Dk Ndalichako: Siasa zisipewe nafasi kwenye mitihani yetu;

Dk Ndalichako: Siasa zisipewe nafasi kwenye mitihani yetu; 

 

ndalichako_35ec2.jpg
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Joyce Ndalichako amesema siasa hazipaswi kupewa nafasi katika mchakato wa usimamizi wa mitihani na kwamba athari za mwenendo wa aina hiyo ni kubwa kwa taifa.Dk Ndalichako alisema akiwa kiongozi wa Necta hapendi ifike mahali ambako kila mtu atatakiwa afaulu hata kama hana sifa kwani madhara yake yatakuja kuonekana kwenye rasilimali watu siku zijazo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu Arusha hivi karibuni alisema: "Tukiruhusu mitihani iingiliwe na wanasiasa tutakuwa tunajimaliza wenyewe, kama ni wanasiasa wafanye kazi ya kushauri halafu waache wanataaluma husika wafanye kazi yao.

"Wanaohusika na kutunga sheria watekeleze jukumu lao siyo kuingilia moja kwa moja suala la mitihani. Sisemi kuwa tuachwe tu tufanye kazi kama tunavyotaka, ikibidi kuwe na chombo cha wanataaluma kutukagua, kwa sababu hii ni taaluma siyo kitu cha kila mtu kuingilia.

"Madhara ya kuingilia mitihani matokeo yake yataweza kuja kuonekana baada ya miaka hata 10 ijayo, ili kukwepa hali hiyo, kila mtu afanye kazi yake kama itaonekana watendaji hawana sifa waondolewe wawekwe wengine wenye sifa."

Dk Ndalichako ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuongoza Mabaraza ya Mitihani Afrika (AEAA) alisema: "Mtu akipewa alama asizostahili na akawa mwalimu atawafundisha nini watoto? Hawa ndiyo utakuta wana sababu zisizokwisha, kila siku utamsikia akisema watoto wa siku hizi hawaelewi kabisa."

Dk Ndalichako pia alipinga mawazo kwamba Necta inapaswa kushirikiana na wadau wa elimu katika kila kitu. Alisema ni hatari... "Tusifike mahali tuambiwe tuwaulize watoto tuwaletee maswali gani kwenye mtihani."
Kauli ya Dk Ndalichako imekuja wakati taifa likiendelea kuugulia maumivu yaliyotokana na matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne ya 2012 ambayo karibu nusu ya wanafunzi walifeli. Matokeo hayo yaliifanya Serikali kuunda tume iliyoogozwa na Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome ambayo ilipendekeza matokeo hayo yafutwe na yapangwe upya, hatua ambayo wengi waliita ni ya kisiasa.

Mahojiano kati ya Dk Ndalichako

Swali: Hii ni mara ya tano kwa Necta kuwa mwenyeji wa mkutano wa AEAA, na pia mmekuwa mkihudhuria mikutano kama hii inapofanyika nje ya nchi, ni nini hasa mmeona kuwa ni changamoto kwa mitihani inayotungwa katika ngazi ya shule?

Jibu: Hii mitihani inayotungwa shuleni ni changamoto sana, lakini ukiangalia utagundua kuwa tatizo lipo kwenye mitalaa ambayo walimu wanafundishiwa. Huko suala la ufundishaji limetiliwa mkazo sana lakini lile la kuwapima watoto halijapewa kipaumbele kabisa.
Wanachofundishwa huko ni kama orientation (utangulizi) tu, walimu wanatakiwa wajue mbinu gani zitumike kutunga mitihani.

Sisi kwenye ngazi ya taifa tunapotunga maswali tunazingatia mengi, kuanzia idadi ya watahiniwa na mambo kama hayo. Mwalimu darasani angetakiwa kutunga mtihani kwa kuangalia watoto wake na ajue ni mbinu gani za kutumia.

Tumekuwa tukifanya mafunzo kwa baadhi ya walimu kuhusu namna bora ya kutunga mitihani, ili waweze kufanya tathmini ya kile walichowafundisha watoto. Hata hivyo kwa kuwa sisi tupo wachache na mitihani yetu ni mingi tunashindwa kuwafikia wote. Tuna mpango wa kutoa mafunzo hayo kwa wakufunzi 200 wa walimu.

Swali: Vipi kuhusu ubora wa mitihani inayotungwa na Necta, mnadhani inakidhi viwango?
Jibu: Ubora wa mitihani inayotungwa na Baraza upo juu sana, hata usahihishaji wake ni wa hali ya juu. Mfumo wa kuwa kila mwalimu anasahihisha swali lake ni wa kipekee na sisi tulikuwa kati ya nchi za kwanza kuutumia.

Kuna nchi mtu anapewa burungutu la mitihani ya watoto anakwenda nayo nyumbani kusahihisha akishamaliza analeta majibu kisha watoto wanatangaziwa. Sisi mfumo wetu ni bora sana na sijui kwa nini watu wanakuwa na mtazamo hasi na Necta. Sifa kubwa ya baraza lolote lile la mitihani ni kutoa majibu yanayofanana na hali halisi ya elimu ilivyo.

Tunachotaka siku zote kuona ni mtu anapewa kile anachostahili. Watu wengine wanasema mitihani inayotungwa na kupewa watoto wote siyo sawa kwa sababu kuna baadhi ya shule walikuwa hawana walimu au vitabu, sasa swali la kujiuliza nani alitakiwa kutoa hivyo vitabu?

Kwa vipi utunge mtihani mmoja useme ni kwa ajili ya shule ambayo haina vitabu na walimu! Ni watoto gani ambao tumewaandaa kwa sababu ya kwenda kwenye hizo shule?

Naona ni bora kabisa shule isiwepo kama hakuna walimu na vitabu kwa sababu hii ndiyo roho ya elimu. Kukiwa na walimu na vitabu watoto wanaweza kukaa hata chini ya mti na wakafundishwa na kupata maarifa.

Necta tunatunga maswali kwa kuzingatia vitu vingi na kutokana na suala la uwazi, kila swali linalotungwa kuna sehemu tunaonyesha mada ambayo swali hilo lilipotolewa kwa mujibu wa silabasi pia kuorodhesha baadhi ya vitabu vyenye mada hiyo, mpaka ukurasa tunaonyesha. Hata Tume ya Waziri Mkuu walipokuja tuliwaonyesha vitu vyote hivyo.

Swali: Katika mkutano huu, baadhi ya mambo yaliyozungumziwa ni pamoja na athari za siasa kuingizwa kwenye mitihani, kwa upande wa Tanzania unazungumziaje hali hiyo?

Jibu: Tukiruhusu mitihani iingiliwe na wanasiasa tutakuwa tunajimaliza wenyewe, kama ni wanasiasa wafanye kazi ya kushauri halafu wawaache wanataaluma husika wafanye kazi yao, wanaohusika na kutunga sheria watekeleze jukumu lao siyo kuingilia moja kwa moja suala la mitihani.

Sisemi kuwa tuachwe tu tufanye kazi kama tunavyotaka, ikibidi kuwe na chombo cha wanataaluma kiwe kinatukagua, kwa sababu hii ni taaluma siyo kitu cha kila mtu kuingilia.

Madhara ya kuingilia mitihani matokeo yake yataweza kuja kuonekana baada ya miaka hata 10 ijayo, ili kukwepa hali hiyo kila mtu afanye kazi yake kama itaonekana watendaji hawana sifa waondolewe wawekwe wengine wenye sifa.

Tukitaka kila mtu afaulu hata kama hana sifa madhara yake yatakuja kuonekana kwenye suala la rasilimali watu, mtu akipewa alama asizostahili na akawa mwalimu atawafundisha nini watoto? Hawa ndiyo utakuta wana sababu zisizokwisha, kila siku utamsikia akisema watoto wa siku hizi hawaelewi kabisa.
Pia hili suala la kusema kila kitu tushirikishe wadau ni la kuangalia. Tusifike mahali tuambiwe tuwaulize watoto tuwaletee maswali gani kwenye mtihani.

 

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger