KASHFA YALIKUMBA JESHI LA POLISI TENA-CCTV ZAZIMWA KURUHUSU UJAMBAZI
SIKU chache baada ya tukio la wizi
mkubwa wa fedha katika Benki ya Habibu mjini Dar es Salaam, siri nzito
zimeanza kuvuja kuwa polisi wanadaiwa kuhusika katika tukio hilo kwa
kuhujumu kamera za usalama za CCTV zinazomilikiwa na jeshi hilo. Katika
tukio hilo, watu wanaodaiwa kuwa majambazi walipora dola za Marekani
20,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 32 za Tanzania.
Katika tukio hilo, Polisi Mkoa wa Ilala
inamshikilia askari mmoja kwa kosa la kuhusika katika tukio hilo
kutokana na kushindwa kuchukua hatua za haraka wakati tukio linatokea.
Habari za uhakika kutokana ndani ya
jeshi hilo, zinasema siku ya tukio polisi waliokuwa zamu kuongoza
mitambo hiyo, kwa namna moja au nyingine wanadaiwa kufanya hujuma hiyo,
kwa lengo la kupoteza mawasiliano na maeneo mengi ya polisi.
Chanzo chetu hicho, kiliongeza kuwa siku
ya tukio eneo lote la mzunguko wa barabara ya Uhuru na maeneo ya jirani
na Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL), sehemu zote hazikuwa na huduma ya
kamera za usalama, jambo ambalo si la kawaida kutokea.“Hatua iliyofikia sasa ni mbaya, huwezi amini siku ya tukio kamera za CCTV zinazotumiwa na polisi zilizimwa kabisa, kitendo hiki kilisababisha polisi makao makuu wasijue nini kinachoendelea pale.
“Ndiyo maana utaona kuna askari mmoja anashikiliwa katika tukio lile, haiwezekani kituo kikuu kishindwe kubaini uwapo wa tukio hili, wakati kuna mawasiliano ya kutosha, umefika muda wa kulisafisha jeshi letu kwa kasi,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho, kilisema mitambo ya kamera hizo, ilizinduliwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa mwaka 2004 na imekuwa ikifanya kazi bila matatizo yoyote.
“Nimekuwapo hapa tangu mwaka 2004, kamera hizi zilipozinduliwa rasmi na hazijawahi kuharibika hata siku moja, iwe siku ya tukio zisifanye kazi,” kilihoji chanzo chetu.
Askari aliyekamatwa katika tukio hilo, anadaiwa anafanya kazi katika kituo cha Oysterbay Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alithibitisha kukamatwa kwa askari huyo.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipoulizwa na MTANZANIA jana, alisema ameipokea taarifa hiyo na wanaifanyia kazi haraka iwezekanavyo.
“Taarifa hii tumeipokea, tunaifanyia kazi haraka sana ili kupata ukweli, naomba tuwe na subira,” alisema kwa kifupi Kamishna Kova.
Alisema bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba watu waliokamatwa watafikishwa mbele ya vyombo vya dola.
Post a Comment