Dawa ya mifugo yatengenezea gongo Dar
Wakati
Serikali ikiahidi kuongeza nguvu katika vita dhidi ya wauza dawa za
kulevya nchini, imebainika kuwa kuna mtandao wa wafanyabiashara wa pombe
haramu ya gongo unaopika na kuichanganya na dawa za mifugo ili
kuiongezea ukali.
Mtandao
huo unaomiliki mitambo ya kupika gongo katika eneo la Mto Kizinga uliopo
Dambweni, Kata ya Kilungule, wilayani Temeke, unadaiwa kuchanganya
pombe hiyo na dawa ya mifugo aina ya Multivitamin ambayo hutumika
kurutubisha wanyama.
Wafanyabiashara hao wamekuwa wakipika
gongo hiyo katika eneo hilo kwa miaka zaidi ya 10, huku baadhi ya
viongozi wa serikali ya mtaa wakitajwa kuwalinda.
Kwa
mujibu wa uchunguzi, eneo hilo lina mitambo zaidi ya minne ya
kutengeneza gongo na kila mtambo unazalisha pipa moja lenye ujazo wa
lita 200.
Uchunguzi
ulibaini kuwa kila siku wanazalisha zaidi ya lita 800 za gongo ambayo
huuzwa kwa rejareja na jumla. Bei ya rejareja kipimo kinaanzia Sh500
hadi Sh5,000, ambapo bei ya jumla ni Sh38,000 kwa ndoo yenye ujazo wa
lita 20.
Kwa mtu
anayefika kwa mara ya kwanza eneo hilo atakutana na makundi ya watu
wakiwa chini ya miti wakijipumzisha wakati wakisubiri pombe hiyo kuwa
tayari, huku wakazi wengine wa eneo hilo wakionekana kuendelea na
shughuli zao kwenye bustani za mboga za majani zilizolimwa kando kando
ya mto.
Mbali ya
kuwa wanalindwa na baadhi ya viongozi wa mtaa, wameweka ulinzi wao
wenyewe, kwa kuweka vijana zaidi ya 10 ambao hukaa katika eneo hilo
kuhakikisha kuwa mtu anayefika katika eneo hilo wanamtambua.
Ukifika
katika eneo ilipo mitambo yao, watu wanaofanya kazi ya kupika ni
wacheshi, wanaojaribu kumsalimia kila mpita njia bila ya kuwa na hofu
yoyote, huku mmojawao ambaye jina lake halikufahamika mara moja akisema
kuwa wao ndio waliotengeneza barabara ya kupita magari inayoingia sehemu
hiyo.
Mkazi
mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa
kuhofia usalama wake, alisema watu hao ndiyo wasambazaji wakubwa wa
gongo jijini Dar es Salaam.
"Biashara
hii inalipiwa 'kodi' kila mwezi, hawa jamaa huchangishana fedha halafu
huwapelekea baadhi ya askari ambao huwalinda wasikamatwe, kuna wakati
huchanga hadi laki tatu. Vigumu sana kukamatwa," alisema.
Gongo
inavyotengenezwaUchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini pombe hiyo
inatengenezwa kwa kutumia malighafi mbalimbali ikiwamo mapapai
yaliyooza, vitambaa vichafu vilivyovunda, mihogo na wakati mwingine
kinyesi cha binadamu hasa wakati bidhaa nyingine zinapoadimika.
Mfanyabiashara
mmoja (jina linahifadhiwa) alisema amekuwa akipika gongo na kuigawa
katika madaraja matatu; iliyopikwa kwa mapapai yaliyooza ndiyo
inayopendwa zaidi na wateja wake ikilinganishwa na iliyotumia malighafi
nyingine.
"Sisi
tunatumia mapapai yaliyooza, tunaongeza na sukari pamoja na hamira,
ikishaiva tunaitenga kutokana na madaraja yake. Gongo ya eneo hili
inasifika sana kwa sababu ya ubora wake, hatuna tatizo la ukosefu wa
maji kama walilonalo wenzetu ndiyo maana unaona tunaung'ang'ania huu mto
hapa," alisema na kuongeza :
"Kama mapapai yakiadimika sana, tunaweza kupika kwa kutumia vitambaa vichafu au mihogo."
Akifafanua
alisema wamekuwa wakitembea kwenye madampo kuokota vitambaa pamoja na
takataka nyingine, kisha huziloweka kwenye maji kwa muda mrefu hadi
zivunde ndipo huwa tayari kwa kupikia gongo.
Uchunguzi
uliofanywa unaonyesha kuwa mbali ya pombe hiyo kutengenezwa kwa kutumia
takataka zinazookotwa kwenye madampo, pia huongezewa ukali kwa kutumia
dawa za kuongezea vitamini mifugo.
Mteja
mmoja wa pombe hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Sadick,
alisema gongo inayopikwa eneo hilo imekuwa maarufu kwa kuwa kuna dawa ya
mifugo ya Multivitamin ambayo huongezwa baada ya pombe hiyo kuiva.
"Mimi
ninafahamu kuna dawa ya mifugo inawekwa kwenye hii gongo ili kuiongezea
nguvu. Sijui ni dawa aina gani, lakini kuna jamaa huwa namwona anakuja
kuuza hiyo dawa. Gongo iliyowekwa hiyo dawa inakuwa na nguvu
sana,"alisema Sadick.
Mtaalamu
wa Mifugo, Joseph Nong'ona alisema wanywaji wa pombe hiyo wapo katika
hatari ya kudhurika kiafya kwa kuwa dawa ya Multivitamin inayotolewa kwa
wanyama ina nguvu zaidi ikilinganishwa na ya binadamu, na kwamba mtu
haruhusiwi kunywa maziwa au nyama ya mnyama aliyepewa dawa hiyo kwa siku
tatu.
"Multivitamin
anayopewa mnyama ina 'concentration' kubwa ikilinganishwa na ile ya
binadamu, lakini pia ikumbukwe kuwa ile ni kemikali sijui inakuwaje
inapochanganywa na gongo ambayo yenyewe tu ina madhara makubwa kiafya.
Kwa kawaida mnyama akipewa dawa hiyo huwa tunashauri asikamuliwe mazima
au nyama yake isitumike kwa siku tatu," alisema Nong'ona.
Akizungumzia
biashara hiyo, Katibu wa Mtaa wa Kilungule, Juma Ahmed aliwatetea
wafanyabiashara hao kwa madai kuwa hajawahi kupata taarifa zozote za
kufanya uhalifu badala yake wamekuwa walinzi wa amani katika mtaa
huo."Ni watu wazuri sana, sijawahi kusikia wamefanya jambo lolote baya,
kwanza wamegeuka kuwa walinzi wa amani hapa mtaani kwetu... wanajua
biashara wanayoifanya siyo halali kwa hiyo hawataki matatizo na mtu,"
alisema Ahmed.
Kamanda
wa Polisi wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema suala la biashara ya gongo
linatakiwa kudhibitiwa na jamii inayowazunguka wafanyabishara hao kwa
kutumia ulinzi shirikishi"Wanataka kuipa Polisi kazi bure tu, jamii
ndiyo inayohusika na suala hilo. Serikali ya mtaa kwa njia ya ulinzi
shirikishi wanaweza kuamua kwenda kuvunja mitambo ya gongo," alisema
Kiondo.
Akizungumzia
tuhuma kuwa baadhi ya Polisi wanawalinda wafanyabiashara wa gongo,
Kiondo alisema tuhuma hizo zimekuwepo muda mrefu na kwamba zimeshapitwa
na wakati.
CHANZO MWANANCHI.
Post a Comment