MKUU wa shule ya Sekondari ya Kwamatuku, iliyopo Kata ya
Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani
Tanga, Faustine Mroso, amesema pamoja na changamoto wanazokutana nazo, lakini
shule yake imejipanga imara kuwapatia wanafunzi elimu bora.
Mroso ameyasema hayo siku chache baada ya kuwa na malalamiko
kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne, waliotia hofu ya ufindishwaji
katika shule hiyo.
Akizungumza na Handeni Kwetu Blog, Mroso alisema kuwa si
kweli kama shule yake haifundishi vizuri, hivyo wanafunzi hao waendelee
kujiandaa kwa kusoma kwa bidii, huku uongozi wa shule yake ukiwa umejipanga
imara kuwaandaa wanafunzi hao.
Alisema shule yake ilikaguliwa mapema mwaka huu na kuonekana
ina mipango kabambe yenye maendeleo ya kielimu, hivyo kinachosemwa dhidi ya
wanafunzi hao si kweli.
"Mimi katika shule hii
si mwenyeji, maana nimekuja mapema mwaka huu, hivyo naomba wanafunzi wanipe
ushirikiano kwa lolote linalotokea kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanajiandaa
vizuri kwa ajili ya kupata matokeo mazuri,” alisema Mroso.
Kwa mujibu wa Mroso, shule yake ina uongozi mzuri pamoja na
mipango ya kuwaandaa vyema wanafunzi, ikiwa ni njia nzuri ya kuhakikisha kuwa
wanakuwa katika nafasi nzuri.
Awali, baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne katika shule
hiyo walilalamikia uongozi wa shule kwa madai kuwa ufindishwaji wao si mzuri na
unaweza kuwaweka katika nafasi mbaya kwenye mitihani yao ya kidato cha nne
baadaye mwaka huu.
Chanzo; Handeni kwetu.
Post a Comment