Wafanyakazi walaumu:wahamiaji haramu wameajiriwa kwenye nafasi nyeti JNIA

Wafanyakazi walaumu:wahamiaji haramu wameajiriwa kwenye nafasi nyeti JNIA

julias_airport_489c3.jpg

Baadhi ya wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam wamedai kuwepo kwa wafanyakazi ambao ni wahamiaji haramu katika uwanja huo, ambao wamekuwa wakipewa nafasi nyeti katika mamlaka hiyo.

Aidha, wameeleza kuwa wahamiaji hao haramu pia wamekuwa wakipatiwa vitambulisho nyeti kama watanzania halisi.

Wafanyakazi walimueleza Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe jana alipofanya ziara uwanjani hapo na kuzungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) katika uwanja huo.


Mfanyakazi Dominic Bomani alisema licha ya juhudi za serikali kuwaondoa nchini wahamiaji haramu, kiwanja hicho cha ndege kimekuwa chimbuko la wahamiaji hao ambao wamekuwa wakipewa nafasi nyeti.

Aliomba serikali kusaidia katika kuwabaini na kuwaondoa wahamiaji hao ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi hizo ziweze kushikiliwa na watanzania ambao wako wenye sifa stahili.

Dk Mwakyembe alishukuru kwa taarifa hizo na kuahidi kufanyia kazi huku akimtaka mfanyakazi huyo kufika ofisini kwake ili kumpa taarifa zaidi.

"Nashukuru kwa taarifa hizo kwani hatukuwa nazo na ninaahidi kuanza kuzifanyia kazi na kutoa majibu yake haraka kuanzia Jumatatu (kesho)," alisema.
Kuwepo kwa wafanyakazi wahamiaji haramu kumeonekana huenda ikawa ndiyo sababu ya matukio
yaliyotokea katika uwanja huo ya kupitisha dawa za kulevya kutokana na wahusika kutokuwa na uzalendo na taifa hili.

Katika siku za hivi karibuni serikali ilianzisha operesheni za kuwarejesha makwao wahamiaji haramu kutoka nchi mbalimbali.

Operesheni hiyo iliyobatizwa jina la 'Kimbunga' iliahidiwa na Rais Jakaya Kikwete akiwa mkoani Kagera hivi karibuni, baada ya kuwataka wahamiaji haramu kurejea walikotoka au kufuata taratibu za kisheria za kuishi nchini, huku akionya kinyume cha hapo, kwa kuwa miongoni mwao wanajihusisha na ujambazi, watasakwa misituni, majumbani na hata ardhi itachimbuliwa, kutafuta silaha walizozifukia ilianza kwa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kumalizika katika mikoa ya Geita, Kagera Kigoma.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe, aliyekuwepo katika mkutano huo wa Rais Kikwete alisema ni wahamiaji haramu 11,601 tu walioondoka wakati uongozi wa mkoa huo, ulitarajia wahamiaji haramu kati ya 52,000 na 53,000 waondoke.

Mkuu wa Operesheni hiyo ya Kimbunga, Kamanda Simon Sirro alisema tangu operesheni hiyo ianze, wahamiaji haramu 1,851 wamekamatwa, ng'ombe 1,763 na silaha za moto saba, bunduki za kienyeji maarufu magobori sita na shotgun moja katika mikoa lengwa ya Kagera, Kigoma na Geita.
Katika Mkoa wa Kigoma, operesheni hiyo imefanikiwa kukamata wahamiaji haramu 885, silaha mbili, gobori moja na shotgun moja na ng'ombe 200.

Mkoani Geita, wahamiaji haramu 246 wamekamatwa, magobori matatu, ng'ombe 240, sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kibuyu cha maji cha jeshi hilo.
Katika mkoa wa Kagera, wamekamata wahamiaji haramu 750, magobori mawili na ng'ombe 1,323. Mbali na silaha hizo zilizokamatwa, silaha zingine 65 zimesalimishwa; SMG tatu, shotgun 10 na magobori 52.
Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, silaha nyingi zilisalimishwa katika wilaya ya Biharamulo na ndizo zilizokuwa zikitumika katika utekaji na unyang'anyi katika mapori wilayani humo.

Jijini Dar es Salaam, Operesheni Kimbunga kwa ajili ya wahamiji haramu kwa mujibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, hadi jana wahamiaji 465 kutoka mataifa 17 wakiwamo walimu wanaofundisha shule za michepuo ya Kingereza wamekamatwa.

Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Hokororo alitaja waliokamatwa kuwa ni Warundi 181, Wakongo 38, Wanyarwanda watano, Waganda 16, Wakenya 38, Wapakistani sita, Wasomali 28, Wanigeria 12, raia wanane wa Msumbiji, 114 wa Malawi, wawili wa Cameroon na 10 wa India.
Aidha, walikamata raia watatu wa Uturuki, watatu wa Comoro, mmoja wa Afrika Kusini, mmoja wa China na mmoja wa Burkina Faso.

Alisema wahamiaji hao wengi wao ni vijana na wamekuwa wakijifanya walimu wa shule za michepuo ya Kingereza, lakini hawana taaluma hiyo, isipokuwa wanakijua Kingereza na wengine ni wauza kahawa, wafanyakazi wa ndani, walinzi, watunza bustani, wauza matunda na maji. --- HabariLeo, JUMAPILI

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. TANGA LEO - All Rights Reserved
Proudly powered by Blogger