WAKATI
Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa asaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 ili iwe sheria, viongozi wa
upinzani nchini wameamua kuanza mchakato wa kumn
g’oa kiongozi huyo, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.
Wenyeviti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, Profesa
Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), leo wanatarajia
kukutana na wahariri na waandishi wa habari kueleza mikakati na mbinu
watakazozitumia kunusuru taifa lisiingie kwenye utungaji wa Katiba mpya
itakayobeba masilahi ya chama tawala.
Tanzania
Daima Jumapili limedokezwa kuwa mikutano ya hadhara, maandamano na
elimu kwa umma juu ya athari ya muswada huo ni miongoni mwa mbinu
zitakazotumiwa kuhakikisha Rais Kikwete hasaini muswada huo au serikali
inapeleka tena mabadiliko ya sheria hiyo katika Bunge lijalo iwapo rais
atasaini.
Wapinzani
wanadai kuwa serikali iliubadili kwa nguvu muswada huo kwa kuondoa
maoni muhimu ya wadau, pia walilalamikia kitendo cha wajumbe wa Kamati
ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge kutokwenda Zanzibar kuchukua maoni
ya upande huo wa muungano.
Wakati
wapinzani wakijipanga kuweka wazi mikakati ya kumshinikiza Rais Kikwete
asisaini muswada huo, wadau mbalimbali wamemtaka kiongozi huyo atumie
busara ili taifa lipate katiba itakayokuwa na manufaa kwa taifa kuliko
inavyoonekana itikadi za vyama kugubika mchakato huo.
Wiki
iliyopita akiwa Dodoma, Mbowe alikionya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa
wasitarajie kuwa kupitishwa kwa marekebisho ya muswada huo ndiyo Katiba
mpya, bali kura ya maoni ndiyo itakayoamua jambo hilo.
Tanzania
Daima Jumapili imedokezwa kuwa wapinzani wamejipanga kuhakikisha
wananchi wanaitumia kura ya maoni kupinga mpango wa Rais Kikwete na
serikali yake kupitisha Katiba mpya yenye mwelekeo wa kukibeba chama
tawala.
Hoja za wapingaji
Kamati
Maalumu ya Katiba, nayo imepinga marekebisho ya muswada huo ikiainisha
eneo mojawapo lenye tatizo ni kuruhusu asilimia 72 ya wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba kubeba wanasiasa.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Dk. Khoti Kamanga, alisema iwapo Katiba mpya itaundwa
bila upungufu unaoonekana sasa kupatiwa ufumbuzi itazalisha migogoro
zaidi, itakayosababisha nchi kuingia kwenye machafuko.
Alikosoa
Kifungu cha 8 na Kifungu kidogo cha 4 na 5 cha muswada huo kwamba vina
kasoro, kwa kuruhusu wabunge wa Bunge la Katiba kufanya uamuzi kwa wingi
wa kura badala ya kutumika utaratibu wa theluthi mbili kutoka Zanzibar
na Tanzania Bara.
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, naye anapinga muswada huo kwa madai
kuwa una upungufu mkubwa, ukiwamo wa Zanzibar kutoshirikishwa, pia kumpa
nafasi kubwa rais kuteua watu kutoka katika asasi mbalimbali badala ya
watu hao kuteuliwa moja kwa moja na asasi au asasi husika.
Hofu ya yaliyotokea Kenya
Baadhi
ya wachambuzi wa masuala ya siasa wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili
kuwa Tanzania inafuata njia iliyopitwa na Kenya katika kupata katiba
mpya, ambayo ilipatikana baada ya kutokea machafuko mwaka 2007 mara
baada ya kufanyika uchaguzi mkuu.
Mwaka
2005, wananchi wa Kenya wakiongozwa na wanasiasa maarufu, Raila Odinga
na Kalonzo Musyoka, waliibwaga serikali ya rais mstaafu wa nchi hiyo,
Mwai Kibaki, katika kura ya maoni ya kuamua kuikubali au kuikataa rasimu
ya katiba iliyokuwa imependekezwa na utawala wa rais Kibaki.
Ni
kutokana na matokeo ya kura hiyo, uchaguzi mkuu wa 2007 ulizaa
machafuko na mauaji ya mamia ya Wakenya wasiokuwa na hatia, baada ya
kushindikana kupatikana kwa katiba mpya, hivyo utawala wa Kibaki kuamua
kuitisha uchaguzi mkuu kwa kutumia katiba na sheria za uchaguzi za
zamani zilizokuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu.
Wachambuzi
wa siasa hapa nchini wanasema kuwa mwenendo wa hivi karibuni wa
mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Tanzania unaonesha ishara za wazi za
kutokea yaliyotokea nchini Kenya. Kwamba, kushindwa kufikia mwafaka
baina ya wabunge wa Bunge la Tanzania lililomaliza vikao vyake hivi
karibuni mjini Dodoma, kuhusu muundo wa Bunge Maalumu la Katiba ni
uthibitisho wa wazi wa matatizo yanayoweza kutokea siku za usoni.
Bunge
Maalumu la Katiba ndilo litakaloandaa rasimu ya mwisho ya Katiba mpya
itakayopelekwa kwa wananchi mapema mwakani kwa ajili ya kura ya uamuzi,
hivyo muundo wake na kukubalika kwake ni jambo muhimu na linalohitaji
mwafaka wa kitaifa.
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA ilipeleka mapendekezo
ya kutaka uwakilishi wa Bunge hilo upanuliwe kutoka wajumbe 600 wa sasa
na kuwa wajumbe 789 ili kulifanya bunge hilo lisihodhiwe na wanasiasa
ambao zaidi ya asilimia 70 ni wanachama wa CCM.
Hata
hivyo, pendekezo hilo lilishindwa baada ya wabunge wa CCM kutumia wingi
wao katika Bunge hilo kuyakwamisha mapendekezo ya upinzani na badala
yake kuamua kuendelea na muundo wa sasa unaoipa CCM haki ya kisheria ya
kulihodhi Bunge la Katiba.
Wachambuzi
hao wanatabiri kuwa kama Rais Jakaya Kikwete atakubaliana na msimamo wa
wabunge wa chama chake, kwa kuitia saini sheria ya marekebisho ya
sheria ya mabadiliko ya katiba na hatimaye kuwa na Bunge la Katiba na
baadaye kura ya maoni, basi kuna uwezekano katiba hiyo mpya ikakataliwa
na wananchi katika kura ya maoni kama ilivyokuwa kwa Kenya mwaka 2005.
Kwa
mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya 2011, kama wananchi
wataikataa katiba inayopendekezwa, basi katiba ya zamani itaendelea
kutumika katika shughuli zote za nchi, ikiwamo kuendesha Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015, jambo ambalo linapingwa vikali na viongozi, wanachama,
wafuasi wa vyama vya upinzani na wanaharakati.
Ni
kutokana na mazingira haya wachambuzi wa masuala ya siasa nchini
wanaamini na kutabiri kuzuka kwa ghasia, machafuko na umwagikaji wa damu
kama ilivyotokea Kenya mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Mhadhiri
Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Bashiru Alli, anasema: “Tunakabiliwa na hatari mbele yetu, maana
tunakwenda kwenye kura ya maoni kuhusu Katiba mpya tukiwa tumemeguka
vipande vipande. Tulipaswa kufika huko tukiwa wamoja kama taifa,
tulipaswa kuwa na mwafaka wa kitaifa katika suala hili la katiba ya nchi
badala ya kwenda kwa kuongozwa na itikadi zetu za kisiasa,” alieleza
Bashiru na kuongeza:
“Machafuko
na mauaji yaliyotokea Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 yalitokana
na makosa ya utawala wa rais mstaafu wa nchi hiyo, Mwai Kibaki, ambaye
aliamua kuwadharau na kuwapuuza wananchi katika mchakato wa kuunda
katiba ya nchi yao kama inavyofanyika sasa nchini mwetu, hili ni jambo
la hatari sana,” alionya Bashiru.
Bashiru
anasema kuwa ili kuufanya mchakato wa sasa wa Katiba mpya kuwa wa
wananchi na kuepusha kuiingiza nchi kwenye machafuko na mauaji ya
wananchi wasio na hatia, mchakato wote unapaswa kurudiwa.
“Ili
yasitufike yaliyotokea Kenya, tunapaswa kuanza upya mchakato wa Katiba
mpya, wananchi wapewe fursa ya kuumiliki mchakato mzima. Kwa mfano,
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanapaswa kuchaguliwa na wananchi, si
kuteuliwa. CCM na wapinzani wanataka wajumbe wapatikane kwa kuteuliwa,
mimi nasema huo si utaratibu sahihi, dhana ya Bunge la Katiba inataka
wajumbe wake wapatikane kwa kuchaguliwa na wananchi, si kuteuliwa,”
anabainisha Bashiru.
Ulivyopitishwa
Mjadala
wa muswada huo uliopitishwa Ijumaa iliyopita na wabunge wengi wakiwa wa
CCM, ulizua tafrani bungeni iliyosababisha Kiongozi wa Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
(CHADEMA) kutolewa nje na askari. Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge
wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote
wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema,
wakiususia. TANZANIA DAIMA.
Post a Comment