MADAKTARI, MANESI WADAIWA KUFANYA VITENDO VYA KINYAMA IKIWEMO KUMNYWESHA KICHANGA MAJI YA DRIPU HOSPITALI YA ZAKHEM JIJINI DAR ES SALAAM,

MADAKTARI, MANESI WADAIWA KUFANYA VITENDO VYA KINYAMA IKIWEMO KUMNYWESHA KICHANGA MAJI YA DRIPU HOSPITALI YA ZAKHEM JIJINI DAR ES SALAAM


HOSPITALI ya Mbagala Zakhem, jijini Dar es Salaam, inakabiliwa na kashfa nzito, baada ya madaktari na wauguzi wake kudaiwa kuwafanyia vitendo vya kinyama wagonjwa, ikiwamo kumfukuza mama mjamzito mwenye uchun
gu usiku wa manane na mtoto mchanga kunyweshwa maji ya dripu.
Tuhuma hizo zimetolewa hivi karibuni na watu waliokumbwa na matukio hayo wakati walipofuata tiba hospitalini hapo.

Madai ya watu hao yalitolewa mbele ya Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile, wakati alipokutana na wananchi wa Mbagala Kichemchem kujua kero zinazowakabili.

Hata hivyo, madai hayo yalionyesha kumpa wakati mgumu mganga mkuu wa Hospitali hiyo, Julius Nyakazilibe, ambapo ilibidi aokolewe na mbunge huyo kufuatia wananchi hao kupinga utetezi wake.

Mwananchi wa kwanza kuituhumu Hospitali hiyo yenye hadhi ya Wilaya, alikuwa Omar Lipweremwike (50), ambaye alidai mke wake alifukuzwa usiku akiwa katika hali ya mwisho ya kujifungua na muuguzi mmoja kwa kile alichoelezwa muda huo hawezi kuzalisha mtu.

"Mama mjamzito akiwa katika hatua ya mwisho ya kujifungua hawezi kusubiri, lakini yule muuguzi alituambia tuondoke na turudi pale asubuhi ndipo atakuwa tayari kumuhudimia," alisema Lipweremwike.

Hata hivyo, alidai baada ya kuona hali hiyo, ilimbidi kumuwahisha kituo cha Afya cha Roundtable na alifanikiwa kujifungua salama muda mchache.

"Jambo hili ni baya sana tena linawanyanyasa wanawake kwa ujumla, haiwezekani Hospitali kubwa ikawa na wafanyakazi wazembe huku vituo vya afya vikisifika kwa huduma bora," aliongeza kusema.

Naye Ester Makunda. (25) alisema mtoto wake mchanga, Mariam Mohamed alinusurika kupoteza maisha baada ya wauguzi kukataa kumuwekea dripu ya maji kwa njia ya kawaida, badala yake walimlazimisha mama yake kumnywesha maji hayo kwa kutumia chupa ya maji safi.

Alisema tukio hilo lilitokea Agosti 15, mwaka huu, baada ya mtoto wake kuugua ugonjwa wa kuharisha.

Makunda alisema alipofika hapo alifuata taratibu zote ikiwamo kumuona daktari na mtoto kufanyiwa vipimo, baada ya majibu kutoka ilionekana ameishiwa maji, hivyo ilihitajika kuongezewa.

"Kitu cha kushangaza nilipofika wodini ili mtoto awekewe maji, wale wauguzi wakaanza kushindana wenyewe na baadaye walikataa wakanilazimisha nikanunue chupa ya maji ili niweke yale maji ya dripu ili nimnyweshe mwanangu, kwa kweli nilikataa," alisema Makunda.

Kama hiyo haitoshi, Makunda, alisema hata yeye mwenyewe wakati aliporudi kwa mara ya pili kupata matibabu kutokana na afya yake kutokuwa nzuri, aliambiwa maini yake yameharibika jambo ambalo si la kweli.

Alisema alibaini kitu hicho baada ya daktari aliyemuona siku hiyo kumshauri kumtafuta daktari bingwa wa maini wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, lakini baada ya kumtafuta daktari mwingine kwa ajili ya kuomba msaada zaidi alimueleza mtu aliyemuona awali hakuwa na utaalamu kwa sababu majibu ya vipimo vyake vinaonyesha yupo safi.

Tuhuma hizo zilimfanya Dk. Ndugulile kumuinua Mganga Mkuu wa hospitali hiyo kujibu, huku akimuambia afanye uchunguzi wa kina kubaini wafanyakazi wanaofanya vitendo visivyofaa kwa wagonjwa.

Wakati akijibu, Nyakazilibe aliwataka wananchi kumpigia simu haraka endapo watapata manyanyaso wakati wanapokwenda kupata huduma.
Alisisitiza ofisi yake ipo wazi muda wote kupokea malalamiko ya wananchi na kuyafanyia kazi.

Hata hivyo, aliwakasirisha wananchi hao na kuanza kupiga kelele za kumtaka akae chini, baada ya kuwaambia wananchi hao waache kutoa tuhuma kwenye mikutano ya viongozi kwani wanaweza kumuona yeye na kutatua kwa wakati.  CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger