WANANCHI WENYE HASIRA WAUCHOMA MOTO MSIKITI WA ANSAR SUNNI KILINDI.

WANANCHI WENYE HASIRA WAUCHOMA MOTO MSIKITI WA ANSAR SUNNI KILINDI.

PASKAL MBUNGA,KILINDI
WANANCHI wenye hasira na ambao bado hawajafamika wameuchoma moto na kuubomoa kabisa msikiti unaotumiwa na  waumini wa dhehebu la dini ya kiislamu la Ansar Sunni wanaoaminika kuwa chanzo cha  chokochoko  na machafuko yaliyosababisha  mauaji ya watu hivi karibuni katika kijiji cha Lulago, Kata ya Lwande wilayani Kilindi.
 
Sambamba na ubomoaji huo wa msikiti, lakini pia wamezichoma moto nyumba 16 zinazokaliwa na wafuasi hao wa Ansar baada ya wao kukimbilia misituni wakikwepa kukamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama kutokana na kuhusika kwao na mauaji ya mwanamgambo kijijini hapo.
 
Akizungumza na waandishi wa habari i waliotembelea kijiji hicho mwanzoni mwa juma hili, Mwenyekiti wa kijiji cha Lulago, Mohamed Waziri Mwariko (48), alisema kwamba baada ya kuzusha furugu na machafuko kijijini hapo  juma lililopita ambapo walimwua askari mgambo kwa kumkata mapanga, , walikimbia na kwenda kujificha misituni ambapo mpaka sasa hawajonekana.
 
Mwariko alisema wafuasi hao ambao wanajinadi kuwa ni waislamu safi na kuwaita waislamu wengine ni makafir, walianza kukinzana na uongozi wa serikali ya kijiji kwa kuwashawishi watu wasiiti serikali iliyoko madarakani wakidai kuwa ni ya kikafir na hivyo kukataza wasilipie ushuru kwa kijiji.
 
Akisimulia chanzo cha vurugu kilichopelekea mauaji hayo, Mwariko alisema kuwa tarehe 23 Oktoba mwaka huu, mfanya biashara Haji Mtana alinunua iliki gunia mbili na kulipia ushuru wa  kijiji wa shilingi 20,000 ambapo walitokea wafuasi hao na kumtaka mnunuzi huo asilipie kwa madai kuwa serikali ya kijiji na serikali kuu zote ni za kikafiri.
 
Uongozi wa kijiji ulipowaita kuja kutoa maelezo ya matamshi yao, walikataa wito na ndipo uongozi wa kijiji uliwatumia mgambo ambaye walimwua  kwa kumkata mapanga na kisha kuanza kutamba kijijini hapo kwa kufyatua ovyo risasi.
 
Mwenyekiti huyo alieleza kwamba pamoja na uongozi wa kijiji kutoa taarifa polisi, lakini wananchi waliingiwa na hofu baada ya kuchinjwa mgambo huyo kwani wananchi walizihama nyumba zao na kukimbilia porini kujificha
 
”:Kwa kusaidiana na majeshi ya ulinzi na usalama, wananchi hao waliweza kuwakamata wafuasi 16 pamoja na silaha walizotumia zikiwemo bunduki 4 bastola 2, mapanga 18 na visu 12”, alisema Mwariko na kuongeza kwamba viongozi wakuu wa kikundi hicho walikimbilia misituni  na hawapatikana hadi sasa..    
 
Mwenyekiti huyo wa kijiji alisema kutokana na hasira walizokuwa nazo wanakijiji juu ya watu hao ambao walihamia kijijini hapo mwaka 2009 wakitokea Dar es Salaam hawataki warudi tena katika maeneo yao waliyoyahama.
 
Idadi kubwa ya wakazi wa Kijiji cha Lulago chenye watu 4063 ni Waislamu ambao ni karibu 99.5% ya wakazi wote. ,
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger