TASAF II ilivyogeuza changamoto ya uhaba wa chakula kuwa fursa ya uchumi na maendeleo kwa wananchi wa korogwe vijijini
Mzee Rajabu Kufa mlemavu wa macho na
mkazi wa kijiji cha Kwetonge kilichopo kata ya Mashewa mmoja wa wakazi
wa Korogwe ambao wamenufaika na mradi wa TASAF II wa ufugaji ng’ombe
kupitia kikundi cha Jipemoyo.
Watu wengi duniani
huziona changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku kuwa ni
vikwazo vya kutofikia malengo waliyojiwekea au wanayopaswa kuyafikia
kama binadamu.Ni watu wachache sana wenye ujasiri wa uthubutu katika
maisha yao,hata ikawapelekea wenye busara kutengeneza msemo wa “uoga
wako ndiyo umasikini wako” wakilenga kuwatia watu moyo na kuwataka kuthubutu hasa katika masuala yenye changamoto.
Korogwe vijijini yenye
ukubwa wa kilomita za mraba 3544,kata 20,vijiji 122,vitongoji 610 na
jumla ya Wakaazi 242,038 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 ni moja ya
jamii iliyojipatia manufaa kwa kutumia hekima za msemo huo.Korogwe
ambayo kilimo ndiyo njia kuu ya wakaazi wake kujipatia chakula na kipato
kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2010 imekuwa ikipata mvua za
kubahatisha jambo lililopelekea kukabiliwa na uhaba wa chakula kwa
baadhi ya maeneo na maeneo mengine kukumbwa na njaa hata kupelekea
Serikali kupeleka chakula cha msaada.
Pamoja na kukabiliwa
na changamoto hiyo wakaazi hao hawakukaa na kuiangalia njaa ikiharibu
maisha yao,badala yake kwa kutumia fursa zilizopo kama Mfuko wa
maendeleo ya Jamii (TASAF II) iliyokuwa ikitekeleza program zake
wilayani humo waliiona ni nafasi nyingine ya kujipatia maendeleo
endelevu,wakaonesha uhitaji wao,wakathubutu na kwa kushirikiana vyema na
Wataalamu wa kada mbalimbali katika Halmashauri, leo hii Wananchi hao wanajivunia mafanikio yao.
Edward Lukinisha
ambaye ni mratibu wa Mfuko wa maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya
wilaya ya Korogwe anaeleza kwa kina jinsi jamii ya wanakorogwe
ilivyofaidika na changamoto ya uhaba wa chakula kwa kuigeuza kuwa fursa
ya kiuchumi,na kwamba sasa Wananchi hao wanayo miradi inayowaingizia
kipato na kuwahudumia kila siku hata wameondokana kabisa na changamoto
ya uhaba wa chakula.
“Korogwe ilipotangazwa
kuwa ni moja ya wilaya zinazokabiliwa na uhaba wa chakula,TASAF kama
Mfuko wa kusaidia jamii katika fedha za bajeti kuanzia mwaka 2010
tulikaa na baadhi ya vijiji na kuwataka waibue miradi ambayo si tu
ingekidhi haja ya kumaliza uhaba wa chakula kwa wakati huo,bali pia
ingekuwa ni miradi endelevu hata kwa vizazi vijavyo” alisema Lukinisha.
Anafafanua kuwa
uibuaji wa miradi hiyo iliyogawanyika katika Sekta kuu tatu za
mawasiliano,kilimo na ufugaji uliolenga kukabiliana na uhaba wa chakula
ulikuwa katika sura mbili,miradi ambayo ingeinufaisha jamii moja kwa
moja na miradi ya vikundi.Katika miradi ya jamii iliwapasa wanajamii
wenyewe kuibua miradi endelevu ambayo ingeinufaisha jamii nzima na
kisha kubainisha kaya zizoathiriwa zaidi na uhaba wa chakula, hivyo wale
wenye uwezo wa kufanya kazi katika kaya hizo ndiyo ambao wangefanya
kazi ya ujenzi wa mradi wa jamii na kulipwa ujira ambao ungewasaidia
kupata chakula kwa wakati huo,na wakati huo huo jamii nayo ingenufaika
kwa kupata mradi endelevu.
Moja ya miradi iliyojengwa wilayani humo kutokana na changamoto hiyo ni barabara ya kijiji cha Changarikwa kilichopo kata ya Magamba
Kwalukonge.Barabara hiyo ilichimbwa kwa urefu wa km 5.5 na upana wa mita
4.5 kwa gharama ya Tsh ml 32 zilizotolewa kwa Wananchi hao kama ujira.
Rukia Hamisi aliyekuwa mmoja wa
washiriki katika ujenzi wa mradi huo anasema barabara hiyo ilianza
kuchimbwa mwaka 2010 na kukamilika 2011,ambapo wataalamu wa Halmashauri
walipima na kutoa ushauri na wao Wananchi walichimba kwa ujira wa Tsh
3000 kwa kutwa.Fedha ambayo anasema ndiyo ilikuwa ikimsaidia kununua
chakula kwa ajili ya familia yake.
“Barabara
hii licha ya kuwa sasa inatusaidia sana kwa usafirishaji wa mazao
yetu,lakini wakati wa kuitengeneza ilitusaidia sana kwani tulioichimba
tulilipwa na fedha ile tuliitumia kwa kununua chakula kwani hatukupata
kabisa mazao kwa mwaka ule.”Anasema Rukia.
Naye bi.Ndatima Shemshi anaongeza kuwa
hapo mwanzo walitembea umbali mrefu kwa miguu kwani ilikuwa ni vigumu
kwa magari kufika kijijini kwao,lakini sasa magari yanaingia hadi
kijijini na kubeba mazao yao kama mahindi na ngwasha ambayo hununuliwa
sana na Wakenya kwa ajili ya kutengenezea biskuti. Hata hivyo mama huyo
ana ombi maalum kwa wadau wenye uwezo kuwekeza zaidi katika barabara
hiyo ili iweze kutokezea kitongoji cha Mlembule katika Mamlaka ya Mji
mdogo wa Mombo ambako ndipo kuliko na barabara kuu inayounganisha nchi
za Afrika Mashariki kupitia Arusha.
Sekta ya mawasiliano inapewa nafasi pia katika kijiji cha Makumba ambapo
wanakijiji hao kwa pamoja wanaamua kujenga kivuko kitakachounganisha
kijiji chao na kijiji cha Kazita.Wanakijiji hao wa Makumba wanapata
msukumo wa kujenga kivuko hiki ili kuisaidia jamii kubwa ya wenzao waishio katika kijiji cha kazita katika vitongoji vya Magunga na Mtemiroda huku huduma zote muhimu za kijamii zikipatikana kijiji cha Makumba.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Makumba
Petro Harawa anasema kimsingi vijiji hivyo viwili ni kama kijiji kimoja
cha watu 3069 huku 800 kati yao wanaoishi Kazita wakitenganishwa na
bonde korofi hasa nyakati za mvua,hivyo kama kijiji waliona ni vyema
kujenga kivuko kitakachowaunganisha nyakati zote na ndipo TASAF II
ilipowapatia ml 28 na kuanza ujenzi wa kivuko hicho Mei 2012.
Oddos Komba Mwanakijiji wa Kazita
pamoja na kushukuru kwa kuondokana na njaa pia anasifu jitihada za
Serikali za kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na uchukuzi vijijini
kwa kuielezea kadhia waliyokuwa wakiipata hapo awali hasa nyakati za
masika huku akitolea mfano wa mwaka 2006 pale
wanafunzi wa kijiji cha kazita waliposhindwa kufanya mtihani wa darasa
la nne kutokana na mvua kubwa kusababisha mahali hapo kutokupitika na
kukifikia kijiji cha Makumba ambako ndikokuliko na shule.
Sambamba na mawasiliano miradi mingine
iliyokusudiwa kuinufaisha jamii nzima ni ile ya Sekta ya kilimo, ambayo
ni ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji.Katika utekelezaji wa kusudio hilo
vijiji vinne ambavyo ni Chekelei, Mazinde Mheza,Mazinde Goha na
Makangara Songea vilinufaika nayo.
Michael Cassian ambaye ni Mwenyekiti wa
kamati ya mradi wa mfereji wa umwagiliaji kijiji cha Chekelei anasema
kuwa wao walipatiwa ml 31 ambazo zimeweza kuchimba
na kujenga mfereji wenye urefu wa mita 200 pamoja na vigawa maji
nane.Mradi huo ulioanza kujengwa mwaka 2011 ulikamilika 2012 na tayari
Wakulima wameanza kutumia katika msimu huu wa kilimo wakiwa na matumaini
ya kuongeza uzalishaji wa mpunga mara dufu kwa sababu sasa hivi maji
yanafika mashambani kwa uhakika na kwa kipimo kinachotakiwa.
Wakati Chekelei wakisubiri mavuno,
kijiji cha Mazinde Goha wao wanajivunia mavuno ya matunda aina ya
matikiti maji tani sita katika msimu wa kwanza kabisa April 2012 mara tu
baada ya kukamilika kwa mradi wao Januari 2012, na sasa wanajipanga
kufanya kilimo cha pilipilihoho,vitunguu , nyanya na mbogamboga kwa
kipindi cha kiangazi.
Iddi Uledi Mwenyekiti wa kikundi hicho
kiitwacho Songambele anasema walipatiwa ml 8.9 za kuchimba kisima na
ununuzi wa mipira yenye uwezo wa kuhudumia ekari 15 za shamba ambazo
walipewa na kijiji,lakini mpaka sasa wametumia ekari nne tu huku
wakiendelea na juhudi za kufyeka pori lililobaki ili waweze kunufaika
zaidi
Katika harakati hizo za kuwapunguzia
Wananchi makali yatokanayo na uhaba wa chakula TASAF II iliwekeza pia
katika sekta ya mifugo huku wanufaika wakishuhudia ya kwamba wamepata
faraja kubwa kwa kupata miradi ya ufugaji ng’ombe na mbuzi kwani mbali
ya kuwapatia kipato pia imeimarisha afya zao kwa kunywa maziwa kila
siku.
Miradi hiyo ya ufugaji ilitolewa kwa
vikundi vya watu kumi na nne na kumi na tano kwa vigezo vya kuathiriwa
na uhaba wa chakula na kuwa katika makundi maalumu ambayo ni
walemavu,wajane na wagane, na kwa kuzingatia uwiano wa jinsia.
Rajabu Kufa ni mlemavu wa macho na
mkazi wa kijiji cha Kwetonge kilichopo kata ya Mashewa anasema yeye
amenufaika na mradi wa TASAF II wa ufugaji ng’ombe kupitia kikundi chao
cha Jipemoyo.Anasema ng’ombe wake aliyempa jina la Sara amekuwa mkombozi
mkubwa sana kwake hasa kwa kuzingatia hali yake isiyomwezesha kufanya
kazi nyigine ngumu.
“Ng’ombe huyu ananisaidia sana kwani
napata lita nne kila siku ambazo naziuza kwenye kituo cha maziwa
kilichopo hapa kijijini kwetu,napata pesa za kujikimu mahitaji yangu
kutokana na ng’ombe huyu,hivyo imenisaidia kuondokana na tatizo la
kuombaomba na kuwa na uhakika wa kupata chakula kila siku”.Anasema Kufa.
Mzee huyu anakiri kuwa hawezi
kumhudumia ng’ombe wake yeye mwenyewe,lakini ng’ombe huyo wa asili
aliyeboreshwa ili kutoa maziwa ana afya njema sana.Kufa anasema ng’ombe
huyo huhudumiwa na mtoto wake ambaye humkatia majani ya kutosha kwa siku nzima kila asubuhi kabla ya kwenda kwenye shughuli zake.
Anaongeza kuwa kijana wake ana furaha
sana kumhudumia ng’ombe huyo kwani amempunguzia majukumu ya kumgharamia
yeye kifedha.Mzee Kufa anaishukuru Serikali kwa kuleta mradi wa TASAF
kwa wahitaji kama yeye na kusema kwake yeye hakika Serikali imemjali
sana,pia anaishukuru Jamii ya kijiji chake kwa kuuona uhitaji wake na kumchagua kupewa ng’ombe huyo.
Naye Bi. Stara Ponda mjane aishie
katika kijiji hicho cha Kwetonge anasema mbali ya ng’ombe wake
kuimarisha afya ya familia yake wakiwemo watoto ambao ni wajukuu zake
anaowalea kwa kunywa maziwa lakini pia ng’ombe huyo humsaidia kupata
mahitaji ya shule ya watoto kwa kuuza maziwa kila siku.
Wakati Wananchi hao wakifurahia
ufumbuzi wa tatizo la uhaba wa chakula na kujipatia miradi ya maendeleo,
Afisa Kilimo na Ushirika wa Halmashauri ya wilaya ya Korogwe Kakulu
Lugembe anakiri kuwa katika kipindi cha mitatu maeneo mengi ya Halmashauri yamepitia kipindi kigumu cha upungufu wa chakula hata kupelekea Serikali kuleta chakula cha msaada.
“Novemba 2012 Halmashauri ilipokea tani
111.8 za mahindi ya msaada toka Serikalini na kugawa katika vijiji 60
vya Kata 12 na Machi 2013 ilipokea tani 350.6 na kugawa katika vijiji 63
vya kata 12” anasema Lugembe.
Hata hivyo anasifu jitihada
zilizochukuliwa na TASAF II kwani zilisisimua uwajibikaji kwa kuwa suala
la upungufu wa chakula husababishwa na mambo mengi ikiwemo uvivu wa mtu
husika,majanga kama mafuriko na
mabadiliko ya tabianchi.Anaielezea hali ya chakula kwa mwaka huu kuwa
ina ishara njema kwani hali ya mazao mashambani ni nzuri ukiachilia
mbali kata nne tu za Mashewa,Mkomazi,Mkalamo na Mazinde.
Lugembe anawapongeza zaidi Wananchi
waliochagua ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji kwa kueleza kuwa kwa sasa
kilimo cha uhakika na tija ni cha umwagiliaji kutokana na mabadiliko ya
hali ya hewa yasiyotabirika.Anaeleza kuwa hata Halmashauri imeelekeza
nguvu zake katika ujenzi wa skimu za umwagiliaji ikiwemo ya Kwemkumbo
katika mamlaka ya mji mdogo Mombo na katika bonde la Mkomazi ambazo
zinatarajiwa kukamilika mwaka 2014.
Anatoa wito kwa Wananchi kutumia kanuni
bora za kilimo kwa mazao yote,kulima mazao mbadala yanayostahimili
ukame kama mtama,muhogo na viazi vitamu na zao la biashara la alizeti
kwa maeneo yasiyo na mvua za kutosha.Anasisitiza zaidi Wananchi kutumia
chakula kwa uangalifu,kujiwekea akiba na kuacha uuzaji holela ili
kuepuka upungufu wa chakula mara kwa mara.
Post a Comment