skip to main |
skip to sidebar
MADIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliofukuzwa katika Manispaa ya
Bukoba, wamesema wako tayari kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kama chama chao kitaendelea na msimamo wa kuwafukuza.
Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, mmoja wa madiwani hao
ambaye alikataa kutaja jina na kata yake, alisema wako tayari kuhamia
Chadema muda wowote kama hawatarudishiwa uanachama wao.
Alisema, madiwani wote waliofukuzwa wana msimamo mmoja ambapo wanasubiri vikao vya Kamati Kuu ya CCM ili wajue hatima yao.
Kwa
mujibu wa diwani huyo, wanachokifanya wao ni kutetea maslahi ya taifa
na wananchi waliowapigia kura, wala siyo kulinda biashara za watu hata
kama wanaungwa mkono na uongozi wa CCM.
Msimamo wa madiwani hao,
umekuja siku mbili baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman
Mbowe, kuwakaribisha Chadema madiwani wote waliofukuzwa katika manispaa
hiyo na kwamba kama wakijiunga na chama hicho, watafundishwa siasa za
mageuzi.
Mbowe aliwakaribisha madiwani hao katika mkutano wa
hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Uhuru Mjini Bukoba juzi, katika
mwendelezo wa mikutano ya chama hicho ya mabaraza ya wazi yanayojadili
rasimu ya Katiba mpya.
Katika mazungumzo yake, Mbowe alikwenda
mbali na kusema chama chake kiko tayari kushirikiana na kiongozi wa CCM
anayepinga ufisadi kama anavyofanya Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis
Kagasheki.
Alipoulizwa kama wamepata mawazo ya kujiunga na
Chadema, baada ya kauli ya Mbowe, diwani huyo alisema wao walishakuwa na
mawazo hayo, lakini kauli ya mwenyekiti huyo imewaweka huru zaidi.
“Si
kama tumeamua sasa, mawazo ya kuhamia Chadema tulikuwa nayo baada ya
uongozi wa mkoa kutangaza kutuvua uanachama, lakini kwa kauli ya Mbowe,
kutukaribisha rasmi Chadema, ametujengea moyo zaidi.
“Tatizo letu
na meya linafahamika kwamba, ni ufisadi wake tulioulalamikia tangu
mwaka jana kwenye vikao vya baraza la madiwani, hatukusikilizwa badala
yake tunaonekana wasaliti wa chama.
“CCM wanapaswa kujua kwamba,
hoja za wapinzani zikiwa sahihi wananchi wanawaunga mkono, vivyo hivyo
na sisi hatuwezi kubeza hoja zao kwa sababu tu ni wapinzani, tutaonekana
watu wa ajabu.
“Kimsingi, tumefarijika na kauli ya Mbowe, baadhi
yetu tulikuwapo katika mkutano wake jana (juzi) pale Uwanja wa Uhuru,
ni suala la muda tu mtasikia Bukoba imezaliwa upya,” alisema diwani
huyo.
Balozi Kagasheki ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini
(CCM), anatajwa kuwa na uhasama wa kisiasa na kada mwenzake, Anatory
Amani ambaye awali wawili hao walikuwa na ushirika wa karibu.
Alipotakiwa
kuzungumzia suala la kufukuzwa kwa madiwani hao, Kagasheki alisema yeye
hakuwepo katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa kilichowavua
uanachama.
Kuhusu taarifa za kutoelewana na Amani, alisema kila mmoja amekuwa na mtazamo wake juu ya mvutano huo.
“Kila
mtu ana maoni yake, siwezi kuzuia hisia na maoni ya watu wengine, kila
mtu anaweza kutoa maoni atakavyo, ngoja watu waseme,” alisema Kagasheki.
Madiwani
wanane waliofukuzwa wanatuhumiwa kushirikiana na wenzao wa upinzani
kusaini hati maalumu na kuiwasilisha kwa mkurugenzi wa manispaa,
wakimtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kumng’oa madarakani Meya
Amani.
Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera kilichokaa
Agosti 3 mwaka huu, kiliwafukuza uanachama na uongozi madiwani hao
akiwamo Mwenyekiti wake wa Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na Diwani wa
Kata ya Kashai.
Wengine waliofukuzwa ni Diwani wa Kata ya
Buhembe, Alexander Ngalinda, Samwel Ruhangisa (Kitendaguro), Dauda
Kalumuna (Ijuganyondo), Deus Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi
(Hamugembe), Richard Gasper (Miembeni) na Murungi Kichwabuta ambaye ni
Diwani wa Viti Maalumu.
-Mtanzania
Copyright © 2011.
TANGA LEO - All Rights Reserved
Post a Comment