Jinsi uboreshwaji wa Miundo Mbinu Mkoani Tanga umesaidia kukuza Uchumi

Jinsi uboreshwaji wa Miundo Mbinu Mkoani Tanga umesaidia kukuza Uchumi 

Mkoa wa Tanga umejaliwa kwa kuwa na ardhi nzuri na yenye rutuba, fukwe nzuri za bahari za kihistoria, safu za milima ya Usambara inayovutia, mabonde na maporomoko mazuri ya maji  na mbuga za wanyama ambazo huvutia sana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kutoa fursa nyingi za kimaendeleo kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Mkoa huu ni kiungo muhimu sana katika historia ya uchumi nchini Tanzania. Kwa upande wa Kaskazini Tanga imepakana na nchi jirani ya Kenya, vilevile imepakana na Mikoa ya Kilimanjaro na Manyara upande wa magharibi, imepakana na Mikoa ya Morogoro na Pwani upande wa kusini na upande wa Mashariki imepaka na Visiwa vya Unguja na Pemba.

Kuwepo kwa miundo mbinu mizuri ya barabara, reli, bandari na usafiri wa anga vyote kwa pamoja vinauweka Mkoa wa Tanga katika nafasi nzuri ya kuwa miongozi mwa Mikoa ambayo mtu mmojammoja au mashirika huvutiwa kuwekeza. Ni fursa hizi zote pamoja na ushirikiano mzuri wa wadau mbalimbali, wananchi na Serikali, Mkoa umeweza kupiga hatua katika Nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiulinzi, kitekinologia, kimazingira na kiutamaduni.

Wakazi wa Tanga pia wamepata fursa ya kufikiwa na huduma za kijamii kwa wepesi zaidi kutokana na kuwa na usafiri wa uhakika. Jambo hili limesaidia kuokoa muda na hivyo wananchi kujishughulisha na uzalishaji badala ya kutumia muda mwingi njiani kwenda kufuata huduma za kijamii kama afya n. k.

Barabara ya Tanga –Horohoro ni barabara yenye kiwango cha lami na urefu wa kilometa 65 ambayo inaunganisha Mkoa wa Tanga na Nchi jirani ya Kenya. Ikianzia kutoka Wilaya ya Tanga inaunganisha  Wilaya ya Mkinga  na kisha kuunganisha nchi ya Kenya. Wakazi wa Tanga kwa sasa wana fursa ya kusafirisha mazao yao ya biashara katika Wilaya zilizotajwa na pia kuyapeleka mazao yao  nchi jirani ya Kenya. Hivyo kupanua wigo wa masoko ya biashara kwa wakazi wa Tanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete  ( Mwenye koti la blue bahari) akiwa na Mwenyeji wake  Mhe. Chiku Gallawa  ( wa tatu kushoto kwake ) wakati wa ufunguzi wa barabara ya Tanga- Horohoro  eneo la Kasera Wilayani Mkinga mwezi Aprili mwaka huu.
Nayo barabara ya yenye kilometa 65 kwa kiwango cha wami inayounganisha Wilaya ya Handei na Korogwe ambayo iko mbioni kukamilika inategemewa kuwa kiungo kikubwa cha usafiri na hivyo kuboresha maisha ya wakazi wa Tanga na wawekezaji.
Barabara ya Handeni- Korogwe yenye kilometa 65 kwa kiwango cha lami.

Uwepo wa Uwanja wa Ndege ambao hurahisisha usafiri wa anga. Wakazi wa Tanga na Wageni huweza kuokoa muda kwa kutumia njia ya anga ambayo hutumia muda mchache kuweza kufika katika maeneo mabalimbali ya Tanzania na nchi zingine. Nayo Bandari ya Tanga ni muhimu sana katika uchumi wa Tanga. Uboreshwaji wake katika  kujenga bandari ya nchi kavu ya Mwambani itasaidia kukidhi mahitaji ya wakazi wa Tanga, Tanzania na dunia kwa ujumla.
Bandari ya Tanga
Jina Tanga lilitolewa na wafanyabiashara wa kishirazi likiwa na maana nne ambazo ni Tambarare, mabonde ya Kijani, Barabra za milima na Kilimo cha Milimani. Mkoa wa Tanga ni mkulima na msafirishaji mkubwa wa zao la Mkonge duniani ambalo ni  muhimili wa kukua kwa uchumi wa nchi ya Tanzania.
Zao la Mkonge
Mkoa wa Tanga una eneo la ukubwa wa quare km 27,342 na jumla ya idadi ya watu 2,045,205 wakiwemo wanaume 992,347 na wanawake 1,052,858 ( sense ya  2012) na una jumla ya Wilaya nane ambazo ni Handeni, Kilindi, Korogwe, Lushoto, Muheza, Mkinga, Pangani na Tanga Halmashauri za Wilaya, Miji na Jiji zipo 11 ikiwemo mpya ya Bumbuli iliyoanzishwa hivi karibuni.
Kwa kuzingatia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2025, ambapo sekta za Viwanda, Biashara na Masoko zinatakiwa kuwa miongoni mwa mihimili mikuu katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa kulifanya Taifa lifikie kiwango cha kati cha maendeleo ya uchumi, Mkoa wa Tanga kwa kutekeleza majukumu yake umeamua kushirikisha Sekta Binafsi katika kuendeleza sekta ya Viwanda, Biashara na Masoko.
Lengo kuu la mkakati huo ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji katika mkoa wetu sambamba na kujenga uchumi endelevu, unaostahimili ushindani katika masoko ya ndani na nje ikiwa ni chachu ya kuchochea kasi ya maendeleo kiuchumi.
Kihistoria Mkoa wa Tanga ulitumiwa sana na wakoloni wa Kireno, Kiarabu, kijerumani na mwishoni Waingereza ukiwa lango la biashara na uchumi kwa kuunganisha sehemu za ndani za Africa Mashariki na Kati na sehemu mbalimbali za dunia kupitia bahari ya Hindi. Kutokana na mwingiliano wa tamaduni mbalimbali, wenyeji wa Tanga wamerithi tamaduni, lugha na ustarabu wa mataifa mbalimbali ya Washirazi, Waarabu , Wachina, Wahindi, Wareno, Wajerumani, Waingereza na Waswahili.

 

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger