|
KAPOMBE AKIWA AS CANNES NA GALLAS |
Baada ya
chenga za hapa na pale, kila kitu sasa kimewekwa hadharani kwamba beki wa
zamani wa Simba, Shomari Kapombe, ametaka mkataba wake na AS Cannes ya Ufaransa
uvunjwe na imeelezwa anataka kubaki nchini na kujiunga na Yanga.
Habari za
uhakika kutoka ndani ya AS Cannes nchini Ufaransa na kuthibitishwa na wakala
wake anayeishi nchini Uholanzi, zimeeleza Kapombe amefanya mazungumzo na Yanga
ambao wamemshawishi kubaki nchini.
Mmoja wa
viongozi wa AS Cannes ameliambia Championi Jumatatu kwamba: “Shomari amesusa
kuja na anataka mkataba wake uvunjwe, lakini bado hatujaelewa hasa tatizo ni
nini, ila tunajua amefanya mazungumzo na timu ambayo ni mabingwa wa Tanzania
(Yanga), kitu ambacho si sahihi.
“Amesema
anataka kubaki Tanzania, kidogo inatushangaza kwa kuwa kesi yake moja kuhusiana
na kutaka kulipwa fedha imefika Fifa, lakini ajabu kabisa hatukuwahi kukataa
kumlipa, badala yake tulisimamisha malipo kutokana na kuchelewa kwake. Huo
ndiyo ukweli, ila sipendi jina langu liandikwe gazetini.”
Blogu hii ilikuwa ya kwanza kuandika kuwa Kapombe amekwama nchini na yuko mkoani
Morogoro licha ya kuripotiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba
alishaondoka kwenda Ufaransa.
Juhudi za
kumpata wakala wake, Dennis Kadito akiwa nchini Uholanzi anakoishi zilizaa
matunda jana na akasema ana taarifa za Yanga pamoja na Azam FC kufanya naye
mazungumzo.
“Kweli kuna
hizo taarifa, si nzuri kwa kuwa ni kukiuka utaratibu. Tayari Kapombe amesema
anataka mkataba uvunjwe, kama umesikia hivyo ni sahihi. Nawashauri Yanga au
Azam kama wanamtaka waje nizungumze nao tukae na AS Cannes, basi tumalizane.
“Mkataba
wake ni wa miaka miwili, hivyo wasitumie njia ya mkato kwa kuwa mambo yako wazi
na mimi au AS Cannes hakuna mwenye shida,” alisema.
Kapombe
alitokea Simba na kujiunga AS Cannes bure, Simba ikitegemea kupata fedha kama
atauzwa katika timu nyingine za Ulaya, lakini mgogoro ulianza baada ya
kutolipwa mshahara wake kutokana na kutokuwa na akaunti ya benki za kule
Ufaransa lakini baadaye alilipwa baada ya kumaliza utata huo.
“Kweli kuna
fedha anadai, utaona katika miezi minne aliyokuwa Ufaransa hajalipwa mwezi
mmoja. Hii inatokana na ile ishu ya kuchelewa alipokuwa katika timu ya taifa.
Halafu, awali alichelewa kulipwa kutokana na suala kutokuwa na kibali cha kazi
kilichochelewesha ashindwe kufungua akaunti ya benki.
“Ila AS
Cannes ambao walikasirishwa na Kapombe kuchelewa Tanzania walitaka TFF ndiyo
wamlipe mshahara kwa kuwa ndiyo walimchelewesha, sasa kesi yake iko Fifa.
Ninaamini atashinda na mimi niko upande wake maana ndiyo wakala wake.
“Lakini
bado nasisitiza kuwa lazima Yanga wafuate utaratibu maana taarifa za kuzungumza
naye ninazo na ni za uhakika,” alisema wakala wake huyo.
Kiongozi wa
AS Cannes alisema wametumia mamilioni ya fedha kumtibu Kapombe, lakini
wanashangazwa na mambo yanavyokwenda.
“Suala lake
tutalishughulikia baadaye, tulikuwa na mechi muhimu na ngumu za FA. Tumeitoa St
Etienne inayoshiriki ligi kuu, sasa tutarudi kushughulikia suala lake ingawa
tunaweza kulifanyia kazi zaidi baada ya Fifa kutoa hukumu.”
Yanga
wamekuwa wakikataa katakata kulizungumia suala la Kapombe kwa hofu ya kuingia
kwenye adhabu ya kuzungumza na mchezaji mwenye mkataba.
“Najua sasa
Yanga hawawezi kukubali, ila wanawasiliana naye na walishakaa wakamalizana kwa
mazungumzo ya awali na sasa kuna mambo kadhaa wanamsaidia,” alisema rafiki yake
aliyetoa siri kwa mara ya kwanza kuwa yuko Morogoro.
Taarifa
zinaeleza Yanga wamelenga kumjumlisha kwenye dirisha la Caf kama watasonga
mbele au mwanzoni mwa msimu mpya, mara tu baada ya dirisha kufunguliwa.
Kabla
ya kuondoka nchini na kujiunga na AS Cannes inayoshiriki Ligi Daraja la
Kwanza nchini Ufaransa, Kapombe alikuwa nahodha msaidizi wa Simba.
Posted by
Unknown
5:32 AM