BABU SEYA, PAPII KOCHA VICHEKO VYAANZA

BABU SEYA, PAPII KOCHA VICHEKO VYAANZA

Stori: Richard Bukos na Denis Mtima
MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ pamoja na ndugu zao, Jumatano iliyopita walitoka kwa vicheko katika Mahakama ya Rufaa Tanzania baada ya kuridhishwa na utetezi uliotolewa na wakili wao, Mabere Marando, anayepinga hukumu ya kifungo cha maisha jela, waliyopewa wanamuziki hao.

Mbele ya majaji watatu wa Mahakama hiyo, Marando alikabiliana na timu ya mawakili watano waandamizi wa serikali ambao ni Jackson Brashi, Angaza Mwaipopo, Imaculate Banzi, Joseph Pande na Apimark Mabruk.

Miongoni mwa hoja ambazo Marando alionekana kuwabana mawakili wa serikali ni jinsi Jamhuri ilivyowatia hatiani wateja wake kwa kutumia ushahidi uliotolewa na watoto katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar, akisema zipo taratibu za kuchukua katika ushahidi kwa mtoto ikiwemo kurekodiwa, jambo ambalo halikufanyika.

Marando alizidi kuweka wazi kuwa katika ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, ulionesha nyumba iliyodaiwa kufanyiwa uhalifu huo ilikuwa na mlango wa siri uliotumiwa na watoto hao kupenya hadi ndani pasipo kuonekana jambo ambalo baadaye lilidhihirika si kweli kwani nyumba hiyo haikuwa na mlango mwingine zaidi ya wa uani na barazani.

Hata hivyo, jopo la mawakili wa Jamhuri licha ya kukumbana na wakati mgumu kutoka kwa wakili Marando, liliendelea kusisitiza kuwa hukumu iliyotolewa dhidi ya washitakiwa hao ilikuwa sahihi.

Baada ya mawakili hao kusisitiza hivyo Marando alipewa nafasi nyingine ya kutoa utetezi wake, ambapo aliendelea kufafanua makosa mbalimbali yaliyofanyika kuwahukumu wateja wake kwa kutaja vifungu vya sheria ambavyo vilionekana kama kuwasafishia njia wateja wake hao hali iliyozua tabasamu na vicheko mahakamani hapo.

Baada ya kupitia marejeo ya kesi hiyo kwa pande hizo mbili, jopo la majaji akiwemo, Salum Masatti liliahirisha kesi hiyo na kusema litapanga siku ya hukumu huku wafungwa hao wakirejeshwa gerezani wakiwa na vicheko vya furaha huku ndugu na jamaa nao wakikumbatiana kwa shangwe.

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger