MEYA WA CCM BUKOBA AKESHA OFISINI IKIDAIWA KUBADILISHA NYARAKA KISA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI.
MEYA wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, anadaiwa kukesha ofisini na baadhi ya watendaji wake, hatua inayoibua taharuki kwa wananchi kuwa huenda anabadili nyaraka kabla ya kukaguliwa.Hali hiyo imekuja zikiwa ni siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua miradi inayotek
elezwa na meya huyo baada ya madiwani kudai ina harufu ya kifisadi.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu kutoka mjini Bukoba, Amani alionekana kwa siku mbili na baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo ofisini usiku wa manane, hatua iliyowalazimu baadhi ya wananchi kuhoji ni kazi gani zinafanyika usiku kucha hasa wakati huu wa mgogoro.
Hatua ya Amani kujihami kila anapotakiwa kukaguliwa ilijitokeza hata miezi michache iliyopita wakati timu ya wakuu wa mikoa iliyoundwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kushughulikia mgogoro huo.
Kabla viongozi hao hawajafika mkoani humo, Amani alimrejesha kazini katibu muhtasi wake aliyekuwa amestaafu ili aweke mambo sawa.
Tayari baadhi ya madiwani wanaompinga meya huo, wamemtaka akae kando ili kupisha wataalamu wa CAG kufanya kazi yao bila kuingiliwa.
Wakizungumzia kitendo hicho cha meya kujifungia ofisini usiku na baadhi ya watendaji kabla ya CAG kuanza ukaguzi, walisema kinatia mashaka na kuitaka serikali imchukulie hatua haraka kabla ya kupoteza ushahidi mhimu.
“Tunatoa tahadhari mapema kwa serikali na CCM wajue kuwa mtuhumiwa ameanza kujihami kwa kukesha ofisini na watendaji wake, hili si jambo la kawaida CAG atapaswa kuwa makini zaidi,” walisema madiwani hao.
Amani hakupatikana kujibu tuhuma hizo kwani simu yake ya kiganjani haikupatikana hewani alipotafutwa.
Katika kumaliza mgogoro wa umeya mjini Bukoba, Kamati Kuu ya CCM (CC) ilitengua uamuzi wa kuwafukuza madiwani wanane wa manispaa hiyo, ambapo chama kilidai kuwa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kagera iliyokuwa imewafukuza ilikiuka katiba.
Kamati Kuu chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete ilimwagiza CAG kwenda mjini Bukoba wiki hii ili kukagua tuhuma hizo dhidi ya meya na kisha ripoti hiyo kuwasilishwa kwenye baraza ka madiwani ili hatua zaidi zichukuliwe ikithibitika alifanya ufisadi.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho cha CC kilichoketi hivi karibuni mjini Dodoma zilisema kuwa Kikwete alikiri timu iliyoundwa na Waziri Mkuu kuchunguza mgogoro huo kuwa ilibaini mianya ya ufisadi katika manispaa hiyo.
“Rais alisema hawezi kumfukuza meya kwa vile mamlaka hayo yako kwa madiwani waliomchagua, hivyo aliagiza CAG aende Bukoba kuchunguza tuhuma hizo halafu ripoti iwasilishwe kwenye baraza la madiwani hatua zichukuliwe,” alisema mtoa taarifa.
Hatima ya meya itategemea kitakachokuwa kimegunduliwa na CAG na kuwekwa katika ripoti hiyo.
“Baada ya hapo madiwani wanaweza kufanya lolote wanalotaka.
“Kama ni kumfukuza meya au la wataamua wao, kwa maana sasa watakuwa na vielelezo halisi mbele yao,” kilisema chanzo hicho.
Madiwani hao wanane waliorejeshwa na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza.
Wengine ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na Dauda Karumuna (Ijuganyondo).
Vile vile, Rais aliwataka meya na mbunge wafanye jitihada za kupatana na kufanya kazi pamoja kama ilivyokuwa zamani; hata wakitaka kutumia viongozi wa dini au wa kisiasa.
Katika hali inayoonyesha kuwa hoja ya ufisadi ndiyo ilikuwa kiini cha uamuzi wa CC kutofukuza madiwani, iliamuliwa pia viwanja 800 vilivyokuwa na mgogoro, warudishiwe wananchi waliokuwa wanavimiliki na wasitozwe hata senti tano.
Madiwani hao wamekuwa wanamlalamikia meya kuwa ameiingiza manispaa katika ufisadi kwenye miradi kadhaa. Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) ambao haukufuata taratibu na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko.
Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani.
Vilevile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90 lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka.
Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134 za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Kwa mujibu wa kanuni za manispaa hiyo yenye madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM, ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo. TANZANIA DAIMA.
Post a Comment