofisi yake haina taarifa za mtoto huyo kushindwa kujiunga na shule, hivyo kumshauri mwandishi amueleze mtoto huyo kufika ofisi za halmashauri ili aweze kujieleza na ikiwezekana kusaidiwa.

“Kama huyo mtoto yupo mwelekeze aje pale ofisini kuna wataalamu wa utambuzi watamuhoji na kuangalia namna ya kumsaidia…sisi hatuna taarifa hizo na huenda wahusika wanatuficha,” alisema kiongozi huyo.
0 comments

Waziri Muhongo azindua hafla ya udhibiti wa vihatarishi katika usimamizi wa fedha

Waziri Muhongo azindua hafla ya udhibiti wa vihatarishi katika usimamizi wa fedha

Mkurugenzi Mtendaji wa Banki ya Barclay's Tanzania Kihara Maina akitoa hotuba ya kumkaribisha  Mgeni Rasmi Waziri wa Wizara ya Fedha na Uchumi  Dkt. William Mgimwa katika hafla ya uzinduzi wa udhibiti wa vihatarishi katika  usimamizi wa fedha (Risk Management Solutions).Uzinduzi huo uliyofanyika leo kwenye hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi Waziri wa Wizara ya Fedha na Uchumi Dkt. William Mgimwa akiongea na viongozi, wawezeshaji na wateja wa  Benki ya Barclays Tanzania  wakati wa  hafla ya uzinduzi wa udhibiti wa vihatarishi katika  usimamizi wa fedha (Risk Management Solutions)  iliyofanyika leo kwenye  hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam
Mjumbe wa bodi ya benki ya Barclays Tanzania Fatma Karume (kulia) akisisitiza na kufurahia jambo alipokuwa anaongea na Mgeni Rasmi (hayupo kwenye picha) wakati wa hafla ya uzinduzi wa udhibiti wa vihatarishi katika usimamizi wa fedha (Risk Management Solutions) iliyofanyika leo kwenye hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam. Kushoto ni mjumbe wa bodi ya benki hiyo Suleiman Mohamed.
Baadhi ya washiriki wa semina ya udhibiti wa vihatarishi katika usimamizi wa fedha (Risk Management Solutions) wa Benki ya Barclays wakihudhuria  hafla ya uzinduzi huo uliofanyika leo kwenye  hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Eleuteri Mangi-Maelezo)
0 comments

WANACHAMA AFRICAN SPORTS JITOKEZENI KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI-SHEWALLY

WANACHAMA AFRICAN SPORTS JITOKEZENI KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI-SHEWALLY


Na Oscar Assenga,Tanga.
WAPENZI wa Klabu ya African Sports na wanachama wa zamani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu ya kuomba uanachama ili waweze kupata fuksa ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wao utakaofanyika hivi karibuni.
Akizungumza jioni hii na Tanga Raha,Mwenyekiti wa Klabu ya African Sports “Wanakimanumanu”Asseli Shewally alisema mchakato wa kujaza fomu za uanachama wa klabu hiyo tayari umeshaanza na fomu hizo zinapatikana makao makuu ya klabu hiyo barabara kumi na mbili jijini Tanga.
Shewally alisema lengo la kusajili wanachama upya ni katika kupitisha katiba mpya ili hatimaye kuweza kufanya uchaguzi mkuu wa viongozi wapya watakaoingoza timu hiyo.
Aidha aliwataka wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi ili kuweza kuchukua fomu na kurudisha kwa wakati ili kuweza kupata viongozi watakaoiletea maendeleo timu hiyo.
0 comments

"NINA WAKE FEKI WENGI SANA HAPA MJINI".....MZEE MAJUTO


"NINA WAKE FEKI WENGI SANA HAPA MJINI".....MZEE MAJUTO

Majuto anasema kuwa ana watoto tisa ingawa hakuwa tayari kuwazungumzia mama wa watoto hao zaidi ya kumwongelea mkewe wa sasa, Aisha Mbwana kwa kuwa wake zake aliozaa nao baadhi ya watoto kwa bahati mbaya walishafariki dunia.
Alisema kuwa yanapokuja masuala ya familia huwa anapenda azungumze mkewe na kwa ridhaa yake. Kwa mujibu wa Majuto anapenda aitwe mke halali kwa kuwa wake feki anao wengi kupitia michezo ya kuigiza na wengine wenye fikira potofu hutumia picha hizo kutengeneza habari za uongo.
Aisha anaizungumziaje familia yake
Kama kawaida ya wanawake wa Tanga ana lafudhi ya huko ambayo huvutia kuzungumza nao, anaanza kwa kunieleza kuwa alianza kuitwa mke halali wa nguli huyo wa sanaa za maigizo mwaka 1997, walipofunga ndoa .
Anasema kuwa alikutana na nguli huyo maeneo ya Buguruni, Dar es Salaam, ambako alikuwa akiishi na dada yake aliyekuwa kaolewa na rafiki yake mzee Majuto, ‘Mwanachia’ (kwa sasa ni marehemu), ambaye walikuwa wakiigiza pamoja.
Anasema hakuwa na hili wala lile hadi alipoamua kuondoka na kurudi kwao maeneo ya Vingunguti, ambako ndiko walikokuwa wanaishi wazazi wake na kupewa taarifa kuwa posa imepelekwa kwa ajili yake.
“Nilipoambiwa kuhusu hiyo posa sikufikiria kama atakuwa ni mzee Majuto kwa kuwa alikuwa ni kama shemeji yangu kutokana na kuwa karibu na shemeji yangu,” anasema Aisha ambaye ni mama wa watoto watatu.
Anaendelea kueleza kuwa siku ambayo wanafamilia walikutana na kumuuliza kama anamfahamu mchumba na kutajiwa jina kuwa ni Amri Athumani, aliuliza mara mbili kwa kuwa alikuwa hamfahamu huyo mtu hadi alipoambiwa kuwa ni King Majuto.
“Kwa mila za Wabondei mchumba wa kwanza anakubaliana na wazazi, halafu binti anapewa taarifa na kwa kuwa wazazi ni wakubwa inabidi binti akubali, na ndivyo ilivyokuwa kwangu nikakubali na kuolewa na Majuto,” anasema mama huyo.
Anaingia kwenye uigizaji kufuata nyayo za mumewe
Aisha anafafanuwa kuwa kabla ya kuolewa na Majuto hakuwa mwigizaji lakini baada ya kuolewa, mumewe huyo alimwingiza kwenye uigizaji na filamu ya kwanza kuigiza na mumewe huyo ni ‘Fukara hatabiriki’.
Mkewe huyo anasema kipindi hicho Majuto alikuwa anafanya kazi bila kuwa na kikundi zaidi ya wanafamilia, hivyo na yeye alikuwa mmoja wao akicheza kama mama na Majuto kama baba.
0 comments

HIVI NDIVYO VYAMA VYA UPINZANI VILIVYONGURUMA JANA..MSWADA WA KATIBA WAPIGWA VIKALI

HIVI NDIVYO VYAMA VYA UPINZANI VILIVYONGURUMA JANA..MSWADA WA KATIBA WAPIGWA VIKALI


Vyama vya upinzani jana vilifanya mkutano mkubwa kuwashawishi wananchi kupinga kile walichokiita kuhujumiwa kwa mchakato wa Katiba Mpya, wakitangaza Oktoba 10 kuwa siku ya Watanzania wote kushiriki katika maandamano kushinikiza wapewe haki ya kuandaa Katiba yao.

Wakizungumza kwa kupokezana katika Viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam jana, wenyeviti wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF, walieleza kuwa wataendelea kushirikisha taasisi za kiraia kupinga hujuma dhidi ya mchakato wa Katiba Mpya na kwamba hawatakubali endapo Rais Jakaya Kikwete atasaini Muswada wa Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.

Akizungmza katika mkutano huo Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema chama chake hakitakubali endapo Rais Kikwete atasaini muswada huo kwa kuwa una lengo la kupata Katiba Mpya isiyokuwa na tija kwa taifa. Alisema kuwa Katiba inayoandaliwa ni kwa ajili ya Watanzania wote na siyo kundi la watu, hasa CCM na kwamba mchakato wa kuwapata wajumbe 166 wa Bunge la Katiba kutoka makundi mbalimbali siyo sahihi.

“Haiwezekani kila taasisi ikateuwa wajumbe tisa ambao majina yao yatakwenda kuchakachuliwa na usalama wa taifa, kisha kupata majina ya watu wanaowataka wao, kitu hiki kama CUF hatutakubali,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Hatutarudi nyuma na kukubali kuendelea na mchakato huu endapo Rais atasaini muswada huu. Tutaendeleza harakati za kupinga kwani bila hivyo tutapata Katiba Mpya isiyokuwa na tija.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuwa ni wakati wa kukaa meza moja ya mazungumzo kuondoa tofauti zilizopo ili kulinusuru taifa kuingia katika machafuko.

Alisema kama taifa, linatakiwa kujifunza kutoka mataifa mengine yalivyotokea maafa katika michakato ya kuandikwa kwa Katiba Mpya.

“Ni wakati wa kukaa meza moja, kwa kushirikisha wadau mbalimbali kwani Katiba inayotafutwa ni ya Watanzania wote na siyo ya CCM,” alisema Mbatia na kuongeza:

“Lazima tupate Katiba Mpya kwa gharama yoyote ile, iwe ndani au nje ya Bunge ili kuhakikisha tunapata Katiba ya Watanzania wote.”

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alisema kosa kubwa katika kudai haki ni woga na hatutapata Katiba Mpya kama tutaendelea kuwa taifa la watu wenye hofu. Tunataka kukutana na makundi mbalimbali katika jamii ambayo ni viongozi wa dini, wasomi na watu wa makundi mengine kuwaeleza kinachoendelea sasa hivi.

Hata migogoro ya kiimani baina ya Wakristo iliyotokea nchini imesababishwa na katiba iliyopo sasa, kama Rais atasaini wao hawatashiriki Bunge la Katiba na watatumia kila mbinu iliyopo duniani kuueleza umma nini kimetokea na hawataendelea kunyenyekea vitisho vya Jeshi la Polisi.

Tunalaani mchakato wa katiba kuhodhiwa na chama kimoja na tunatangaza Oktoba 10, mwaka huu kuwa ni siku maalumu ya kudai katiba na sasa hawataenda tena Ikulu kwani inaaminika huko ni kwenda kunywa chai na watatangaza maandamano nchi nzima.


Tumemwambia IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema) kuwa hatutaomba ruhusa bali tutampa taarifa.Tunaomba walio makanisani na misikitini kutafuta katiba mpya na jambo la mwisho Jumatato tutaenda kufanya mkutano kama huo Zanzibar,” alisema Mbowe.

Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema chama chake kinapinga namna mchakato wa Katiba ulivyoendeshwa kwasababu kilichopelekwa bungeni kilikuwa Muswada wa Katiba Mpya, lakini kilichopo mitaani ni Mchakato wa Rasimu ya Katiba Mpya.

“Tunawaambia CCM hawatengenezi Katiba Mpya, wanachofanya ni danganya toto kwa kuwa wanatakiwa kuirudisha Katiba ile ile ya awali.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe aliyefika katika viwanja hivyo alisema kuwa Rais Kikwete akisaini muswada huo, Watanzania watajua kuwa hana nia njema na taifa kwa kuwa wengi wanaipinga.

“Mimi natega masikio kusikia kama utasaini au la ili kujua kama unawatega na kuwahadaa Watanzania. Tunakuomba usikubali mtego huo,” alisema Kakobe akimwambia Rais Kikwete.

Alisema tangu awali CCM ilikuwa ikipinga kuandaliwa kwa Katiba Mpya, ingawa Rais Jakaya Kiwete alijitosa na kukubali mchakato huo kuanza nchini.

“CCM ilikataa katakata Katiba isianzishwe. Jakaya Kikwete pekee yake alijipiga kifua akakubali ingawa alishambuliwa kuwa amefanya makosa,” alisema Kakobe.

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kukuu cha Dar es Salaam(Udsm), Dk Azaveli Lwaitama alisema kuwa duniani kote shinikizo la kuundwa kwa Katiba Mpya hutoka nje ya Bunge na Serikali iliyopo madarakani.

“Tangu mwaka 1992 vyama vya upinzani vilikuwa vikitaka Katiba Mpya... Katiba Mpya huzaliwa na wanamapinduzi waliopo nje ya Bunge,” alisema Dk Lwaitama.

Akizungumzia ushirikiano wa vyama kumzuia Rais asisaini Sheria ya Rasimu ya Katiba, alisema: “ Ukifanya jeuri kwa sababu upo madarakani, watu uliodhani wamegombana watashirikiana.”

Mbunge wa Ubungo John Mnyika, alisema Mahakama ya wananchi ndiyo itakayotoa uamuzi wa mwisho.

“Ninyi ndiyo Mahakama yenye uamuzi wa mwisho, tunasubiri mwongozo wenu, mtakachosema tutafanya,” alisema Mnyika.

Kabla kuwasili kwa viongozi wakuu wa vyama hivyo vya siasa kwenye Viwanja vya Jangwani, jana wafuasi wao walikuwa kwenye makundi wakichambua baadhi ya mambo yaliyoonekana kuleta utata kwenye mchakato wa Katiba Mpya.

Rangi za bluu, nyekundu na nyeupe zinazotumiwa na vyama vilivyoshiriki kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini Muswada wa Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba Mpya zilionekana kuzagaa katika viwanja hivyo.

Magari ya Polisi yalionekana kuzunguka maeneo ya viwanja hivyo kuhakikisha ulinzi unaimarika wakati wote wa mkutano.

Nao wafuasi wa vyama hivyo waliokuwa wamevaa suti nyeusi, miwani na mashati meupe waliimarisha ulinzi katika eneo la mkutano, wengine wakiingia Viwanja vya Jangwani kutoka eneo la Barabara ya Morogoro, huku wakibeba mabango, bendera za vyama hivyo na picha za viongozi wao wakiimba nyimbo mbalimbali.

Wengi wa wafuasi hao walifika uwanjani hapo kwa kuletwa na mabasi madogo aina ya Coaster na wengine wakija kwa makundi kutokana Jeshi la Polisi kuzuia kufanyika kwa maandamano.
0 comments

KINANA,NAPE WAZURU KABURI LA BABA WA TAIFA HAYATI JULIUS NYERERE

KINANA,NAPE WAZURU KABURI LA BABA WA TAIFA HAYATI JULIUS NYERERE

721_e8e65.jpg

Katibu Mkuu wa CChama Cha Mapinduzi CCM Ndugu Abdulrahman Kinana katikati akiweka shada la maua kwenye kaburi la Hayati. Mwalimu Julius K. Nyerere huku Nape Nnauye Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi akishuhudia tukio hilo.

IMG_7745_ab5c6.jpg

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Ndugu Abdulrahman Kinana katikati akiwa katika picha ya pamoja na Andrew Nyerere Mtoto wa Kwanza wa Baba wa taifa Mwalimu Julius K. Nyerere wakati alipozuru kaburi la Mwaasisi huyo wa taifa la Tanzania Mwitongo, Butiama Nyumbani kwa mwalimu Mkoani Mara jana, Kinana alifanyakazi na Andrew Nyerere wakati wakilitumikia Jeshi la Ulinzi la wananchi la Tanzania (JWTZ), Katibu Mkuu huyo jana aliendelea na ziara yake katika wilaya ya Butiama katika kuimarisha chama na kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, Kinana ataendelea na ziara yake katika Wilaya ya Serengeti leo. Kushoto ni Nape Nnayue Katibu wa (NEC) Itikadi Siasa na Uenezi.PICHA NA KIKOSI KAZI CHA FULLSHANGWE-BUTIAMA MARA


IMG_7746_457c1.jpg

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akiagana na Andrew Nyerere mara baada ya kuzuru Kaburi la Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere Mwitongo Butiama jana

430_0a75e.jpg

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Ndugu Abdulrahman Kinana wa tatu kutoka kulia akiongozwa na ndgu wa Mwalimu Mzee Jack Nyamwaga wakati akielekea kuweka shada la maua katika kaburi la Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere jana mjini Butiama, Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mama Mabula

1015_e5c12.jpg

Wana habari nao wakishiriki kuweka mashada ya maua katika Kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere jana kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Fullshangwe Bw. John Bukuku, Said Mwishehe kutoka Jambo Leo Oktavian kutoka CCM Gerson Msigwa wa TBC, Ufo Saro wa ITV na Prosper Dereva wa CCM.

0 comments

Familia ya Nditi yazidi kutesa England

Familia ya Nditi yazidi kutesa England

nditi1 7e101

FAMILIA ya kiungo wa zamani wa Kikwajuni na timu ya taifa ya Zanzibar, Eric Nditi inaendelea kutesa katika soka la Ulaya baada ya watoto watatu wengine wa staa huyo kuibukia katika timu ya vijana ya Reading iliyo Ligi Daraja la Kwanza, England. (HM)


Wakati kaka yao, Adam Nditi akiwa ameingia kikosi cha kwanza cha Chelsea, mdogo wake anayemfuatia, Roberto Nditi (13) yuko katika kikosi cha timu ya Reading chini ya miaka 14, na mapacha wawili (pichani) wanaofuatia, Zion na Paolo (8) wako katika kikosi cha Reading chini ya miaka 10.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Basingstoke, Uingereza, Nditi alisema kwamba watoto wake mapacha walitakiwa na Chelsea lakini akashindwa kuwapeleka kwa sababu ya kushindwa kugawanya muda.
"Hawa Zion na Paolo walichukuliwa na Reading ingawa Chelsea iliwataka kwa sababu ningeshindwa kumudu kumpeleka kaka yao Reading kisha niwe nawapeleka wao London. Ndio maana nikaamua wote wakulie Reading," alisema Nditi. Chanzo: mwanaspoti
0 comments
 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger